Utungo wangu naanza, mie mwana wa kipwani
Naandika na kuwaza, mazuri yalio ndani
Mola nipe muangaza, hadi pale kikomoni
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Nimezijaza salamu, kwenye bakuli la sini
Nikazipamba kwa hamu, vilua na asumini
Nikaongeza utamu, kutia waridi ndani
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Na sijamaliza waja, kutoa zangu salamu
Nimezivisha makoja, ziwapendeze kaumu
Tuzichambueni hoja, kuisifu pwani tamu
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Pwani iliyo na mengi, mazuri ya kupendeza
Pia sifa kila rangi, kote zimehinikiza
Wala uzushi situngi, insi ‘kawapoteza
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Kama mama alozaa, najivunia na pwani
Situngi kuwahadaa, na sitii chumvi ndani
Pwani yetu inang’aa, mithili mwezi angani
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Sana ninafurahia, kuwa mzawa wa pwani
Sehemu ilotulia, isiyo na kisirani
Wale wanoichukia, bila shaka mahaini
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Pwani kwangu siyo jina, wala mahala pekee
Inayo kubwa maana, pwani yetu iko mbee
Fahamuni waungwana, walozama waelee
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Siachi kuisifia, miundo msingi pwani
Imerahisisha njia, ya kukua maishani
Na ikairembesha pia, sehemu yetu ya pwani
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Ukitaka tamaduni, bila shaka njoo pwani
Tena za uswahilini, pia zile za kigeni
Waja wana ihsani, wanawapenda wageni
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Mgeni akiwajia, vizuri humkirimu
Vyema ‘kamuandalia, vyakula vitamu tamu
Mgeni hufurahia, ‘karudi na tabasamu
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Udugu umekithiri, na umoja kadhalika
Watu waishi vizuri, pamoja kufurahika
Na hilo liko dhahiri, kote linafahamika
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Majirani ‘meshikana, wanaishi kama ndugu
Mno husaidiana, kukitokea vurugu
Aidha wanapendana, kwa mapenzi ya kidugu
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Na kukiwa na harusi, au pia na matanga
Hujumuika insi, kibwebwe wakajifunga
Hufanya mambo rahisi, mikakati kuipanga
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Sitomaliza kutunga, nisipotaja vyakula
Huo wa nazi mpunga, kwa nyama maziwa mala
Viazi vya kukaanga, katiye kuna masala
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Nikisema sivitaji, itakuwa si vizuri
Si vingine ni vipaji, kwa sana vimekithiri
Mfano uigizaji, nao pia ushairi
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Nao upande wa dini, waungwana mufahamu
‘mekita mizizi pwani, mabanati maghulamu
Hujaa misikitini, kuomba kwake rahimu
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Ni tamu lugha ya pwani, maswahibu sidhihaki
Nyingineyo mi sioni, kwayo mimi ni ashiki
Wengi wanaitamani, meru na hata nanyuki
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
Sifa ni kathiri sana, ‘kiendelea ‘takesha
Kwaherini waungwana, uwanjani nawapisha
Na pia sina khiana, pwani nawakaribisha
Jamani kutoka pwani, ni raha iso kifani
