Siku za hivi karibuni, kumekua na mwenendo mpya katika mawasiliano ya kijamii maarufu kama #Ifikie wazazi. Mwenendo huu unahusu picha za wanafunzi wa shule za upili. Picha ambazo hazikuwa na muonekano wakuvutia kimaadili. Hii imekusudiwa ili wazazi waone mambo wanaofanya watoto wao wakiwa shuleni.
Jambo hili naweza kulisawirisha na msumeno,hukereza mbele na nyuma.
Ni vyema iwapo wazazi watajuzwa na mambo yanayoendelea shuleni.
Hii inawapa nafasi adhimu ya kurekebisha panapostahiki marekebisho mapema kabla mambo kuharibika kabisa. Waama, usipoziba ufa utajenga ukuta na udongo uwahi ungali maji.
Ni uchungu sana kwa mzazi kumtizama mwanae akipotoka kimaadili na kukosa kufaulu kwenye sekta ya elimu.
Yakini, kumrekebisha mtu mbele ya adinasi lukuki sio kumrekebisha bali ni kumfedhesha. Fedheha huchangia kwa mkosa kutokubali makosa yake na pengine azidi kukosea. Mafunzo ya kidini ya kiislamu pia yanakana tabia hii. Ni vyema ikiwa mkosa ataelezwa kwa hekima na upole ili apate kuelewa uovu na madhara ya kosa lake. Ndiposa iwe rahisi kwake kuamua kubadili mienendo.
Pia,ni wajibu wa wazazi kubadilisha muono wao kuhusu kufuzu kimaisha. Elimu ya kidunia ni muhimu bila shaka,lakini umuhimu wake unapo zidi umuhimu wa kuwafundisha watoto kuishi kulingana na maadili ya kidini ya kiislamu,ndo pale kitumbua kiingiapo mchanga
Tukiangazia upande wa intaneti. Kumbukumbu za intaneti katu haziwezi kutoweka. Kwa hivyo picha zilizomo ndani bila kufutwa zitabaki humo milele. Jambo ambalo si la kupendekeza kwa wanafunzi hao. Huenda mtu baadae akabidilika, akawa mtu mwema. Sasa kumbukumbu za picha zile za kitambo zitakuwa zikimshushia hadhi yake. Au pengine mtu kaoa au kaolewa na amezaa watoto. Baadae watoto wake wakija kuona zile picha itakuwa ni aibu kubwa.
Ni wangapi watoto wameruhusiwa kutumia mtandao bila kuhadharishwa kuhusu uovu, hatari na hasara iwezayo kupatikana kupitia wavu huu uliotuzingira? Ni wazazi wangapi wanaelewa kinaga ubaga maovu yawezayo kupatikana kupitia mitandao? Iwapo unaelewa basi jee uko radhi kumtosa mwanao mwituni? Ajuae ana hasara na asojua ana hasara zaidi.
Daima, kosa halirekebishwi na kosa. Likiwepo jambo lisilo la sawa, basi namna mwafaka ya kulisawisha ni kwa kutumia jambo la sawa.Kuweka picha za ukosefu adabu za wanafunzi kwenye mitandao ya kijamii sio sawa, hivyo basi haisaidii katika kuwaboresha kimaadili bali inazidi kuzorotesha. Kwa mfano, wapo wanafunzi ambao wataona ni kama sifa kwao, au ndio wanapata umaarufu, baadaye wazidishe ukosefu wa adabu.Hapa tutakuwa tumebomoa au tumejenga?
Mkuki kwa nguruwe tu kwa binadamu ni mchungu bwana! Hivi ingekua ni dadako au kakako kaanikwa hivyo kwenye mitandao ya kijamii, ungefurahia? Mtume wetu Muhammad (rehma na amani zimshukie yeye) alituusia tupendelee watu yale tunayoyapendelea nafsi zetu. Tusifurahie kuona na kusambaza picha za wenzetu kiholelaholela wakati tunajua fika sio haki. Mstiri mwenzako. Hakuna aliyekamilika ila MwenyeziMungu. Kuna leo na kesho. Mimi siijui kesho yangu itakuwaje, pengine nitakuwa mtu mwema,au mtu muovu, au hata nitakua hai ama nimefariki. Wewe mwenzangu unaijua kesho yako?
Naomba MwenyeziMungu awaongoze vijana wetu, awatie fahamu, awatulize mabongo yao, waeze kumaliza kusoma salama salmin.. Amin