Unaweza kusoma sehemu ya kwanza hapa: https://creativewritersleague.co.ke/wasia-sehemu-ya-1/
Mfalme akawaita na kuwaambia, “nimewakaribisha vizuri na kuwakirimu kisha mwatukana ukarimu wangu? Haya niambieni, wali wangu una kasoro gani, na mbuzi wangu ana kasoro gani na mimi mwenyewe nina kasoro gani?” Kabla hawajibu akatokea mtu wa kwanza waliekutana nae njiani.
Baada ya salamu, yule mtu akasema, “bwana mfalme, hawa vijana wameniibia ngamia wangu!” Mfalme akashtuka na kuwauliza, ” kwa nini mumemuibia ngamia wake?” Wote wakakataa na kusema kuwa hawajaiba ngamia na isitoshe wao hawakumuona kamwe huyo ngamia wake. Mwenye ngamia akasema, “mbona mumenipa alama kamili za ngamia wangu?” Mkubwa akasema, “mimi nilisema kuwa ngamia mwenyewe ni mkubwa kwa sababu niliona ukubwa wa alama za kwato zake.” Wa pili akasema, “mimi nilisema kuwa ngamia mwenyewe alikuwa amebeba vyuma vizito kwa sababu niliona kuwa alama za kwato zake zimeingia sana mchangani.” Wa tatu akasema, “mimi nilisema kuwa ngamia mwenyewe hakupita kitambo kwa sababu alama zake hazikuwa zimefinikwa na mchanga.” Mfalme akasema, “haya bwana umesikia, hawa hawakumchukua ngamia wako. Nenda ukamtafute kwengine.” Yule bwana akaenda zake.
Kabla mfalme hajawauliza chochote akaingia yule mtu wa pili waliyekutana nae njiani. Baada ya salamu yule mtu akasema, “bwana mfalme hawa vijana wameniibia mke wangu!” Mfalme akawauliza, “haya, kwa nini mumemuiba mke wa mwenyewe?” Wote watatu wakakana kwa pamoja kuwa hawakumuiba mtu yeyote na wala hawakukutana nae kamwe. Yule bwana akawauliza, “na mbona mumeweza kunipa alama zake zote?” Yule mkubwa akasema, ” mimi niliona ukubwa wa alama ya kitako iliyo onesha kuwa palikaa mtu mkubwa sehemu hiyo ndio nikasema kuwa aliyekaa pale alikuwa na mwili mkubwa.” Wa pili akasema, “mimi nilisema kuwa kitako chenyewe ni cha mwanamke kwa sababu niliona palikuwa na ushanga aliousahau.” Wa tatu akasema, “mimi nilisema kuwa alikuwa na mtoto kwa sababu ilionesha wazi kuwa alivua ule ushanga kwa madhumuni ya kumpa mwanawe achezee la sivyo asingeuvua.” Mfalme akasema, “haya bwana, umesikia. Hawa hawajamuiba mkeo. Nenda kamtafute kwengine.” Yule mtu akatoka akaenda zake.
Kabla mfalme hajasema chochote akaingia yule mtu wa tatu waliyekutana nae njiani. Baada ya maamkuzi yule mtu akasema, “bwana mfalme, hawa watatu wameniulia babangu!” Mfalme akashtuka na kuwauliza, “haya semeni, kwa nini mumeua?” Wote watatu kwa pamoja wakakana kumuua babake yule mtu. Nae akawauliza, “na ni vipi muliweza kunipa alama zake zote?” Mkubwa akasema, “mimi niliuliza aina ya nguo alizovaa kwa sababu ndizo nilizomuona nazo.” Wa pili akasema, “mimi niliuliza kama ana masharubu kwa sababu niliona alikuwa na nywele za kifuani,na kawaida mtu mwenye nywele za kifuani hakosi masharubu usoni.” Wa tatu akasema, ” mimi niliuliza kama alikuwa mtu wa makamo kwa sababu niliona damu iliyomtoka ilikuwa majimaji kuonesha kuwa alikuwa amekaribia utu uzima.” Mfalme akasema, “haya bwana, pole sana kwa kuuliwa babako lakini sio hawa waliomuua.” Yule mtu akatoka na kwenda zake.
