Maisha ya utotoni ni maisha matamu sana kwa wengi. Wengi utawasikia wakisema wanatamani warudi katika maisha hayo kwa sababu ni maisha yenye raha tele. Hakuna kuwaza kuhusu hili wala lile, kubwa wanaloliwaza watoto ni michezo. Ni michezo gani unayoikumbuka?
Binafsi nikikumbuka maisha yangu ya utotoni nabaki kufurahi na kutabasamu tu. Kuanzia michezo, uchokozi, kuadhibiwa kwa makosa haya na yale na pia mambo mengi ya kitoto tuliokuwa tukiyafanya. Nakumbuka vyema siku moja mimi na dada yangu tuliwaita maswahiba zetu nyumbani ili tuwapatie aiskirimu. Tuliwarambisha lakini badala ya utamu ulikuwa ni uchungu wa ajabu. Naam, haikuwa aiskirimu bali subili iliyotiwa kwenye mkebe wa aiskirimu. Tuliwakomesha kwa kweli.
“Kama wanidanganya ujue astaghfirullah yako haikubaliki.”(astaghfirullah inamaanisha, ‘Mungu nisamehe’).Haya ni maneno ambayo mmoja angemwambia mwengine lau angehisi anadanganywa kwa sababu tulikuwa na tabia tukidanganya tunasema astaghfirullah haraka haraka.
Loh! Sijui hili lilitokea kwa mimi na dada yangu tu au nawe pia msomaji ulipitia hili?
“Fanta, kokakola…….Sprite?” Kibe! Kibe ulikuwa mchezo mkubwa tulioupenda hadi ya kuupenda. Mwenye ‘kukishika’, yaani mtu ambaye angewatafuta wengine waliojificha alisema “fanta” na wenye kujificha walisema “kokakola” mpaka hatimaye mwenye kutafuta akisikia kimya atauliza “sprite” na kama hakuna jibu basi anafahamu kila mtu ashajificha na ataanza kuwatafuta.
Wakati mwingine tulifokewa kwa kuchelewa kurudi nyumbani kula chamcha. Mchezo wa makwanza, kiguru(blada) huwa umenoga mpaka hamu ya kula inapotea. Huu ulikuwa mchezo ambao kwanza kamba huwekwa katika kina kifupi ili watu waruke, alafu husongezwa mpaka wakati mwengine inafikia makwapani. Wapo wasichana wenzetu waliokuwa wakiruka mpaka vina vyote, naweza sema pengine ni kipaji hicho kwa sababu mimi binafsi nilikuwa siwezani kuruka katika kina kirefu. Hivyo basi, nilikuwa nikipenda nichaguliwe na wale magwiji ili niwe kwenye kundi lao nipate ‘kuokolewa’. Makundi yalikuwa mawili katika michezo mingi. Si uki, si mstatili, si makwanzaaa, si mpira wa kujaza. Hata hivyo, kulikuwa na mchezo uliotwa ‘wote wote’. Huu ni mchezo ambao haukuwa na makundi. Watu wote waliingia katikati kucheza na upande wa kulia na kushoto kulikuwa na wenye kurushia hao watu mpira. Atakayelengwa alitakiwa kutoka mchezoni na wengine kuendelea mpaka abaki mmoja wa mwisho ambaye angetakiwa ‘kuokoa’ wenzake. Na kwenye huu mchezo kulikuwa na nyimbo yake, ‘wote wote, iyaa wote kwa wote iyaaa…kina mama iyaaa na kina baba iyaaa’.
Turudi kwenye yale makundi mawili. Katika kucheza kwa mfano, ‘uki’ watu walichaguana makundi mawili. Kundi la kwanza lilicheza huku watu wawili katika kundi la pili wakirusha mpira na wakati mwengine kuwa na ‘msaidizi’ nyuma ambaye alisaidia kuleta mpira ukienda mbali. Kizaa zaa kilikuja pale kundi la kwanza wawe ‘wakali’, wawe ‘hawalengwi'(yaani wanacheza bila kukosea). Wanaweza wakacheza mpaka kukaingia jioni, wakati tunaotakiwa kurudi nyumbani. Hii ilipelekea kundi la pili kutopata wakati wa kucheza. Unapojikuta upo kwenye kundi la pili unakuwa unaudhika sana.
Utasikia watu wakilalamika, “hamujatupa kichems chetu.” Kichems nadhani ilimaanisha kichance.
Hivyo basi, siku ya pili watu walirudi mchezoni kupeana ‘vichems’ vyao au hiyo stori iliisha hivyo.
“Una malali.” Haya ni maneno ambayo mtu angesema lau angeona kuna dhulma flani inaendelea. Mpaka leo sijafahamu neno ‘malali’ linamaanisha nini. Malali kwa mfano yangetokea wakati wa kucheza lenga lenga, ambapo mpira ungegusa nguo ya mtu.”Sijalengwa! Mpira umegusa nguo tu, nyi muna malali.” Mwenye kucheza angejitetea. “Unlengwa unlengwa, we ndio una malali.” Wangejibu wenye ‘kukishika’ Hapa unadhani ni nani mwenye malali?
Magrumachi dondoo, chako, ‘watoto wangu eh’, ‘twamtaka rafiki’, kigogo. Hii yote ni michezo ambayo ilikuwa ikijaza furaha ghaya katika nyoyo zetu. Aidha baadhi ya michezo hii ilikuwa mizuri sana kwa afya, naam bila shaka, kukimbia na kuruka ni mazoezi si haba. Bila kusahau kuruka kamba huku tukiimba nyimbo ambazo mpaka leo sifahamu ni nani aliyezitunga. Watu wawili walirusha kamba na mmoja kuingia katikati na nyimbo kuanza kuimbwa. ‘A,b,c,d,e,f’……mwenye kuruka akikosea katika herufi ‘f’ basi hapo hapo hupewa mume ambaye jina lake linaanza kwa f, mfano Faridi. Nyimbo inaendelea, ‘Farwa Farwa, je unakubali kuolewa na Faridi?’
Ilimradi ulikuwa mchezo tuliofurahikia.
Hadithi tamu tamu vile vile zilikuwa zikiniacha nikiogelea kwenye bahari ya furaha. Mama yangu na nyanya yangu walikuwa wakipenda sana kututambia hadithi. Hadithi nimezisahau sahau ila ipo moja bado naikumbuka kuanzia mwanzo wake hadi mwisho wake; Hadithi ya Makame.? zipo hadithi nyingine ambazo sizikumbuki vyema na nyingine nakumbuka nyimbo zilizokuwemo kwenye hadithi hizo, kama, ‘ng’ombe wa baba ng’ombe wa mama, fungua mlango nipite’. Je ni hadithi gani unayoikumbuka?
Pia kulikuwa na mchezo wa gololi ambao aghlabu ulichezwa na wavulana. Mimi sikuwa shabiki wa mchezo huu kwa hiyo siukumbuki vyema.
Hatimaye ikifika jioni watu huanza kuagana kwa kuambiana, ‘kalale nacho’. Au pia kuna nyimbo ya kuagana, ‘kila mtu kwao kwao, asokuwa aje kwetu tumpige fimbo….’
Hapo kila mtu hushika njia na kuelekea kwao akiwa amechoka hoi bin tiki .
***
