Nina swali ikhiwani,ninaomba munijibu
Limekaa akilini,nijibuni maswahibu
Naomba yenu maoni,tena kwa utaratibu
Je ni haki kuongeza,mke wa pili kwa siri?
_
Mke wako laazizi,barafu ya moyo wako
Kakupa mola mwenyezi,
Utimize dini yako,
Ila leo humaizi,wamficha mambo yako
Je Ni haki kuongeza,mke mwingine kwa siri?
_
Ni ruhusa sikatai, kutoka kwake rabbana
Sio kwamba haifai,jamani kuoa tena
Ila Ni jambo la hai,Ushauri kutakana
Je Ni haki kuongeza,mke mwingine kwa siri?
_
Ifikiri hiyo hali,’mkeo ‘takayokuwa
Kugundua jambo hili,kwamba wewe umeowa
Mfanyie usahali,ushauri kuchukuwa
Je Ni haki kuongeza,mke mwingine kwa siri?
_
Ila pia tafakari,zogo atakalozua
Ukitaka ushauri,huenda kakuzingua
Hivyo basi fanya siri,oa bila ye kujua
Je Ni haki kuongeza,mke mwingine kwa siri?
_
Aeza leta mashaka, Hilo ukimueleza
Akataka na talaka, na ndoa kuipuuza
Akavuka na mipaka,jamani kwa uke wenza
Je Ni haki kuongeza,mke mwingine kwa siri?
_
Hivyo simpe habari,kuilinda yako ndoa
Mke mwenza awe Siri,ndoa isingie doa
Ukitaka washa nari,basi Siri we toboa
Je Ni haki kuongeza,mke mwingine kwa siri?
_
Ni ruhusa ya karimu,hivyo mashaka ondoa
Sio Jambo la haramu,mke wa pili kuoa
Na pia sio muhimu,mke wa kwanza kujua
Je Ni haki kuongeza,mke mwingine kwa siri?
_
Akija kujua mbele,pia itakuwa kheri
Akileta makelele,mshauri asubiri
Mfanyie mema tele,ili awe na sururi
Je Ni haki kuongeza,mke mwingine kwa siri?
_
Mwishoni nimefikia,kwaherini waungwana
Mola ‘kitupa afia,tutazidi kujuzana
Jina mnaulizia? Naona mnanongona
Farwa Shariff nawambia,in shaa Allah tutaonana