Kwa karne nyingi zilizotutangulia, kumeshuhudiliwa mafungamano makuu kati ya waarabu, haswa wa Hadhramout na Oman, na wakaazi wa mwambao wa Afrika mashariki na visiwa vyake, KIlwa, Lamu, Mombasa, Zanzibar, Tanga na kwingineko. Mafungamano ya ukwe, nasaba, utamaduni, elimu na dini yaliyokita mizizi kiasi cha kwamba ndiyo misingi iliyojengewa tunaloita leo ‘uswahili.’
Siku zote, makundi yakiwa mingi, moja humpiku mwenzake. Japokuwa waomani, waliokuwa waislamu katika mfumo wa kiibadhi, ndiyo walioshika mamlaka na kutawala kutoka Mogadishu kwenda kusini, ni wahadhramy, waliokuwa katika mfumo wa kisufi, walioweka athari kubwa zaidi. Usufi ukaenea kwa kasi zaidi. Kwa mtazamo tu, zaidi ya asilimia 80 ya waislamu wa mwambao huu wako katika madhhab ya kishafi lakini utekelezaji wa ibada ni kwa mrengo huu wa kisufi, wakiwemo katika twariqa za qaadiriyya, shaadhiliyya na alawiyya. Kwasababu ya athari hii, hivileo Afrika mashariki, mtu akikwambia kuwa ni mshafi, ni sawia na kusema mimi ni sufi, japokuwa ni vitu viwili tofauti. Na hili jambo lingeleta utesi katika siku zinazotukabili.
Dini ndiyo mti ambao chini yake watu hupata kubarizi kwa kivuli cha tamaduni zake, hata mti ukawa umepinda vipi. Hivyobasi, kwa mlipuko uliotokea kwa watu hawa wawili kukutana, tamaduni zetu zikajengewa kutoka huu mrengo wa wawahadhramy, maharusi, maulidi na mengine mingi.
Kuna maswali mingi mi hujiuliza hivi sasa uzeeni ambayo najuta kutouliza katika ujana wangu kwani walio na majibu washatangulia mbele za haki. Maswali kama “tulitokea wapi?”
Marehemu babu Hatibu sikumdiriki. Kiasi cha habari zake ninazozijuwa ni kuwa alitokea arabuni, Hadhramout na alipofikia hapa akamchumbia marehemu nyanya, Tima na kumzaa babangu Ali Hatibu. Naye baba alipokuwa naye akamchumbia mamangu na kutuzaa sisi wanne, dada Tima, da Binti-Ali, kakangu Mwinyi nami kitinda mimba Mwanasha. Pamoja tukaishi Ngare, katika mji huuhuu wa Mombasa.
Kupita kwa umri kumenifanya nisahau kumbukumbu nyingi za maisha utotoni. Ila ninalojuwa kwa yakini ni kuwa nilikulia katika nyumba iliyojaa furaha chini ya Ali Hatibu. Nilicheza na ndugi zangu michezo ya kila aina huku tukitunda matunda ainati kutoka shamba la baba. Katu baba hakutukemea kwani ni kama alivyotuambia siku zote kuwa yote haya yalikuwa kwa ajili yetu. Baba alitupenda sana na hakuhitaji lolote kutoka kwetu isipokuwa kumsikiliza maneno yake na kufwata nasaha zake. Na huu ndiyo msingi tulioishi nao maishani.
Miaka ya hamsini ilipoingia nilikwenda kwenye densi nyingi zilizofanywa kwa ajili ya vijana wa mji na hivyo ndivyo nilivyokutana na masahibu wangu wingi nilio nao karibu hivi leo. Hapo tukiwa wanawali katu hatukuwahi kufikiria kuwa ipo siku ingefika tukawa tunaangaliwa kama wakwasi wa busara na maneno yetu yakawa ni yenye kukamatwa kwa magego na aila zetu.
Ipo siku ya kuzaliwa, kisha kuna ile siku ambayo maisha huanza rasmi. Siku yangu ilikaribia zaidi nilipoingia ndani ya nyumba ya mume wangu Hasani.
