Alfajiri ya jumatatu,mwezi wa kenda, mwaka wa elfu mbili na ashara, kaski iliyongojewa kwa raghba ya mkanja hatimaye iliwadia. Niliamshwa na sauti tamu na henezi za nyuni waliokuwa wakizighani nyimbo zao za kuongoaongoa kuashiria siku njema. Furaha sufufu ilinitinga si kidogo. Ilikuwa siku ya aina yake kwani nilikuwa najiunga na chuo kikuu cha Jomo Kenyatta mjini Mombasa, naam siku njema huonekana asubuhi.
Kwa hakika ni wanafunzi wachache sana tuliofuzu mtihani wa kidato cha nne ,na kuweza kuendelea na chuo kikuu hapa kijijini Lamu. Msafiri ni aliye bandarini. Hivyobasi, tulijitayarisha wanguwangu na baada ya muda wa bana banua tulifika Jeti, tayari kuingia kwenye mashua itakayotufikisha Mokowe. Bahari ilikuwa imetulia tuli huku ikipeperusha mawimbi yake kiaina ungedhani inanipa hongera na kuniaga. Kwa jinsi nilivyokuwa na furaha,nilihisi kila kitu chenye uhai au kisichokuwa na uhai, kilikuwa kikiwasiliana nami kwa vicheko na tabasamu. Ama kweli,zito hufuatwa na pesi na bidii hulipa. Hatimaye ndoto yangu ilikuwa imetimia.
Baada ya muda wa takriban masaa nane, tuliwasili mjini Mombasa. Nilikuwa pamoja na wanahodari ithineni waitwao Musa na Issa. Sisi ndio tulioongoza mtihani kijijini Lamu. Sote tuliteuliwa kusomea uhandisi ila kwenye nyanja tofauti. Moja kwa moja, tulienda hadi chuoni. Baada ya mwia kichele tulianza hatua za usajili na hatimaye kuorodheshwa kwenye idadi ya wanafunzi wapya waliojiunga na chuo kikuu.
Hewaa, kila mchukuzi huusifu mzigowe. Nami sitochelea kuwasifu mabui wangu wa chanda na pete. Issa, hakuwa mfupi kama nyundo wala mrefu kama twiga. Alikuwa na kijuso kidogo cha mduara mfano wa tungule na macho ya kunasa machozi. Pua yake ilikuwa ndogo na nyembamba ya kitara. Mwenye meno ya mchele na nywele nyeusi tititi. Hata hivyo, kitabia alikuwa mpwamu na mwenye kipawa cha ucheshi. Hakutaka kamwe kuniona nimenuna kwasababu yoyote ile. Kila wakati akiniona sina furaha alifanya juu chini hadi niweze kutabasamu. Wimbo wake kila siku ulikuwa,
“Maisha ni ureda, furahia.”
Hata angekumbwa na tatizo gani, daima yeye yu furahani. Katu usingeweza kumuudhi.
Aidha, Musa naye, alikuwa kijana mmoja mpole sana. Kimaumbile ni mwenye umbo la wastani. Mweupe, kichwani alikuwa na nywele singa na vilevile alikuwa mtanashati mno. Tabia yake ilikuwa ya kupigwa mfano. Alikuwa mkarimu, mpenda watu na pia mwerevu. Walakin, hakuna bamvua lisilo usubi kwani alikuwa na kasoro yake moja tu. Yeye hupandwa na hasira za mkizi. Jambo hili kwa mara kadha lilinitia wasiwasi ila kelele zake za mlango hazikuniasi usingizi.
Masomo yalianza rasmi. Hakuchi kwacha. Pilka za hapa na pale zikazidi. Mara tupo maabarani, mara tupo darasani. Mitihani huku na kule. Kupanda na kushuka. Ghafla muhula unaisha ikifuatiwa na likizo fupi mda mwengine likizo ndefu sana. Lakini undugu wetu haukuwahi kutikiswa na lolote lile. Sisi ndio tulikuwa matumaini makubwa ya watu wa huko kwetu Lamu.
Tulishikana na kusaidiana kila palipostahili usaidizi ili mradi tu kila mmoja afaulu masomoni na pia maishani. Kwa hakika, kwa namna tulivyotunzana, nilihisi ni kama nasoma na kaka zangu wa nina mmoja chuoni.Usingalimuona mmoja wetu akitembea pekeyake. Tulikuwa kama jogoo na koo. Mazoea yalizidi kukua. Ikafikia mwia hatukuweza kukosana. Mchana tulikula pamoja. Maabarani tulikwenda pamoja. Vilevile kusoma wakati wa ziada, pia tulikuwa sako kwa bako.Alhamdulillah! Sote tulikuwa tukiongoza kwenye madarasa yetu.
