_
Nimekuja kwenu tena, na ujumbe uso mwema
Watu ni kuambiana, sio kuachana nyuma
Kimya hakina maana, kwa hiyo nitayasema
Maadamu haujafa, ‘we bado hujaumbika
_
Sikuja weka baraza, wala hadithi kutoa
Sitaki kuwaeleza, maneno yasiyokua
Nimekuja kuzungumza, ambayo yanisumbua
Maadamu haujafa, ‘we bado hujaumbika
_
Usimcheke kilema, kijiona ‘we mzima
Hilo silo jambo jema, na pia sio heshima
Kuwa mja wa huruma, utende kwa taadhima
Maadamu haujafa, ‘we bado hujaumbika
_
Huijui kesho yako, utakuwa hali gani
Ikizidi mwisho wako, ajuae ni Manani
Ondoa kiburi chako, hakifai asilani
Maadamu haujafa, ‘we bado hujaumbika
_
Kwani ni ipi hasara, ya wewe kunyenyekeya?
Ukawa mwenye busara, kilema kumpokeya
Daima uwe imara, kwa dua kumuombeya
Maadamu haujafa, ‘we bado hujaumbika
_
Kumbuka ‘e mwanadamu, katika haya maisha
Hakuna kinachodumu, kila kitu kitakwisha
Basi haya yafahamu, yote nilokujulisha
Maadamu haujafa, ‘we bado hujaumbika
_
Lazima tuwakubali, katika jamii yetu
Tuwajali zao hali, kwani wao ni wenzetu
Na hakika kwa Jalali,tutapata fungu letu
Maadamu haujafa, ‘we bado hujaumbika
_