Mwandishi: Fatma Shafii
Nifanye nini? Nitasema nini? Nimfiche wapi? Nitafuta na nini? Damu inazidi kutawanyika. Nitamtoa vipi? Nianze wapi? Siamini! Nimeua kweli ama ni macho yangu? Pengine kazirai tu.
Nimechanganyikiwa. Nani wa kumlaumu? Sigara? Pombe? Mugokaa?Au mimi mwenyewe? Nikitazama nje ya dirisha kumejaa wazee wanakunywa kahawa kwa ‘Mbwana Redio’. Siwezi kumbeba nikiwa pekeyangu. Ama niende kituo cha Central polisi makadara, nijiseme? Loh! Mungu wangu.
Nimemuua mke wangu! Kwa uraibu wangu ulonishinda kuuacha. Watoto wakirudi kutoka madrassa nitawaambia nini? Najuta! Tena najuta sana. Au nikimbie mji? La siwezi kukimbia. Kila siku tunagombana lakini ugomvi wa leo umeshika bendera. Nitajitetea vipi? Hivi kweli MwenyeziMungu atanisamehe?
Sasa ndio nakumbuka ushauri wa wazazi wangu na marafiki zangu. Natamani wakati urudi nyuma nijirekebishe lakini wapi? Yakimwagika maji katu hayazoleki.
Doh! Ama nijiue tu? La! Sidhani kama ni wazo zuri. Wakati unazidi kuyoyoma na damu ishatapakaa sebuleni kote.Ya Ilahi! Mwili wangu wote unatetemeka tem tem. Saa za adhuhuri zimeshafika na mwadhini unaadhiniwa. Najua fika kuwa watoto washatoka madrasa. Au niseme ni jini? Lakini itakua jini kafanyaje? Mmh! Hapa nitaonekanwa mjinga. Natamani ardhi ipasuke inimeze mzima mzima. Laiti ningelijua. Kweli majuto ni mjukuu huja baada ya kitendo.
Wacha nichangamke nifute damu kwanza.
“Ngongongongo! Mamaa! Maaa!…”
Watoto wanabisha. Nahisi moyo unapasuka. Malaika yote yanasisimka. Nimekodoa macho. Kitambara cha kudeki chote kimekua chekundu. Sijui nijirushe dirishani? Hapana! Hapa najidanganya. Nikachukua simu na kuwapigia zahanati ya Kaderbhai ili walete karandinga.
“Ngongongo! Mamaa fungua mlango naskia kuenda haja” Alisema Ahmadi ambae ndie kitandamimba.
“Wototo wangu! Nendeni kwa bibi sioni ufunguo na mama yenu katoka!”
Maneno haya hata sikuyapanga. Nilijiskia naongea tu. Wanangu walijibu,” sawa”, kisha wakaondoka. Haikuchukua mda mwingi, karandinga ikafika. Nikasikia mlango unabishwa tena. Sikusita kuufungua. Walishtuka kuona hali ilivyo. Waliniuliza maswali chungu nzima ila hakuna swali hata moja nilioweza kujibu. Mke wangu akafanyiwa usaidizi wa kuzuia damu isiendelee kutawanyika. Akafinikwa na shuka mwili mzima hadi usoni. Waliniondoa hapo subeleni. Mimi huku nikilia naskia wanapiga simu nyingi. Mda usio mchache kulikuja mapolisi. Wakanifunga pingu. Mara nikaona wazazi wangu, bibi na wanangu wakiingia. Aibu! Aibu ilinivaa mwili mzima nikashindwa kumtazama yeyote ozini. Majirani walijaa hapo, wengi walikua wikipiga gumzo ya tukio hilo lililowashtua huku wakiwa kwa mshangao. Moja kwa moja nikapelekwa hadi kituo cha polisi. Bila shaka nilikua na hatia.
Nimeua. Nimemuua mke wangu kwa kumtia kisu cha tumbo, hali yakua yeye ni mja mzito. Sababu ni mke wangu kujaribu kunieleza kuwa uraibu wangu wa pombe, sigara na mugokaa unaleta ukorofi na ufukara katika nyumba. Nilikua mshindani. Sikutaka kukubali ukweli. Nilikua sipeleki pesa nyumbani. Wanangu walikuwa wakienda shule bila pesa. Mda mwingine chakula kinakosekana nyumbani. Wala sikuwa nikiona ni shida yoyote. Muhimu niwe na pesa za mugokaa. Loh! Ulimwengu leo umenipa funzo kubwa. Tulianza ugomvi mkubwa tukamalizia na vita. Mwishoe nimeua. Siamini. Najuta sana. Hivi nitawaambia nini watoto wangu na wazazi wangu? Ama kweli, asiyesikia la mkuu huvunjika mguu.
Hatimaye, nilihukumiwa kifungo cha maisha katika jela ya Shimo La Tewa- Shanzu. Watoto wangu walichukuliwa kulelewa na bibi yao. Lilikuwa tukio la kustaabisha na kuhuzunisha sana. Nimekosa kulea watoto wangu mwenyewe. Sina la kufanya ila kujilaumu maisha yangu yote huku nikijaribu kuzoea maisha mapya huku jela. Jambo ambalo sikulilalia wala kuliamkia. Nitaishi nikimkumbuka mke wangu pamoja na wosia wake hadi mwisho wa maisha yangu. Najuta sana.
Sasa nachukua fursa hii kuwausia wenzangu wenye uraibu wa aina yoyote. Iwe ni sigara, au pombe, au miraa, au bhangi, au bugizi yaani madawa yote ya kulevya, kuwa URAIBU NI SUMU. Uraibu ni kitu kibaya sana. Inavunja furaha ya nyumba. Inaleta ufukara, ukorofi na ugomvi mwingi usio wa faida. Tujaribu kadri tuwezavyo kuishinda nafsi zetu ili janga hili lipate kutuondokea. Familia ni aula kwetu kushinda madawa ya kulevya. Zipo namna za kujistarehesha pamoja na kuwa na familia yako. Njia hizi ndizo zinazotushikanisha zaidi na watoto wetu na vilevile tunapata fursa ya kuwajua na kuwaelewa vizuri. Badilika leo! Kesho haijaahidiwa. Muusie na mwenzako pia ili tuweze kuboresha jamii yetu. Tahadhirini! Mwiba wa kujidunga hauambiwi pole.