Najua ni muda mrefu sana tangu mwisho kuandika . Nimekuwa nikipigana na fikra zangu juu ya kuandika suala hili. Moyo mmoja ukiniambia nisiliandike huenda nikajiharibia na mwengine ukinihimiza niliandike huenda nikawatia moyo wenzangu tulioko kwenye jahazi moja. Na sasa naliandika ila bado niko katika njia panda ya kuendelea au kuwacha.
Sio rahisi kwa mtu kufungua roho yake na kusema jambo linalomkera kwa mwia mrefu. Katu sio rahisi kumwaya yanayonichoma mtima kila kukicha. Pengine inaweza kuwa ni kutokana na matumaini mengi nilioyaweka hapo awali au tuseme ni ukosefu wa kuwa na subira ya hali ya juu. Subira nilionayo imenifikisha hapa baada ya kungoja kwa miaka minne na bado naendelea kusubiri.
Labda nikuulize tu mwenzangu, hivi umekaa mda gani tangu umalize chuo kikuu bila ya kupata kazi? Tupo wengi au nipo pekeyangu? Tangu nilipohitimu shahada yangu mwaka wa 2016 hadi wakati huu ninaoandika ujumbe huu, sijafanikiwa kupata kazi. Nashukuru niliweza kufanya attachments kwa kampuni chache. Safari hii kamwe haijakuwa rahisi. Upo wakati ilinifisha moyo sana kufikia hata kujuta kusoma walakin minghairi ya hisia hizo, ugumu wa maisha hunilazimu kuendelea kutafuta kazi hadi dakika hii. Kwa hakika, nahisi kama Kenya ina wenyewe, na ndio maana niliwahi kuweka maoni yangu kwa machungu wakati nilipoona ndugu yetu katibu wa baraza la mawaziri, Mheshimiwa Bi. Nadya, kaweka mtandaoni kuwa “Kenya ni mimi na wewe”. Hapana, haiwezekani. Kenya hii naishi kwa imani tu. Maonevu na mapendeleo niliyokuwa nikiyaona hainipi haki ya kusema Kenya ni yangu. Wale wanaopata wakitakacho kwa njia zisizo za sahihi bila kuchukuliwa hatua yeyote. Wale wenye mali tumbu nzima na makampuni na wamesalia kuandikana wao kwa wao. Hao ndio wenye nchi. Sisi walalahoi, tusiokuwa na jamaa zetu waliopo kwenye nyanja za juu. Sisi tuliofundishwa na wazazi kwa shida na hali za kifukara na kufikia kumaliza akiba yao yote, mbona tupotupo tu tukitumiwa kama vijego vya kuwaenua wengine.
Wacha leo nikupe historia fupi ya safari yangu ya ku tarmac. Pindi tu nilipomaliza chuo kikuu, nilijawa na matumaini kuwa ningepata kazi nzuri kwa muda usiokuwa mrefu. Niliamini fika kuwa isingewezekana Mombasa hii ati ningekaa mwaka bila kupata kazi. Kumbe yalikuwa mawazo tasa. Sijakaa mwaka tu bali nimekaa miaka. Polepole nilianza kutafuta kazi. Nilianza na zile kampuni za ndoto yangu. Kampuni kubwa kubwa. Ukapita mda fulani hivi, bila majibu yoyote. Nikaamua kutafuta hata kwenye vijikampuni vidogo vidogo nikijiambia kuwa nitashikilia kiasi cha kupata kazi nzuri. Wapi? Wiki, miezi na hatimaye mwaka. Nikaona mambo hayakuwa kama nilivyotarajia, hivyo basi niliweka ratiba ya kutembelea kampuni kila siku nikiomba kazi. Uzuri nilisomea kuhusu fedha, kwahiyo niliweza kuulizia kazi katika kampuni yoyote. Nikaanza na kampuni zilizohusika na masala ya fedha. Wiki ya pili, nilikwenda kwenye mahospitali, wiki ya tatu katika kampuni za redio na kadhalika. Nilichapisha karatasi zangu na kuwa na nakala nyingi. Nilikuwa nikienda sehemu najieleza alafu nabwaga karatasi zangu. Nikaendelea vivyo hivyo kwa kiasi cha miezi miwili au mitatu sikumbuki vizuri . Hatimaye, niliamua kuenda mtaa ulioko na viwanja (godowns) mbalimbali, uitwao Labour hapa Mombasa. Nilianza mguu mosi mguu pili, kiwanja baada ya kiwanja kuanzia kiwanja cha kwanza hadi cha mwisho kutokea kufikia mtaa mwengine sehemu za makupa. Yaumu hiyo katu siwezi kuisahau wala kuizika katika kaburi la sahau, maana nilirudi nyumbani viatu vikiwa vimetoboka.
