Picha: http://www.deeprootmethods.com/
Enzi hizo,nilipokuwa bado mdogo. Wakati akili yangu ilipokuwa bado changa, bado haijafunguka na bado haijaweza kuelewa uhalisia wa mambo,nilikuwa nikiduwazwa mno na mbio walizokwenda watu. Nilishindwa kuelewa kinaganaga kwanini watu wanajitesa kwa kufanya kazi za sulubu, kujiumiza kwa njia moja au nyingine na wengine kufikia hatua ya kutopumzika isipokuwa usiku tu.Mfano hai kabisa ilikuwa mama yangu. Alirauka alfajiri mno wakati hata jua halijafikiria kuchomoza na kuanza matayarisho ya kupika ndizi za kiume,chapati, maharagwe ya nazi, wali na uji wa ngano ambazo aliziuza na kisha kulala usiku sana wakati watu wengi wakiwa wameshafika katika sayari ya ruya.Mwengine aliyekuwa akiniacha na maswali chungu nzima ni kaka yangu aliyekesha usiku kucha eti anabukua bukua vitabu vingi alivyovipanga vikawa kama mlima Kilimanjaro.Mmh! Mateso haya yote ya nini? Upo wakati nilitaka kukata kiu yangu na nikaamua kumuuliza mama yangu ila jibu nililolipata lilinichanganya maradufu. “Tunatafuta mafanikio mwanangu!” Alinijibu nina.
Hata hivyo, nilipoanza kukua.Kukua kiumri na kiakili niliweza kukitegua kitendawili changu nilichokiona kigumu kama chapatti zilizokosa samli ya kutosha hapo awali.Majibu yote yalianza kutiririka nyweeee! Maisha yalinifunza mambo mengi ambayo kwamba hayafunzwi darasani wala na mzazi.Taswira ya juhudi za mama yangu, kaka yangu na watu wengine kwa ujumla zilinijia upya akilini na nikaelewa ni kwanini walikuwa wakienda mbio kama punda aliyeshikwa na kichaa cha ghafla.Mafanikio! Walikuwa wanayatafuta mafanikio.Ni nadra maishani kufanikiwa bila kujitesa, kujituma na kufanya mambo kinyume na hiari yako.Nilianza kuyafahamu yote haya. Kufahamu kuwa ni lazima kutoa jasho ili kupata tonge la siku.Japokuwa kutoka jasho huko ni kugumu mno ila ni muhimu kujikakamua ili kufikia tunakotaka.
Mizizi ya shajari yeyote ile huwa michungu kama subili ila matunda yake ni matamu au hata kama si matamu huwa yana umuhimu fulani ima kwa matumizi ya binadamu au hata chakula cha hayawani.Aidha, ni vigumu mno, mmh! Vigumu kweli? La! Ni muhali kwa mti wowote ule kumea pasi na mizizi. Mizizi licha ya uchungu wake ndio msingi wa mti wowote chini ya jua.Uwe mti mkubwa kama mbuyu au hata mdogo kushinda uyoga.
Hali kadhalika, mizizi ya mafanikio huwa michungu ajabu.Ili kufanikiwa katika dunia, ili kuyapata matunda matamu ya miti ya mafanikio lazima tukubali kukabiliana na uchungu wa mizizi yake.Lazima tukubali kukabiliana na hali halisia ya kuyafikia mafinikio. Lazima tujifunge kibwebwe bin masombo na kujitolea kwa udi na ambari kuhakikisha kuwa tunaigeuza mizizi kuwa matunda matamu yatakayodondosha watu mate na kuwatia moyo ili nao wameeshe miti yao ya mafanikio.
Tabasamu nyingi tunazoziona za watu walioyapata mafanikio, wameupitia uchungu wa mizizi ya mafanikio hayo.Ila hawakukata tamaa,hawakuiona mizizi hiyo kama nuksi au kisiranu bali waliamua kuinyunyuzia maji ili imee na kuchipuka matunda.Lau wangeshikwa na hamaki na kuikatilia mbali mizizi je wangeyapata matunda walionayo sasa? Je wangekifurahikia kivuli na upepo mwanana unaovuma chini ya miti yao? Miti ya mafanikio.
Aghlabu, kila tunapoona mtu amepata mafanikio makubwa na anayafurahikia matunda ya mti wake, basi hatufikirii kuwa matunda yale yamemea katika mti ulio na mizizi michungu isiyotamanika kuliwa.Tunachokiona cha kwanza ni tabasamu na bashasha katika wajihi wake na kisha tukanong’onezana sisi kwa sisi, “Aaaah Yule alibahatika tu.Bahati ilikuwa upande wake ndio maana akafikia pale.”
Hatuna habari kuwa alikesha usiku mzima,alidamka alfajiri wakati sote tukiwa tumelala fofofo tukiota ndoto zetu na kutumai tutazitimiza bila kuzitolea jasho,alivunjwa moyo ila hakuuruhusu asilani moyo wake kuvunjika, alipigana vikumbo na watu wenye ‘nguvu’, alichekwa na kukejiliwa, alilivumulia jua lilimchoma bila huruma, aliivumilia mvua iliomnyea na kumtotesha akaloa chapachapa.Alivumilia yote yasiovumulika.Aliuhimili uchungu wa mizizi akiamini kuwa mizizi hiyo ipo siku itamea na kuwa mti mzuri utakaodondosha matunda matamu kama asali na kumpa kivuli na upepo mwanana.
Hivyo basi, kila tutakapo fikiria kukata tamaa, kila tutakapoona mizizi imezidi kuwa michungu, kila tukapoona mawimbi yamezidi kuwa makubwa na ya kutisha tukumbuke kuwa hakuna mti unaomea bila mizizi na bahari yenye mawimbi makubwa zaidi ndiyo inayochipua wanamaji stadi.Aidha, lulu na almasi zinapatikana chini kabisa ya bahari.