Kulikuwa na mzee mmoja aliyekuwa mgonjwa na kila akiangalia hali yake aliona umauti umemkodolea macho. Mzee huyu alikuwa na wana wa tatu wa kiume.
Siku moja baada ya kuona hali yake imedhoofu sana akamuita mwanawe mkubwa kwa faragha na kumwambia, “mwanangu, mimi babako hali yangu ni kama unavyoiona. Kaburini kwaniita na akhera kwanipungia mkono. Nendako ni karibu nitokako ni mbali. Sasa akiba nilonayo ni kidogo mno hamtaweza kurithi nyote watatu ikawatosha kwa hivyo mimi nataka nikurithishe wewe pekeyo akiba hii. Nimeificha mahali fulani lakini nikifa usinirithi mpaka ukamrithi mfalme wa Misri.” Yule mtoto wa kwanza akafurahi sana kuwa babake kamchagua yeye kurithi akiba yake.
Siku ya pili, bila ya yule mtoto mkubwa kujua, baba alimuita mwanawe wa pili na kumwambia yale yale maneno aliyomwambia mwanawe wa kwanza na kusisitiza kuwa anamtaka yeye tu arithi lakini asiwaambie nduguze. Na pia kwanza akamrithi mfalme wa Misri kabla kumrithi yeye. Nae pia akafurahi kuona kuwa babake kamchagua yeye kurithi akiba yake.
Siku ya tatu tena yule baba, bila ya wanawe wawili kujua, akamuita mwanawe wa tatu na kumwambia maneno yale yale aliyowaambia wakubwaze. Nae pia akafurahi kuwa babake kamchagua yeye kurithi akiba yake.
Baada ya siku chache, yule mzee akajifia. Watu wakafanya taratibu za mazishi na kumsitiri. Siku iliyofuata yule mtoto mdogo kabisa katika wale ndugu watatu akarauka na kwenda alipoelekezwa na babake akafungua na kuchukua akiba ile. Muda mchache baadae yule mtoto wa kwanza na wa pili wakaenda kwa zamu kuangalia ile amana waliyoambiwa na babayao lakini hawakuikuta.
Wakaanza kuambiana kuwa baba yao alikuwa amewadanganya na hakukuwa na akiba yoyote. Yule mdogo akasikia na kusema kuwa yeye pia aliambiwa maneno kama yao ila yeye tayari alikuwa ashaichukua ile akiba. Hapo nduguze wakamkumbusha kuwa baba yao alikuwa ameusia kuwa wasimrithi mpaka watakapo mrithi mfalme wa Misri. Kwa iyo yule mdogo akakubali kuregesha ile akiba.
Wakaandaa safari na baada ya siku chache wakaanza safari yao ya kuelekea Misri. Ilikuwa ni safari ya mwendo wa miguu kwa iyo walikwenda wakipumzika.
Walipokuwa njiani wakaona alama za kwato za ngamia. Mkubwa akasema, “hizi ni alama za kwato za ngamia.” Wa kati akasema, “ngamia mwenyewe amebeba vyuma vizito” na mdogo akasema, ” ngamia mwenyewe hakupita kitambo.”
Wakaendelea na safari yao na walipofika mbele wakakutana na mtu aliyewauliza kama wamemuona ngamia wake. Mkubwa akauliza, “ngamia mwenyewe ni mkubwa?” Akajibiwa, ndio. Wa kati akauliza, “na amebeba vyuma vizito?” Akajibiwa, ndio. Na mdogo akauliza, ” ngamia mwenyewe hujamkosa kitambo?” Akajibiwa ndio. Wakasema kwa pamoja, “basi tumepishana nae huko nyuma nenda utamkuta.” Yule mtu akaelekea walikotoka.
Baada ya mwendo kiasi walifika mahali wakaona alama ya kitako, kumaanisha kulikuwa na mtu ameketi muda mfupi uliopita. Mkubwa akasema, ” hiki ni kitako.” Wa pili akasema, “kitako chenyewe ni cha mwanamke.” Na mdogo akasema, ” mwanamke mwenyewe alikuwa na mtoto.” Wakaendelea na safari yao.
Walipofika mbele kidogo wakakutana na mtu akawauliza kama wamemuona mke wake. Mkubwa akauliza, “ni mwanamke mzito ivi?” Akajibiwa ndio. Wa pili akauliza, “alikuwa amevaa ushanga shingoni?” Nae pia akajibiwa ndio. Wa tatu akauliza, “alikuwa na mtoto?” Pia akajibiwa ndio. Wakasema kwa pamoja, “tumepishana nae huko nyuma nenda utamuona.”
Baada ya mwendo tena wakakuta mtu ameuwawa kwa kuchinjwa na kichwa hakikuwepo pale. Mkubwa akasema, ” hii ni maiti ya mwanamume.” Wa pili akasema, “mwanamume mwenyewe alikuwa na masharubu.” Wa tatu akasema, “mwanamume mwenyewe ni mtu wa makamo.” Wakaenda mbele na kukutana na barobaro mmoja akawauliza, “mumenionea babangu huko mtokako?” Mkubwa akauliza, “amevaa nguo fulani?” Akajibiwa ndio. Wa pili akauliza, ” babako ana masharubu, sio?” Akajibiwa ndio. Na wa tatu nae akauliza, “ni mtu wa makamo?” Akajibiwa kuwa ndiye haswa! Wakasema kwa pamoja, “tumepishana nae huko nyuma nenda utamuona.”
Baada ya muda mfupi wakawasili nyumbani kwa mfalme walikokuwa wanaelekea. Mfalme akawakaribisha vizuri kisha wakajieleza wao ni kina nani na kuwa baba yao amekufa juzi tu. Mfalme akaamrisha waandaliwe chakula wale.
Muda mfupi baadae wakaitwa katika chumba kimoja kwa ajili ya chakula. Walikuwa wameandaliwa wali na nyama ya mbuzi. Mkubwa akasema, “huu wali una walakin (kasoro)”. Wa pili akasema, ” huyu mbuzi ana walakin” na wa tatu nae akasema, “mfalme mwenyewe ana walakin.” Mlinzi aliyekuwa karibu akawasikia na kwenda kumwambia mfalme.
Mfalme akawaita na kuwaambia, “nimewakaribisha vizuri na kuwakirimu kisha mwatukana ukarimu wangu? Haya niambieni, wali wangu una kasoro gani, na mbuzi wangu ana kasoro gani na mimi mwenyewe nina kasoro gani?” Kabla hawajibu akatokea mtu wa kwanza waliekutana nae njiani.
_itaendelea_