Ayamu hizi, imekuwa jambo la kawaida kuwaona vijana wadogo kwenye mahusiano ya kimapenzi, kinyume na maamrisho ya dini. Nastaajabishwa sana na tendo hili kwani nashindwa kufahamu ni penzi la aina gani. Kwa kweli ni jambo la kusikitisha mno, kwani janga hili limewaathiri hadi watoto wa umri mdogo. Wamejiingiza kwenye mambo ya upotofu. Mambo yasiyokuwa ya sawa na yenye kuwatia madhambini.
Iweje tupende viumbe vya Mwenyezi Mungu na tumsahau aliyeviumba? Kwanini tusifuate maamrisho yake? Mwenyezi Mungu pekee ndiye anayetufahamu vizuri. Anajua kinachotufaa na kisichotufaa. Ndiposa, yapo mambo aliyoyakubali tufanye na yale aliyotukataza. Kila tulilokatazwa lina madhara kwetu. Huu ndio upendo wetu kutoka kwa mola wetu. Yatupasa kufuata maamrisho hayo ili tufuzu hapa duniani na kesho akhera.
Kila jambo lina wakati wake. Walakin, wanaadamu sisi tudhaifu na tuna pupa ya kufanya mambo. Upo wakati muafaka wa mahusiano haya. Nao ni wakati wa baada ya kufunga ndoa. Kabla ya hapo, inatulazimu sisi kuliepuka janga hili kadri tuwezavyo. Ukijaribu tu kujiingiza, utabaki kwenye maovu hayo na itakuwa ngumu kutoka. Waama, mchovya asali hachovyi mara moja ndio sababu MwenyeziMungu anasema kwenye kitabu chake tukufu,
“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (Sura ya 17 aya ya 32)
Anajuwa zaidi maafa yake kwetu sisi ndipo akalikataza tendo hili.
Vipi pendo hili liwe sawa ikiwa tunajuwa fika kuwa kila mda tukikaa na kuongea, tukitumiana arafa kwenye rununu au hata tukionana na kufanya mambo mawili matatu, inazidi kutuleta karibu na adhabu za moto? Litaweza vipi penzi hili liwe sahihi ikiwa matokeo yake ni madhara na madhila chungu nzima? Tafakari! Tena uovu huu unakua. Yaani kila ukikua kiumri na bado upo kwenye mahusiano haya, matendo tufanyao pia yanakomaa.
Tuchukulie mfano, kijana amemaliza darasa la nane tu. Akaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi wa haramu. Kila kukicha anapoteza mda wake huku akiongea na mpenziwe. Mara wanapanga kuonana maana arafa tu hazitoshelezi hamu zao. Kijana anaingia kidato cha kwanza. Anapata mpenzi mpya. Masomoni, hafaulu. Anazidi kukomaa kwenye uovu na afikapo kidato cha nne, Ametembea na wapenzi karibu watano au sita. Hakuna alomridhi. Anabadilisha kama vazi. Kwa huruma ya Mwenyezi Mungu akajaaliwa kujiunga na chuo kikuu. Huku sasa ndio mapenzi yale yanaelekea kuchukua shahada. Kama kawaida, mpenzi ni mwengine. Utapata mschana amesahau kabisa kilichompeleka chuoni huko. Keshakodisha nyumba na mpenziwe. Wanaishi pamoja kama mke na mume. Asubuhi, amtayarishie staftahi, mchana chamcha na jioni, chajio kiko mezani. Mwanafunzi huyu ndiye kawa mfuaji. Yaani anamfulia mpenziwe vichupi wakati wazazi nyumbani wanang’ang’ana kwa udi na uvumba wakimtafutia karo na pesa za matumizi ili mwana wao asiteseke. Balaa hizi! Tena mfano huu una sahali. Wapo wanaochezewa na wapenzi wao, jambo hilo likawaathiri na kuchangia kwa wao kuingilia kwenye mihadharati, wakijidanganya kuwa wanapunguza maudhiko. Ndipo tunamkosa kijana huyo kabisa. Salama awe kijana huyo katubia baada ya hapo, wengine hutoka vyuo vikuu na kuja kupata wapenzi wapevu. Yaani mtu anatembea na mpenzi wa rika la mzaziwe. Chambilecho wazee wa busara na tabasuri tepetepe, “ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.”