Kisha mfalme akawageukia na kumuuliza yule mkubwa, ” sema sasa, ni kwa nini umesema kuwa wali wangu una walakin?” Yule kijana akasema, “ni kwa sababu, mpunga wake umevunwa kutoka kwenye makaburi.” Wakati huohuo mfalme akamuita aliyevuna mpunga ule nae akathibitisha kuwa ni kweli umevunwa makaburini. Mfalme akamwambia yule kijana mkubwa akae kando kwani kesi yake ilikuwa imeisha.
Kisha akamuuliza yule wa pili, “na wewe kwa nini umesema kuwa mbuzi wangu ana walakin?” Yule kijana akajibu, “ni kwa sababu mbuzi mwenyewe alipozaliwa mamake alikufa kwa hivyo yeye akanyonyeshwa na punda.” Mfalme akamuita mfugaji wake nae akathibitisha kuwa yale maneno yalikuwa ya kweli. Huyu nae akaambiwa akae kando kisha mfalme akamgeukia kitinda mimba na kumuuliza, “enhe, kwa nini umesema kuwa mimi nina walakin?” Yule kijana akasema, “ni kwa sababu mtu hurithi ufalme kutoka kwa babake lakini wewe babako hakuwa mfalme. Aliyekuwa mfalme ni ammi yako, na wewe ulipewa cheo hiki kwa ulaghai.” Mfalme akashangaa, kisha akaagiza mamake aitwe. Alipokuja akatisha kumuua kama hatosema ukweli. Ndio mamake akakiri kuwa babake mfalme alimuua ndugu yake aliyekuwa mfalme kisha akauchukua yeye kwa nguvu na ndio mfalme akaja kuurithi.
Mfalme akalia kwa kuwekwa gizani kuhusu suala hili. Kisha akaagiza wale vijana wakusanyiwe mali kila mtu fungu lake waweze kurudi kwao. Wakafanyiwa kama mfalme alivyoagiza.
Wakati wa kuondoka, mfalme akawaambia wanawe watatu wawasindikize wenzao. Watoto wageni walivishwa nguo nyekundu na wa mfalme wakavishwa nguo nyeusi.
Walifika mbali kidogo na wale waliofiwa na babayao wakasema, “sisi tuna msiba wa kufiwa na babaetu kwa hivyo sisi ndio tunastahili kuvaa nguo nyeusi, na nyinyi babaenu yuko hai kwa hivyo mwatakikana muvae nguo nyekundu.” Wale watoto wa mfalme wakaona muna busara ndani ya maneno yao hivyo wakakubali kubadilishana nguo na wale wageni.
Huku nyuma kwa mfalme, mfalme alikuwa ameghadhibishwa sana na tabia za wale vijana kumuanikia aibu zake peupe. Akaamuru askari wawafuate nyuma na wawauwe walovaa nguo nyeusi na warudi na wenye nguo nyekundu. Askari walipowafikia wakashangaa kuona ni watoto wa mfalme ndio walikuwa na nguo nyeusi lakini hawakuweza kuipinga amri ya mfalme.
Hivyo basi wakawauwa wana wa mfalme na kurudi na wana wa aliyekuwa mzee maskini. Mfalme alipowaona akaelewa kilichotendeka na akalia sana.
Mwisho akawaambia kuwa wamemshinda kwa ujanja na hapo akaamuru waongezewe katika mali walizokuwa tayari washapewa halafu warudishwe kwao.
Wakawa wamekuwa na mali nyingi kutoka kwa mfalme wa Misri hadi mali ya marehemu babayao haikuwashughulisha.
Hapo ndipo walipoona hekma ya babayao aliposema wakamrithi mfalme wa Misri kwanza.