Picha: https://jurnalislam.com
Nawasalimu wendani, watoto watu wazima
Khabari ninawapeni, khabari zilizo njema
Atawasili mgeni, mgeni mwenye neema
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Ni mwezi wenye baraka, katuletea qahari
Na tena wa kusifika, na wenye mengi mazuri
Dua zetu Kwa rabuka, tuufunge bila shari
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Sote tunatarajia, kwa qamari kuandama
Ili kumshuhudia, mgeni aliye mwema
Ya rabbi tupe afia, tuufunge kwa salama
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Unapoyafanya mema, kwenye mwezi hu sharifu
Atakulipa karima, malipo ya maradufu
Basi ndugu hima hima, tuyaacheni machafu
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Tuhimizane kuswali, za faradhi na za sunna
tuinukeni laili, kumuomba subuhana
Tukithirishe amali, kuipigania jannah
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Nazo pia adhkari, tusizisahau nyuma
Tufanye ziwe kathiri, na tuzisome Kwa hima
Nyoyo zitajaa nuri, pia kujazwa ruhuma
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Mwezi mwema ramadhani, ndugu zangu mufahamu
Ni mwezi wa qurani, basi tushikeni hamu
Kwa pamoja tusomeni, maneno yake rahimu
Karibu mwezi karibu mtukufu ramadhani
Tarawehe tuswalini, na tahajud kadhalika
Tujae misikitini, tuzitafute baraka
Ziwe nzito mizani, qiyama kitapofika
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Mayatima masikini, tusiwaacheni nyuma
Na wote walio duni, tuwaonee huruma
Na tuwafuturisheni, ndio mwendo ulo mwema
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Ni mwezi wa itifaki, huleta watu pamoja
Basi tuacheni chuki, nawausieni waja
Zitatuondoka dhiki, na kuipata faraja
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Sio mwezi wa michezo, au mwezi wa kulala
Tuyaache makatazo, ndugu zangu hala hala
Ibada ndo ziwe nguzo, zisitupiteni swala
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Tusipotezeni muda, tukivipika vyakula
Ramadhani kina dada, sio mwezi wa chakula
Tutazikosa faida, faida zilizo aula
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Tuziacheni tabia, zile zilizo haramu
Uongo kuteta pia, nako pia kudhulumu
Tusije tukajutia, zisipopaa saumu
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani
Kadi tama nimefika, japo sijesha kunena
Ila nyi kufaidika, ndiyo yangu madhumuna
Wa Halima Farshika, hilo ndilo langu jina
Karibu mwezi karibu, mtukufu ramadhani