Siku na miezi ikasonga, hamna lolote. Waah, nikaamua kuchukua hatua nyengine. Nikawa naenda mjini, nasoma magari, tisheti za watu walovaa, pikipiki, saa kubwa za barabarani zinazofadhiliwa na kampuni tofauti tofauti. Nilitazama kila kitu chenye jina la kampuni, nikiandika jina hilo kwenye simu. Alafu niliporudi jioni, nilikuwa nikizitafiti kwenye mtandao, zengine nikituma baruapepe na kutuma ombi langu la kazi, na zengine nikienda mwenyewe kwenye kampuni na kuwaeleza ombi langu. Jamani, kimya! Sikuvunjika moyo. Nilichukua hatua nyengine, nilienda kutoa copy makaratasi yangu na kuingia kwenye magorofa marefu ya ofisi hapa Mombasa. Nilianza na TSS, jumba la NSSF alafu Ambalala Hse na kadhalika. Zipo afisi hazikuniruhusu hata kuingia ndani, hapa nilihitajika kumwachia askari stakabadhi zangu.
Licha ya hayo, kuna wakati serikali hutangaza kazi. Ningezichangamkia haraka sana, juu ya gharama zilizoandamana nazo ikiwemo kutuma good conduct, helb cert, EACC na kadhalika. Alafu sasa ubaya wa vyeti hivi vina expire baada ya mwaka. Kwa hiyo nimekuwa nikitoa mpya kila mwaka. Kuna sehemu zengine nilikuwa nikituma ombi langu la kazi mpaka nikaona ni kama kumpigia mbuzi gitaa. Ukija kusikiasikia vile watu hupata taabu baada ya kununua hizo nafasi kwa mapesa mengi. Pesa zenye hata sijawahi kuzifikiria, ingenifisha moyo sana. Hapo ndio ninashangaa sisi walalahoi nafasi yetu iko wapi? Mbona watangaze kazi, watutie hasara na kwenye madeni ya kutafuta stakabadhi hizo ilhali wanaowaandika tayari wanawajua. Ndipo nikasema, uchumi wa Kenya ni ule wa maskini kuzidi kuwa maskini na tajiri kuzidi kutajirika. Nimepeleka makaratasi yangu kwa kampuni zisizopungua mia tano. Hii Kenya ingekuwa yangu pia basi ningekuwa nipo sehemu flani inayoniwezesha kutimiza haja zangu za maisha.
Upo wakati hata najuta kwanini nilisoma. Mda wote niliotumia kusoma kwa shida pesa tumbi nzima zilizoenda shuleni, hivi ningepewa tu pale nilipomaliza sekondari nikajifungulia biashara naona ningekuwa mbali sana. Laiti walimu wa vyuoni wangetutayarisha kisaikolojia kuwa kuna na kukaa miaka bila kazi kama vile walivyotutia hamu ya kuwa tungepata kazi haraka sana, pengine mambo yasingekuwa magumu kwetu kama yalivyo sasa. Nimedanganywa na watu sana kuhusu kupata kazi. Nimepuuzwa sehemu nyingi sana ninazoomba kazi. Wanachokitaka wenye kampuni sijui ni kipi ambacho mimi sina. Kilichowazidi wenye kazi sijui ni kipi kilichopungua kwangu. MwenyeziMungu anajua zaidi. Enyi matajiri, munatunyima kazi mukiwapa watu wenu ni sawa, ila kumbukeni huenda kesho nasi tukawa hapo tukitakiwa kuwaajiri watoto wenu. Ya Mungu ni mengi.
Matangazo yenyewe ya kazi ni ya kufisha moyo. Wanaeka kuwa wanahitaji mtu mwenye ujuzi wa miaka kadhaa. Sasa sisi wengine tuliotoka vyuo vikuu mda usio mwingi tutaajiriwa na nani? Kwanini musitupe nafasi angalau mukatuonyesha kazi ndio nasi tuwe sawa? Mwisho wa siku tunasalia kubaki majumbani miaka na miaka. Kukaa nyumbani tu haiwezekani tena, hali zimekuwa ngumu. Tunatokea kufanya kazi za kujitolea, ndio ati tujulikanwe na “wakubwa” ambao wanaeza kutupa kazi. Kazi tunajitolea lakini tunaumia, nauli ya kuenda sehemu hiyo kila siku tuitoe wapi? Chakula? Tunafanya tu kwasababu hatuna budi, lakini tunaumia sana. Walakin, sio wote wenye akili hiyo, wengine huwa wahalifu ili kutafuta riziki. Na wengine wakitafuta ma sponsor ili nao wapate tonge la siku.