Hasani alikuwa kijana wa kwanza wa mzee Juma, aliyekuwa mfanyibiashara kutoka Tanzania. Inasemekana alikuja nchini kwa ajili ya biashara, yeye na dadake Amina. Naye rabana kamkunjulia dunia mpaka ilipokuwa ikitajwa Changamwe nzima aliye na mali zaidi, Changamwe ya chini ilikuwa akijulikana Susu. Ndiyo iliyokuwa lakabu yake aliyojipa mwenyewe kwa fahari aliyokuwa nayo.
Katika zama zile mtu akipika kitoweo ilikuwa akifinika na chombo spesheli iliyokuwa kazi yake hususan ni kukizuia kisiliwe na paka. Chombo chenyewe kiliitwa susu. Mume wangu, sijui zilimtumaje lakini siku hiyo aliingia nyumbani kifua mbele na kusema “mimi ni Susu, siguswi na paka” na kuamrisha kila mtu amuite hivyo kuanzia hiyo siku.
Nilikuwa mke mdogo katika nyumba ya Bwana Susu, kukiwa na wawili wakubwa juu yangu tulioishi pamoja katika nyumba hii moja. Wazo hili la kuwa kuwa mke wa tatu halikunizonga kama ninavyoona linavyokondesha watu siku hizi. Ilikuwa ada.
Lakini pia, haikuwa nyumba ndogo. Ilikuwa nyumba ya gorofa na katika zama hizo ilikuwa nadra kupata gorofa hata mjini mkuu Mvita. Kulikuwa na samani katika kila chumba zilizotoka nchini Tanzania. Nje kulikuwa na magari mawili, wakati huo kuna hata wale ambao hawakuwahi kujuwa kuwa kuna kitu kama gari. Tulikuwa na maboi wawili ambao ndiyo waliokuwa wakishughulika na shughuli za usafi pale nyumbani na kutufulia. Kila siku bwana Susu angeenda shambani kwa gari lake na kurudi na nyama ambayo mimi na wakewenzangu tungeitayarisha. Hiyo ndiyo kazi pekee tuliyofanya katika nyumba hii. Tuliishi kama malkia katika kasri hili na hatukuwahi kukorofishana.
Msiba uliotukumba peke yake ni baada ya Kenya kupata uhuru, kulikuwa na presha nyingi kutoka serikali, tuhame ili uwanja wa ndege wa Moi ufanywe mkubwa zaidi.
Baada ya mwaka, rabana akanibariki na mtoto wangu wa kwanza, tukamwita Kisusu. Nikapata wengine wawili, Ali na Kugesi na hizo ndizo zama mume wangu alipoanza kuugua. Nilipomzaa mwanangu wa mwisho naye kasimu, katika mwaka ya sabiini , hali ya Bwana Hasani ilikuwa mbaya zaidi.
Kasimu alipofika miezi minne nakumbuka kuenda naye chumba cha babake. Akambeba mikononi na kutabasamu, kisha akaniregeshea. Hiyo ndiyo siku alipokuwa anasafiri kurudi nyumbani KIlulu, Tanga kwa ajili ya matibabu, Kilulu, Tanga.
Haikupita miezi mingi mpaka zilipotufikia habari za kifo cha mume wangu. Kuongezea juu ya huzuni, tulilazimiwa kuhama ili mradi wa kupanua uwanja wa ndege wa Moi uendelee. Hatukufidiiwa kwa hasara zilizotufikia baada ya hii.
Wake wenzangu waliguria nyumba aliyotuachia mume wangu iliyokuwa Magongo. Babangu Ali alipopata habari hizi nazo kuwa mi pia nilikuwa nihamie huko, aliniusia kinyume cha hicho na kuniuliza kwani sikuogopa kushambuliwa na kupigwa na wajaluo huko Magongo. Kulikuwa na habari nyingi zinazoenea kuhusu ukatili wa watu hawa na kwa kuwa niliamini kuwa baba alifahamu zaidi, na kuona mingi zaidi,nilimsikiza maneno yake. Akanipa kiwanja kidogo kilichokuwa na nyumba ya makuti inayovuja, na mtu wa kunisaidia kwa lolote lile, Mzee Kiko. Kama nilivyosema, ipo siku ya kuzaliwa, na ipo siku ambayo maisha huanza rasmi. Ndani ya nyumba ile na watoto wangu wanne, ndipo awali nilipopatwa na wimbi la maisha.