Kuche kusiche sichi hichi kisichosichiwa. Ghafla bin vuu, tulipofika mwaka wa tatu chuoni, hulka za maswahiba zangu zikaanza kugeuka. Asilimia kubwa ya hadithi zao zikawa ni mambo ya dini. Awali, jambo hili halikunishtuwa kwani, nililitazama kama muelekeo mzuri. Kila kukicha wakawa wanazidi kutoa maelezo ya dini. Mwanzo ilikuwa nikielezwa mimi tu. Lakini ikafikia wakati hata njiani pia waliweza kusimamisha watu wawili watatu, hapa na pale na kuwaeleza machache kuhusiana na mambo ya dini.
Kibao nikageuziwa mie. Waliniamrisha kuvaa mavazi yaliyo na stara kamili. Kamwe wasingekubali kutembea nami iwapo ningevaa mavazi yakunishika mwili, ya rangi zisizoeleweka na yenye kuonyesha mwili.Kufikia hali hiyo, kidogo nilianza kuwa na tashwishi na nikahisi kuchanganyikiwa. Nilishindwa kabisa kutambua sababu za kugeuka kwa Musa na Issa. Hatimaye, walikataa katakata kutembea na mimi, wakisema kuwa mimi ni msichana sipaswi kutembea nao bila kuwepo kwa maharimu yangu. Mapya! Walizidi kunichanganya. Nikawa sijielewi. Sikuwa na mwengine yeyote wa karibu ila wao. Jambo hili lilinidhuru kiakili pia. Ikawa vigumu kwangu kusoma kwa umakini. Nilihisi upweke umenivamia.
Lisilo budi hubidi. Nikajipanga, nikawa mara moja kwa wiki nikiwapitia bwenini kwao kwa azma ya kuwajulia hali. Cha kushangaza, kitambo walikuwa kucha kutwa kwenye siku zisizokuwa na mafunzo, utawakuta wanacheza mchezo uiitwao “FIFA” kwenye vipakatalishi vyao. Nao ulikuwa mchezo wa mpira wa kandanda ila unachezwa kutumia “padi” ukitizamwa kwenye runinga, kompyuta au hata hivyo vipakatalishi. Lakini hii sio hali nilioikuta hapo chumbani kwao. Walikuwa wameshazitupilia mbali ala za mchezo huo na wapo makini wanatizama habari za nchi za kiisilamu zenye vita ulimwenguni. Nilipigwa kibuhuti chakari. Nikafikiri macho yangu yalikuwa yakinichezea shere.
Kisha walinikalisha chini na kunieleza ni jinsi gani waislamu wenzetu wanapata shida nchi nyenginezo ilhali sisi tupo tunastarehe tu hapa Kenya. Wakaniambia kuwa kesho, siku ya hukumu, tutaulizwa ni kwa jambo gani tulifanya kuwasaidia wanyonge hao. Baadaye wakanifungulia vipindi tofauti tofauti vinavyoonyesha mateso na vita vinavyoendelea ulimwenguni wakati huo. Nilipigwa na bumbuazi. Malaika yalinisimama wima kama kondoo mwenye manyoya haba kondeni. Jekejeke la jasho lilimiminika bwaibwai kwenye uti wa mgongo huku nikiwaya kama ndege mso kwao. Kofi la fahamu likanipiga, nikashindwa kunena lolote. Machozi yalianza kunilengalenga . Polepole tu, niliutweka mkoba wangu na kuondoka. Njiani nilihisi kichwa kinataka kupasuka. Mawazo yananisonga. Upande moja nawaza, ni kitu gani kimewakumba rafiki zangu? Upande mwengine nakumbuka zile filamu nilizoonyeshwa, na kujiuliza vipi sikuwahi hata dakika moja kuwaza kuwa wapo wenzangu wanaishi kwenye mapango wakiogopa kurepuliwa. Wapo walio mbioni na familia zao kukimbia mateso ya maadui yao. Yaani, hivi mna watu hata wamesahau ladha ya chakula? Wanaishi kwenye hofu. Hawana amani.
