Mombasa ni mji wenye historia ndefu sana. Tangu enzi za Wafursi, Wa ajemi, Waarabu hadi enzi za wazungu mifano ya Vascodagama na hatimae mkoloni Muingereza. Historia hii ya mji huu inatoka na uwepo wake katika fukwe za pwani ambazo ni maingilio ya wageni katika bara letu la Afrika. Mombasa ni mji ambao historia yake ilikuwa ni ya wasomi na wachapa kazi. Wasomi hao na wachapa kazi hao wa kila sekta kutoka kwa uhamali hadi kwa biashara waliifanya Mombasa kunawiri na kustawi.
Katika msemo mashuhuri sana ni ule msemo wa Mombasa raha. Raha hiyo ililetwa na tamaduni za pwani na amani iliotanda. Wageni walifurika na kumiminika kuja Mombasa wakati wa sherehe zao za kibinafsi au wakitaka kubarizi katika fukwe za pwani. Mji huu ulikuwa ndio mji unaoenua pwani nzima kiuchumi kutoka Lamu hadi Lunga Lunga.
Masaibu yalianza kuufwata mji huu wa amani pindi tu Kenya iliponyakua uhuru wake. Wenyewe wasema “Safari ya khatua elfu huanza kwa khatua moja” mipango na mikakati kabambe yaliekwa na mkoloni mambo leo ya kuimaliza Mombasa kiuchumi. Mikakati iliochukua miaka mengi kukamilisha na hatimae wameweza kuifanikisha mikakati hiyo. Kulianza kupigwa mbiu ya kuwa wapwani hawakusoma au wapwani ni wavivu. Kabla ya uhuru mahamali bandarini walikuwa ni wapwani ila walitaka kulaza watu na kuwavunja moyo ili wasipiganie haki zao.
Wakoloni mambo leo walisema wapwani wasubiri maembe yaanguke. Walisahau kuwa kabla ya wao kuja Mombasa tayari Mombasa na Pwani kwa jumla ishaimarika na kustawi kiuchumi. Jee kama wapwani wasubiri maembe yaanguke Mombasa hususan na Pwani kwa ujumla ingekuwa imestawi? Jee Mombasa ingekuwa na historia? Lakini nyimbo hizi ziliendelea kuimbwa na viongozi wa juu ya serikali ambayo ilifuatiliwa na wananchi wao. Japokuwa hivi sasa katika kila nyumba Mombasa huwezi kukosa mtu mmoja au wawili ambao wamefika chuo kikuu huwezi kupata kazi ndani ya pwani ambayo wameandikwa asilimia hamsini ya wapwani. Sababu inayotolewa ni kuwa wapwani hawakusoma. Swali linalotatiza akili ni jee wapwani kwa msingi wao huwa si wasomi hata wakisoma mpaka daraja ya juu ya elimu?
Adui hawezi kuwashinda mpaka kuwe na mnafiki katika jumuia yenu. Changamoto kubwa inayotukabili sisi kama wapwani sio ubeberu au ukoloni mambo leo bali ni wale wanafiki waliotuuza kwa zabuni ya juu. Wale tuliowachagua kama viongozi wetu wapwani walituuza kwa zabuni ya juu na kujaza matumbo yao. Hawa ni wale mabwanyenye ambao wako radhi kuwatupilia mbali watu wao ili wajaze mifuko yao. Siasa za kujifanya simba wa pwani kumbe kwa uhalisia ni fisi unaekula mizoga ya pwani. Viongozi walio radhi kuteta na kutukanana katika majukwaa ya siasa ili tu kuridhisha watu waio juu na kuangamiza jamii zao. Mafisi kama hao waliichukua Mombasa wakaipeana kwa simba wenye njaa walio tayari kula kila kinacholiwa hatimae makombo wakapewa wao. Famau hakupata lolote, Mwambodze akaambulia patupu, karisa akala huu.
Hivi sasa nasikia Mombasa iko mahututi yaelekea kuzimu lakini ukweli wa mambo ni kuwa Mombasa tayari ishakufa kitambo yaliobaki ni mazishi na kusomewa hitima.