Tulishuhudia uzamani ukififia, usasa ukiingia
Kaseti na disketi tangia, sasa wi-fi na usb-c twawania
Mawasiliano yalipokuwa kizungumkuti, sasa twatumia simu za tachi
Zama serikali ikiwa Nairobi kati, tukapitia mamlaka pacha na sasa kaunti
Tukaihama mishono na mavazi ya tangu, waume wakabana wake wakafupisha
Aliyesalia bangubangu, basi hajui taiti hajishughulishi kupindisha
TUMEYAONA SISI KIZAZI MPITO, THE TRANSITION GENERATION
Teknolojia ikagura karne za jiwe, mitandao ikapenyeza kwa kasi
Kukipingwa umagharibi mashinani usiwe, Fesibuku Instagramu na Tikitoku zikaasi
Kesi vibarazani zilijadili mashamba, hadi korti zikawa maskani za wataliki
Wachopozi walivokuwa wakiramba, sasa wadukuzi mitandaoni ndio hawashikiki
Sanaa halisia zilivopendwa, zikazamishwa na waiga ughaibu
Lugha na lahaja za asili zikatwezwa, visasa vikasambaa ajabu
TUMEYAONA SISI KIZAZI MPITO, THE TRANSITION GENERATION
Mwanamke alipothamini haiba, usasa ukamvua sitara moja moja
Uraibu ulipokuwa haujapata huba, mara tukaletewa stimu mpaka za mirija
Unakumbuka hekaya za wakoloni, wale waliotia uhuru wetu komeo
Madaraka tukapewa tukasongani, mbio kuukumbatia ubeberu mamboleo
Ardhi zilizoshiba rutuba kukithiri, zikakaushwa kwa kiangazi cha njaa
Sura zilizokuwa kwa neema zikinawiri, zikapiga matuta kwa dhiki na balaa
TUMEYAONA SISI KIZAZI MPITO, THE TRANSITION GENERATION
Tuliuona ujirani mwema, kabla utumiwe kupekuana
Mahusiano yalikuwa ya nia njema, sasa masilahi ndio yanatangulizana
Wadau wa dini walihishimika, maabadi wakayageuza mtaji wa maisha poa
Wajumbe feki kuibuka, wachekeshaji wakatoka vijiweni hadi kwenye majukwaa
Wakubwa walivowahurumia wadogo, wachanga walivowanyenyekea wakongwe
Yote yakazikika kama zao la muhogo, tafrani baina yao zikahanikiza kwa shangwe
TUMEYAONA SISI KIZAZI MPITO, THE TRANSITION GENERATION
Chonde chonde samahani hazikukauka vinywani, dharau na misonyo ikarithi upesi
Tabasamu za dhati zilizotamanika asilani, zikatoweka zikabaki za hadaa na kughasi
Walikuwepo wenye miraba asili wachapakazi kikweli, kwa bahati mbaya walizaa vifito vivimto
Siha walikizijenga si kwa zohali bali kazi na wali, kisha mlo na mienendo ikageuka ndio ikawa ‘finito’
Nganoni mifano ya tamaa tuliisikiya tu, kumbe ilitutayarisha na yatakayofuata
Midahalo ilitasua migogoro ya himaya na mwitu, vita vikafuata mpaka kwenye migongano ya mtungi na kata
TUMEYAONA SISI KIZAZI MPITO, THE TRANSITION GENERATION