Kwa mara ya kwanza maishani, nilitamani ardhi ipasuke inimeze mzimamzima. Hilo lilikuwa swali nyeti. Nisingeweza kujadiliana na mtu yeyote. Sikujuwa pakuelekea. Niliogopa hata kuwaona kwa mara nyengine marafiki hao. Nilikimbilia nyumbani kwangu. Nikajifungia. Sikutaka mawasiliano na yeyote. Ulikuwa wakati mgumu sana, kwani wiki iliofuatia tulikuwa na mtihani. Hatua ya kwanza niliyochukuwa nikuwaepuka maswahiba hao kwa kadri nilivyoweza. Japo ilikuwa jambo gumu kufanza. Walakin, ili nisikorogeke zaidi, ilibidi. Wakati wa mtihani ulipofika ,alikuja mmoja tu. Musa hakutokea. Siku ya pili yake,wote wawili hawakuja kutekeleza wajibu.
Siku ya mwisho ya mitihani, wanafunzi wote walikuwa na mtihani mmoja sawia uliotarajiwa kufanywa saa nane. Nao ulikuwa mtihani wa somo la mawasiliano. Asubuhi , nilikusanya virago vyangu, kwani baada ya mtihani huo kila mmoja alitakiwa aondoke bwenini. Baadae, nikamalizia kupitia sehemu nisizozielewa kwa mara ya mwisho na hatimaye kuenda kwenye chumba cha mtihani. Mda wote huo wa mtihani sikuwa sawa. Mawazo mengi yalinisumbua. Mara kwa mara ungenikuta ninalia. Kila baada ya mtihani, nilikuwa nikienda bwenini kwa kina Issa lakini hawakuwepo.
Saa nane adhuhuri, ukumbi wa mtihani ulikuwa kimya. Kila mmoja akisubiri mtihani huo kwa hamu na ghamu. Ikapita nusu saa, mhadhiri hakutokea. Halikuwa jambo la kawaida. Wakati ulizidi kusonga. Hakukuwa na dalili yoyote ya mhadhiri kuja. Maongezi ya hapa na pale yalianza. Malalamishi yakaanza kusikika kutoka pembe tofauti za ukumbi ule. Mara ghafla tu, aliingia mhadhiri huku ameshikiliwa ukosi wa shati lake na bonge la mtu. Jitu hili lilikuwa limeshika bunduki. Uso wake ulifinikwa na kitambara cheusi kilichoacha upenyo wa macho na mdomo tu. Niliyoyaona sikuweza kusadiki hata chembe. Nikabanwa na kiwewe kisicho na kipimo wala mizani. Nduru zikaanza, kila moja alikimbilia madirisha ya ukumbi ule. Wengine wakiangukiana na wengine wakiweza kutoka. Mara tu, ikaingia mijitu mingine mitatu kama lilivyo lile kwanza.
“Kila mmoja chini! Nasema kila mmoja chini!” alisema mmoja wao.
Mimi nilikuwa chini hata kabla amri hiyo itolewe. Vilio vikaanza, wengine walizirai na wengine walikaa kimya tu. Wengi wetu walikuwa wakitamka kalima ya dini ya mwisho (shahada) kwani bila shaka huo ulikuwa mwisho wetu. Kwa mara ya kwanza nikaskia mlio wa bunduki. Niliweweseka na kutukutika kwa hofu na hawafu. Hapo kwa hapo nilijikojolea. Sidhani kama nilikuwa pekeyangu niliyefanya shughuli hiyo, maana mitiririko ya mikojo ilionekanwa ikitunga mitaro. Mmoja wao alianza kuzungukazunguka na kuhakikisha hakuna mtu anashika simu yake. Akasimama Yusuf, mwanafunzi mmoja kiherehere sana. Kabla hata hajakienua kinywa chake kutamka neno, alinyakuliwa na mauti. Risasi ilirushwa moja kwa moja hadi kwenye kichwa chake. Damu ilitawanyika kwenye sakafu ya ukumbi huo ungedhani ni rangi inapakwa upya. Kijasho chembamba kilitoka kwapani nikabaki nasaga meno.
