Alitoka chumba hiki akaingia chumba kingine.Alizipanda ngazi akizishuka Kama asiyekuwa na akili nzuri.Alipiga usiahi wa ndani kwa ndani kwa uchungu mkali aliokuwa akiuhisi.Milio ya risasi nje haikumtia kimbimbi kwani alikuwa ameizoea hadi ya kuizoea.Kwake ilikuwa Kama milio ya vyuma vya kawaida au watoto wachanga wanaolia.Hatimaye Saida alijifungia na kwa bahati nzuri mpangaji na rafiki yake wa siku nyingi alitokea na kumsaidia katika harakati zote za uzalishaji ingawa kwa Saida halikuwa jambo jipya.Mara nyingi alijifungua bila kupata msaada wa mtu yeyote isipokuwa mumewe ambaye kwa sasa hivi ni marehemu aliyeuliwa kwa mtutu was bunduki miezi miwili iliyopita.
“Huyu mtoto namuita Salim.” Alisema Saida baada ya kujifungua salama wa salmini.
Miaka ilisonga na Salim alianza kuwa barobaro ila hali katika eneo hilo ilibaki kuwa ya sintofahamu.Watu waliuliwa na kuchinjwa kama jambo la kawaida tu.Wengi waliokuwa na nafasi zao walilihujuru eneo hilo na kwenda mbali.Mafukara na walalahoi kama kina Saida waliendelea kuishi hapo kwa kutawakali kwa mola.
“Hivi mama,hii hali ilianza lini na ni kina Nani wasiokuwa na utu wanaoendeleza hali hii?” Aliuliza Salim baada ya kukaa na swali hilo kwa muda mrefu mno.
“Mmh! Mwanangu.”Alianza kueleza Saida huku kayaelekeza macho yake kwenye paa kana kwamba maelezo yapo kwenye paa hilo.
“Hali hii ilianza kitambo mno hata sijawaza kukuzaa.Baba ya..ko…pi…a.”Saida alishikwa na kigugumizi cha ghafla.Macho yalimjaa machozi na hatimaye kudondoka.Alijifuta machozi kwa kanga yake akameza mate machungu Kisha akaendelea.”Baba yako aliuliwa kwa mtutu wa bunduki alipokuwa akitoka kazini. Nilikuwa na ujauzito wako wakati huo.Kikundi kinachotekeleza yote haya ni cha vijana wadogo tu wenye misimamo mikali na wanapokea maelekezo kutoka kwa wazee waliobobea katika suala hilo.”
Maelezo ya mama mtu yalizidi kumchanganya Salim badala ya kumpa mwanga na kutegua kitendawili chake.Maswali aliyotaraji yapate majibu yalizidi kuzaana akilini mwake.Alijiuliza maswali mazito na makubwa kuliko umri wake.Mmh! Kundi lenye misimamo mikali ya nini? Pengine huenda wakawa wako sahihi lakini kwa nini waue watu kikatili?Askari wako wapi?”
Alfajiri moja kabla bwana shamsi kushika usukani,Salim alinyapanyapa na kuelekea kusikojulikana.Aliamua leo ni Leo lazima aende akafanye uchunguzi wake binafsi wa kundi hilo linalojulikana kuwa lenye misimamo mikali.Kundi hilo lilikuwa na sehemu yao maalum ya kufanyia mazoezi na kujadili masuala aina aina yanayohusu kazi zao.Salim aliiulizia sehemu hiyo na akapelekwa.Wengi walimshangaa na kumuona Kama ngombe anayejipeleka kichinjioni ila Salim hakujali wala kubali.Alienda guu mosi guu pili hadi katika sehemu hiyo. Aligonga mlango taratibu na sauti nzito ilisikika kutoka ndani, “Ni nani huyo?”Kisha akatoka kiongozi wao huku kashikilia bunduki kubwa mkononi.
“Kijana unataka nini ? Nani kakuelekeza hapa?au wewe ndiyo jasusi?” Mtiririko wa maswali ulimuandama Salim asijue ajibu swali gani.
“Umekuwa bubu eh!”Aliendelea kiongozi yule huku kapandwa na mori akihofia Salim huenda akawa jasusi.
“Mikono juu silaha chini.” Ghafla ilisikika sauti kutoka mbali.Loh! Ilikuwa mapolisi.Roho ilimdunda Salim akifahamu kuwa leo ndiyo siku ya mtego wa panya kuingia waliomo na wasiokuwemo.Aidha siku utakapotembea uchi ndipo utakapokutana na mkweo.Walijaribu kukimbia ila juhudi zao hazikufua dafu.Wote walikamatwa na kutiwa mbaroni.Wapo waliopelekwa korokoroni na wapo waliopelekwa kusikojulilana akiwemo Salim.
Saida alirukwa na akili baada ya kumsubiri mwanawe kwa miaka na dahari bila dalili za kutokea.