Saidi,shababu mdogo ila mwenye ujuzi na kipawa kuliko umri wake. Kipawa chake kilizidi maradufu kutokana na juhudi zake alizotia. Alidamka alfajiri mno na kukitaliki kitanda chake wakati wengi wakiwa katika ulimwengu wa walalao. Aliamini kuwa usingizi huleta umaskini na yeye katu hakutaka umaskini umvamie na kumrandia. Huo ndio uliokuwa mfumo wa maisha yake,kuamka alfajiri na kwenda kutia zoezi kisha kwenda kuadhini adhana ya kwanza.Ebo! Kumbe ni mswalihina pia.Wengi kijijini walimpenda sana kutokana na juhudi zake pamoja na tabia yake maridhawa. Kila mzazi alitamani mwanawe awe kama saidi. Hata hivyo,wapo wengine waliomchukia na kumuonea gere hasa kutokana na kipawa chake,kipawa cha ulinda lango.
Saidi alikuwa mlinda lango hodari na mbuji. Ilikuwa tukizi sana kwa timu kufungwa ilhali yeye ndio mlinda lango wao.Hili liliwashangaza na kuwakata matumbo wengi ila kwa wengine hawakustaajabu sana kwasababu walizitambua juhudi zake zisizomithilika. Sio siri ukiona vyaelea bila shaka vimeundwa. Tena vimeundwa kwa vifaa madhubuti na vya thamani.Hali kadhalika,mgaa gaa na upwa hali wali mkavu abaadan.
Vijana walijaribu kwa udi na ambari kumpiku lakini wapi! Waliambulia patupu.
“Tupe siri ya mafanikio yako mlinda lango.” Baadhi ya vijana walisikika wakimuuliza.
“Hamna siri isipokuwa kumueka Mungu mbele na bidii za mchwa.” Alijibu Saidi kwa uchangamfu kama kawaida yake.
“Mmh! Muongo huyo.Lazima kuna mkono wa mtu.Anaenda kwa ‘babu’ huyo.Sio bure.” Wengine walisikika wakinongona chini kwa chini. Wapo waliosadiki kuwa huenda Saidi anatumia uchawi katika kuboresha kipawa chake.Ushirikina ulikuwa umekita mizizi katika kijiji hicho.Kila aliyetaka kufanikiwa alikimbilia kwa mganga ila badala ya kufanikiwa walizidi kudidimia.
“Huyu mtoto nitamrithisha kikoba changu atakapofikia umri mwafaka.Nitampa nguvu zangu zote na atakuwa ‘mtaalam’ maarufu kama bibi yake.” Alisema nyanya yake Saidi punde tu Saidi alipozaliwa ila mama yake alikataa kata kata kwani aliuchukia ushirikina hadi ya kuuchukia.Hivyo basi,aliamua kuhama kijiji jirani na mwanawe Saidi.Hata hivyo,mambo huko yalikuwa yale yale tena yalikuwa yamepamba moto zaidi.Wenye kunena hunena ametoka kuchinjwako akaenda kuliwako nyama.Licha ya hayo,mama Saidk alimlea mwanawe katika maadili mema na kumueka mbali kadri awezavyo na ushirikina.
Alhamisi,tarehe kumi na saba Mei,ilikuwa siku adhwimu kwa Saidi na wachezaji wengine.Jua liliangaza na kutoa miale yake kwa ghadhabu kana kwamba linawatahadharisha wachezaji kuwa leo mambo ni moto zaidi.Videge vya kupendeza viliruka kutoka mti mmoja hadi mwingine huku vikiimba nyimbo za kupendeza.Nayo miti ilionekana kukauka kwa kiasi fulanj.Mmh! Pengine imetishika na kitakachotokea leo.Maji kwenye maziwa na mito yalitulia tuli na kusikika kwa mbali sauti za vyura.Ng’ombe walienda mtoni kunywa maji kama kawaida yao isipokuwa n’gombe mmoja mnono na mwenye afya,tena anayetoa maziwa mengi kuliko n’gombe wote kijijini.Yote tisa,kumi leo ilikuwa yaumu ya mchuano mkali kati ya timu ya Saidi iliyojulikana kama ndiosisi na timu nyingine kutoka nchi jirani iliyojulikana kama ‘bluestars’.Timu hii ilisifika sana katika pande zote.Ilikuwa nadra sana kwao kufungwa.Kwa upande mwingine timu ya Saidi nayo ilikuwa imepewa jina la wasioshindika kutokana na kule kutokushindwa kwao hasa Saidi akiwa mlinda lango.Loh! Kweli mambo leo ni mazito,tena mazito kama nanga au kama mchuzi uliotiwa tomato za kutosha,utajaza wewe.Wanakijiji walikuwa na hamu na shauku ya kutaka kujua atakayeshinda leo.Itakuwa bila bila? Au bluestars watashinda? Aah hapana ndiosisi hawaezi shindwa.Mmh! Mtihani.
Uwanja ulitayarishwa ukatayarishika.Ndiosisi walifika uwanjani na kuanza matayarisho kabambe ya mwisho mwisho yaani ‘final touches’.Muda si mlonje bluestars nao walifika huku wakisindikizwa na ngoma,nyimbo na mashairi.
Leo ni leo twasema,tupambane uwanjani
Na tupambane vyema,tuone nani namba wani
Tumekuja hima hima,na pia twajiamini
Ndiosisi waliwaangalia kwa bezo huku wakiambiana wao kwa wao,”Hawa wana nini basi? Hawajui kama tunaye Saidi,bingwa wa mabingwa.Leo ni sare sare au tuwafunge.”
“Lakini Saidi yuko wapi?” Alisikika mwingine akiuliza.Hapo ndipo walipotahamaki saidi hayupo.Loh! Nyoyo zilianza kuwapapa.Jasho liliwatiririka na kuingiwa na vimbimbi.Walianza kizaa zaa cha kumtafuta.Uwanjani pote hakuwepo.Nusu saa tu ilibaki kuanza kwa mchuano.
Walienda guu mosi guu pili huku wamenyon’gonyea na kuwa wadogo kama piritoni hadi kwa kina Saidi.Raha na uchangamfu waliokuwa nao uliyeyuka na kupotelea mbali.Wingu la huzuni na simanzi liliwafunika lisiache hata upenyu wa bashasha.
Walifika kwa kina Saidi na walioyaona yaliwatamausha na wote wakabaki vinywa wazi.Saidi alikuwa kalala chali huku povu linamtoka mdomoni.Kando yake kulikuwa na bilauri ya sharubati.Ghafla kulisikika sauti za watu zikinon’gona kutoka dirishani kisha zikatoweka.Loh! Kitendawili.