Kutafuta kazi imekuwa kama kutafuta pepo. Kuna wakati natembea barabarani naona wanawake wenzangu wananipita na magari nashangaa kwani hawa walitumia njia gani? Mimi nilikosea wapi? Wanasiasa ndio hata usiseme. Ni warongo kupindukia. Hawana wanachofanya, kazi kutuahidi na kututia tamaa za kupooza. Zaidi, wanatutia na hasara kwa juu za kuwaandama kila siku maafisini na hawako. Nimekaa nyumbani mda mrefu imefikia kutumiwa kama mfano na jamaa zangu ambao wanao hawataki kusoma. Wakikanywa kuhusu watoto wao utawasikia, “Fatma huyo amesoma mpaka University amefika wapi? Kila siku yuko barabarani tu na makaratasi.” Aisee! Inauma. Inauma tena sana. Kalenda iliisha maana kwangu pindi nilipopata kofi la ufahamu wa uhalisia. Sioni tofauti ya tarehe moja na tarehe thelathini, mwanzo wala mwisho wa mwezi. Siku zangu zote ni sawa, niamke nitafute hiyo kazi, nihangaike kupata riziki, nirudi kulala jioni. Kuna wakati mashoga zangu niliosaoma nao ambai walibahatika kupata kazi na jamaa pia, waliona heri wanitume kufanya shughuli zao town wakati wao wako busy makazini mwao alafu wanipe japo senti kidogo. Kikweli mimi ni mhitaji kwahivyo sikuweza kukataa, japo haikuwahi kuingia kwenye akili yangu kuwa ningefikia hapo. Nikasema haidhuru, muhimu nipate pesa au riziki ya halali. Nikawa naingia mjini nanulia watu vitu nikiwatumia. Ikafikia siku moja mtu akaniambia, “Sasa siku hizi umekuwa hamali”. Nilihisi kanitia mkuki kwenye moyo wangu. Nilishindwa nimjibu nini, nilimezea huku machozi yakinilengalenga. Kutafuta kazi kumenifanya niwe depressed mara nyingi sana.
Unapokuwa huna kazi na umekaa nyumbani mda mrefu, watu wanaanza kukudharau. Hata wale ambao hawakusoma lakini wamejaaliwa kwa njia moja au nyengine kuwa na pesa, wanakukejeli. Marafiki wanafiki nao wanakuhepa. Wanakuona huna usaidizi wa aina yoyote. Wewe ndio utakayetumika kutimiza mambo ya wengine. Inauma lakini ndio ukweli. Binafsi nimeona maisha ni yenye pande mbili, masikini na matijiri, wazuri na waovu, wenye imani na wenye kukejeli na kadhalika. Mapema mwaka huu nilianza kusomea shahada mpya ya ualimu, baada ya kuahidiwa na mtu kuwa kampuni yao itanismamia kunifundisha. Ni jambo ambalo nililifikiria kwa mda mrefu sana. Nilihofu kufanya uzamili katika sekta ya fedha baada ya kuona shahada yake imenisumbua mno. Nikaona heri nibadilishe nijaribu kitu kipya. Kitu ambacho nakipenda sana. Haya basi, nikafanya nilichotarajiwa kufanya na hatimaye nikajiunga katika chuo kikuu cha Kenyatta University hapa jijini Mombasa. Nilisoma mwezi wa kwanza na wa pili ilhali bado sijalipa ada. Kumuuliza jamaa aliyeniahidi, aliniruka futi mia, simu nikimpigia hakushika kamwe. Nikajaribu mara kadhaa kila siku hakuwa akinishikia simu. Nikaamua kupigia kampuni simu moja kwa moja. Kuulizia, niliarifiwa kuwa waliacha kitambo kulipia watu ada za shule.
Aidha, nilipoona upande mmoja umelemea ilinishuruti kutizama wa pili. Baada ya miaka ya kutafuta kazi bila mafanikio nikaamua kuangalia wazo la kufungua biashara. Nikajaribu kuangalia vipengo katika soko mbali mbali. Nashukuru nilipata mawazo si haba. Sasa kuja katika kuianza biashara yenyewe ndio nilikwama. Hakuna pesa. Kila umfuataye analia yeye njaa. Serikali wanatoa pesa kwa vijana, zinazowafikia wanaowataka wao. Kupata mfadhili wa biashara ikawa kama kupata kazi. Nikarudi palepale. Leo huyu anidanganye anataka kunisaidia nimfuate mpaka nijue kumbe kanitapeli, kesho mwengine naye azuke aniahidi kunisaidia nimfuate hadi mwishoe nigundue ana njama chafu. Mawazo yangu ya kufungua biashara yakasalia vitabuni.
Mara nyingi huwaza na kujiuliza, ama pengine riziki yangu iliandikwa nitaipata vyengine na sio kupitia kuajiriwa? Mwisho wa siku huambia wenzangu, maadamu juu yetu kuna paa yaani tumestirika kwenye majumba, tuwazima na afya yetu, tunapata cha kutia mdomoni basi tumshukuru MwenyeziMungu sana. Naamini ipo siku riziki zetu zitasimama. Ipo siku tutakuja kupata kazi au kuweza kufungua biashara zetu zitakazo nawiri. Siku yetu inakuja. Tuzidi kuwa na imani na kuvuta subira. Hakuna refu lisilokuwa na ncha. Tulipotoka ni mbali ila tunapoelekea ni karibu. Ewe mola wangu tujaalie na sisi kazi zenye heri nasi, zenye usahali na kazi zitakazo tukuza kiakili na kimali nasi tuje tuwasaidie wenziwetu, Ameen.