Kisha, akaingia mwengine na kuwaita wenziwe. Wakaonekana wanajadiliana jambo kwa siri ila ungeona wazi hakukuwa na maelewano. Akatoka mmoja kwenye mkutano huo na kuenua bunduki yake. Moja, mbili, tatu, akaanza kuwauwa wanafunzi walioko kwenye mstari wa mbele huku akiendelea. Wengine wakimzuia. Nilikuwa kwenye mstari wa nne, sio mbali sana na mauti yangu. Nilishindwa kabisa kutizama kinachoendelea. Mshindo wa bunduki uliondelea kusikika. Wengine waliamua kujaribu kukimbia lakini wapi. Hali ya taharuki ilizidi. Ghafla wawili wao walisonga kando na kuzungumza. Kasha wakatutizama kama ambao walikuwa wakitafuta mtu. Kwa haraka, mmoja wao alinijia. Macho na meno yake hayakuwa mara ya kwanza mimi kuyaona. Umbo la jitu hili lilikuwa ni kama nalifahamu vizuri. Machon lilikuwa linatokwa na machozi. Nilichanganyikiwa. Nikamtizama tena ila sikuwa na muda wa kufikiria wala kusema lolote Macho yalinitoka huku machozi yakitirika. Mauti yamenifikia. Ama kweli maisha ni mafupi. Kwa haraka nikafunga macho yangu ili nisione risasi ile itatokea wapi. Buum! kila kitu kilikuwa giza. Sauti zile nilizisikia kwa mbali sana. Sikujua kilichoendelea baada ya hapo.
Masaa kadhaa yalipita. Kisha nikaanza kuuhisi mwili unasongea.
“Kwani sijafa?” nilijiuliza.
Kichwa kilikuwa kizito kidogo. Nikaanza kusikia sauti zile za fujo tena. Nikifungua macho nilijikuta ndani ya kabati la vitabu lilioko kwenye ukumbi huo. Nikajitazama mwili mzima, sikuamini bado nilikuwa hai. Nilijaribu kufungua mlango wa kabati lile, ukakataa. Kumbe ulikuwa umefungwa na nje. Nikachungulia kwa upenyo wa mlango ule. Loh! Sakafu nzima ilikuwa nyekundu. Miili ya wanafunzi ilikuwa ikiolea kwenye damu. Nilibaki kimya kama maji mtugini. Mwili mzima ulitetemeka temtem. Sikujua yalipita masaa ngapi ila njaa nayo ilikuwa imenikolea. Mlikuwa na mikoba miwili ndani ya kabati lile. Nilifungua na kupata vitabu vitatu na mafuta ya mwilini. Bila kupoteza mda, nilianza kuyala mafuta yale kwa pupa sana. Nikabakisha kidogo kwani sikufahamu maisha yale ya kabatini yalikuwa ya siku ngapi. Kimya kilitanda kote. Usiku ukaingia. Nje kulikuwa na mijitu ile imelala. Nami pia japo kwa taabu nikalala mle ndani hadi kulipokucha.
Asubuhi changa niliamshwa na harufu za najisi. Nilichukua mkebe wangu wa mafuta na kula staftahi. Siku ikaendelea vivyo hivyo kwa ukimya na hofu. Jioni, nilisikia mlango ukifunguliwa. Nikaamshwa kutoka usingizini. Ilikuwa mapolisi. Ving’ora vya magari yao vilisikika kwa wingi. Waliniuliza maswali mingi si haba ila hakuna hata neno moja lilitoka mdomoni mwangu. Nilikuwa nawatazama tu. Wakanitoa kabatini mle kutumia nguvu maana sikuwa nataka kabisa kutoka kule. Nilidhani ni kama matukio yale maovu yalikuwa yakiendelea. Wakanifunika na gubigubi na kunitoa nje.
Nje, niliona wazazi, wanahabari na mapolisi wengi sana. Wazazi wangu wakajitokeza na kunikumbatia huku wakilia. Nikapelekwa kwenye hazanati iliyo karibu. Baada ya muda wa mwezi hivi, ndipo nilipoanza kutamka maneno kidogo kidogo. Chuo kilifungwa rasmi. Sikuwahi kuwaona tena maswahiba zangu Musa na Issa.kila mmoja alikuwa na hadithi tofauti ya kuwahusu. Uchunguzi ukaanza kufanywa ila hatima ya uchunguzi huo sikujuwa ulikuwa vipi. Niliugua kwa mda wa mwaka mmoja kwahiyo ilinibidi nisimamishe masomo yangu. Hata nilipopata shufaa nilikataa katakata kurudi chuo hicho. Nikaendelea na masomo yangu kwenye shule ndogo mjini Lamu hadi nilipomaliza. Swali ambalo hunisumbua sana hadi wa leo ni, ni kweli wale wawili waliokuwa kando kisha mmoja akanijia na kunitia kabatini, walikuwa Issa na Musa? Ama kweli, ulimwengu kigeugeu.