Wanasema ulimi hauna mfupa. Kwa hiyo ni vigumu kuudhibiti. Pengine ni kweli au pengine ni sababu ya kusema tunalotaka.
Tukianza kuropokwa maneno humiminika kama maji yanavyotoka kwenye paipu iliyopasuka.
Hatuzingatii uzito wa maneno yetu. Si wakati tunapoongea na wenzetu bali hata tunapokuwa tunazihadithi nafsi zetu.
Wengine tunakariri na kukariri na kukumbusha watu kutwa kucha maradhi au masaibu au changamoto tulizojaaliwa nazo. Tena mara nyingi kuzitumia kama mbinu ya kujishindia mapenzi, usaidizi na imani za watu.
Hatuoni uzito wala taklifu kujibandika lakabu tusizozistahiki. Tena hufanya kama matani:
“Mimi niite mama kusahau.”
“Yule muite mzee wa kutoelewa.”
” Huyu muite bingwa wa chokoraa.”
Lau tutazingatia- kisawasawa- jinsi tunavyotumia maneno yetu tungeshtuka kwa namna na uwepesi tunavyojitilia sumu na kujiapiza wenyewe Allah atustiri.
Bila kutanabahi wala kufahamu tunarudia rudia maneno yale yale ya kuturudisha nyuma.
” Wajua mimi nilikuwa yatima.”
“Wajua mimi nilifutwa kazi” na mbaya kabisa:
“Mimi ndiye mkosa bahati.”
Tena wakati mwengine kutumia hizi kama visingizio na sababu yakutojaribu au kukwepa majukumu na wajibu.
Wengine tunafurahia kutangaza hali ya mifuko yetu.
“Wajua mimi sina hata ndururu mfukoni.”
Tena wengi wanajitambulisha kwa “umaskini” wao.
Utawasikia: “usinidharau kwa kuniona ni maskini.”
Kweli hali za kiuchumi zinatofautiana ;kila mtu ana mitihani yake lakini tusikubali mitihani hiyo ikawa majina yetu au vitumbulisho vyetu. Mwanadamu ana hadhi yake.
Fikra kama hizi hazitusaidii kabisa. In sha Allah huna hata shilingi ya tundu kipochoni mwako hiyo ni siri yako na Mungu wako.
Allah ni mkarimu. Jipe moyo.
Leo sina kesho Mungu ataleta kheri yake.
Na wengine wetu tunapokasirishwa hutamka kwa hasira: “hunijui mimi. Kama wewe ni mwenda wazimu mimi ni mwenda wazimu kukushinda….”
Usijiapize. Mshukuru Mola kwa kuwa na akili timamu siyo kinyume ya hivyo.
Wengine tunawalaani watoto wetu bila kujua.
” Huyu mtoto atanitoa hii roho yangu.”
” Huyu mkorofi, mtukutu, hasikii, afadhali dadake.”
Ama tuwaeleze wasimamizi wa shule na madrasa:
“Huyu mwanangu hashiki ni mzito wa kuelewa ……” SubhanaAllah.
Tena kumimina petroli kwenye moto unaongea hayo kwenye watu chungu nzima.
Maneno jamani. Maneno ni ya kupimwa. Yaonje kabla hujayatema. Si jambo dogo la kupuuzwa.
Mtume Muhammad Rahma na Amani za Allah zimshukia yeye amesema: “Mwenye kumuamini Allah na Siku Ya Mwisho basi atamke ya kheri au anyamaze.”
Huu ni wasia kutoka kwa bora wa viumbe. Kusema maneno mazuri ni kufuata maamrisho yake Swalla Allah alayhi asssalam.
Si tu unapoongea na wengine. Tena basi ni muhimu zaidi uwe mwangalifu kabisa pale unapoongea na nafsi yako. Jisemeshe kwa heshima na taadhima. Tumia maneno matamu ya kukupa motisha.
Hii haimaniishi kuwa unajisahaulisha kasoro zako la. Au kujidanganya kuwa umo hali bora kuliko ulivyo.
Maneno yana uzito wa na yana nguvu za, kwa uwezo wake Mola, kujenga au kuharibu.
Sisi wote ni binadamu na ukamilifu ni wa Allah peke yake.
Kabla hujaongea jiulize: ” Je haya niliyonayo ni ya kweli na uaminifu? Ni mazito ya kuumiza? Ni ya dharura lazima yasemwe?”
Pia pale unapowaza, fikra zikapita akilini mwako ukasema :
“Aaah mimi sina bahati!” Au:
“Mimi ni mzito wa kuelewa!”
Jiulize kweli? Hii fikri ina ukweli gani? Fikra kama hii ina manufaa gani?
Maneno huundwa na fikra, na ndio kioo cha yanoyopita moyoni mwako.
Yatumie kwa busara na mazingatio.
Wengi wamejutia kujikwaa ulimi lakini ni wachache wanaojutia kimya chao…
Maneno ni Silaha-Yatumie Vizuri