Shujaa ni nani? Je ni yule anayejitia kitanzi kwa ajili ya mpenzi wake? Au yule anayetenda mambo makubwa na maovu ili aonekane mbabe mbele ya wenzake? Pengine yule anayetia watu kabare na kuwadhulumu mali zao? Au yule mwenye mamlaka makubwa na anayeyatumia mamlaka hayo kuwanyanyasa na kuwatesa watu kisha akajinaki kuwa hakuna anayeweza kumpiku? Mmh! Bila shaka hao wako mbali na ushujaa wenyewe.
Wapo mashujaa wengi walioacha historia iliyoandikwa kwa wino usioweza kufutika abadaan kataan kuche kusiche! Kila ninaposikia neno shujaa basi jina linalonijia kwa haraka akilini mwangu ni Khalid bin Walid. Khalid bin Walid! Shababu shupavu,jasiri na shujaa aliyeacha nyayo ndani ya nyoyo za wengi waliomjua na waliomsikia.
Khalid bin Walid ambaye kwamba laqab yake ni Sayfullah alikuwa swahaba wa mtume Muhammad (saw) na kamanda wa jeshi msifika. Alitoka katika kabila la Qureysh ambalo liliwahi kuwa mpinzani mkubwa wa Uislamu. Vile vile alitambulika na kusifika sana kutokana na mbinu zake pamoja na ubabe wake katika vita. Ilikuwa chini ya uongozi wake wa kivita ambapo bara Arabu, kwa mara ya kwanza, katika historia liliunganishwa na khilafa.
Aidha Khalid bin Walid alichangia pakubwa kushindwa kwa waislamu katika vita vya uhud. Ilikuwa nadra sana watu kushindwa vita wakati yeye ni miongoni mwao. Hata hivyo, alisilimu na kuwa mtetezi mkubwa wa waislamu. Vile vile alishiriki katika vita tofauti tofauti pamoja na mtume Muhammad (saw), miongoni mwavyo ikiwa vita vya Mutah.
Inasemekana Khalid bin Walid alipigana zaidi ya vita mia moja ila hakufa katika vita hivyo bali alifia kitandani. Hata hivyo, hilo halikumfurahisha kwani alikuwa na hamu ya kufa shahidi ndani ya uwanja wa vita. Alifurahika sana alipokuwa ndani ya vita kuliko mahali pengine popote. Alisema, “Ninapokuwa ndani ya uwanja wa vita nafurahikia sana hata kuliko usiku wangu wa kwanza wa ndoa na msichana mrembo zaidi kuliko wote.” Kutokufa kwake shahidi kulimhuzunisha na kumsononesha sana akasema, “Nimepigana vita vingi mno nikiutafuta ushahidi. Katika mwili wangu hakuna sehemu isiyokuwa na kovu au kidonda vilivyosababishwa kwa kudungwa mshale na upanga ila leo nafa kitandani kama ngamia mzee. Macho ya mwoga yasiwahi pumzika.” Mkewe alipoiona huzuni ya mumewe alimwambia, “Umepewa laqab ya Sayfullah, yaani upanga wa Allah, na upanga wa Allah hauwezi vunjika. Hivyo basi, haukujaaliwa kufa shahidi, bali kufa mshindi.”
Abubakar aliposikia kuhusu kifo cha Khalid bin Walid alisema, “Wanawake hawatozaa mfano kama wa Khalid bin walid.”
Ni shujaa wa dunia, kijana huyu jamani,
Ni upanga wa jalia, jasiri aso kifani,
‘lipigana vita mia, akafia kitandani,
Japokuwa yake Nia, ni kufia uwanjani,
Ila haikutimia, nia yake masikini,
Mkewe akamwambia, isikutande huzuni,
Ni mipango ya Jalia, wewe kufa kitandani,
Ndugu zangu nisikia, mfano tuuigeni,
Tuwe tutajitolea, kwa njia yake Manani,
Ili tutapojifia, pepo iwe masikani,
Maswahaba wote pia, tuweni nao pembeni,
Khalid na walobakia, nao tufufuliweni.