Mahusiano haya huja na kuathiri maisha yao hata pale wakiwa kwenye ndoa zao. Heshima baina ya mke na mume hupungua kwani mke au mume yule aliolewa au kaoa akiwa tayari keshapevuka kwenye suala la mapenzi. Pengine mfano ikiwa wanandoa hao walikuwa wapenzi kabla kuoana, basi huwa wameshazoeana hata kabla ya ndoa. Hii huchangia kwa wao kuchokana haraka na pengine unga ukizidi maji huenda wakaachana. Hata hivyo tumeambiwa zinaa ni deni. Leo wewe wakopa, kesho nani katika aila yako unatarajia alipe deni? Tutafakari zaidi.
Pengine tuangazie sababu chache za vijana kujiingiza kwenye mambo haya. Kwanza ni malezi. Ndiyo, wapo wazazi wanaojitahidi vilivyo kuwakuza watoto wao kwenye malezi bora. Wapo pia walio na udhaifu fulani kwenye malezi yao. Na hatimaye kuna ambao hawashughuliki kabisa na vijana wao, jambo ambalo ni baya sana. Tukiwakuza watoto wetu vizuri tunaijenga jamii kwani watoto wenye maadili mema ni nuru katika jamii. Mzazi anafaa kujikaza katika kumlea mtoto. Amkataze jambo lisilo sahihi pasi na kurudi nyuma. Aifikirie kesho ya mtoto huyo itakuwaje ikiwa leo yake anamlegezea kamba. Hivi tukiwapa simu watoto wenye umri wa chini ya kumi na nane, tumewaelekeza vipi? Tunajuwa fika kuwa simujanja zile zimebeba ulimwengu mzima. Yaani maovu na mazuri. Kwahivyo upo uwezekano wa mtoto yule aidha kuongoka au kupotoka. Basi mbona tuhathirishe maisha yao? Mbona tuwanunulie uangamizi na mikono yetu wenyewe. Daima tukiwalea watoto wetu vyema itakuwa vigumu kwa wao kuharibika. Tusisahau kuwaombea kwa Mola awaongoze na awalinde popote walipo. Juhudi za malezi ni muhimu walakin dua ya mzazi kwa mwanawe ni muhimu zaidi.
Aidha, katika malezi. Waschana wakuzwe wakiwa na haya. Kwani haya imetokamana na imani. Wazazi wanafaa kuelewa mazingira aliyokuwa mtoto yule. Wanatupeleka vyuo vikuu ila wanakosa kuzingatia kuwa sisi kama watoto tumeshakua wakubwa. Tunazo hisia kama mtu mzima yeyote. Twaeza kuona na kutamani. Chuoni kule kuna uhuru na faragha kubwa. Yaani mwenye kuangamia atazidi kuangamia. Ni majaribio makubwa kwetu. Ndio tunajaribu, ila ni ngumu. Ndiposa, ninatuma ujumbe kwa wazazi wote wenye watoto katika vyuo vikuu kutumia shairi hili.
LEO TANENA KWELI.
Leo nitanena kweli, yaliyo mwangu moyoni
Siezi kustahamili, kwani tumo madhambini
Wengi tumekaa tuli, twashindwa tufanye nini
Enyi wazazi wawili, mimi nawaulizani
Kutizama wanandoa, je kuna ubaya gani?
‘Metupeleka shuleni, chuo kikuu hususani
Twawashukuru jamani ,ila tumo matatani
Mumetupa mtihani, hisia kutobaini
Twazuia kisa dini,si rahisi abadani
Kutizama wanandoa, je kuna ubaya gani?
Dunia i mikononi, akhera i visogoni
Leo niko masomoni, kesho ‘na mwana tumboni
Mwahofu ya duniani, na sisi tumapitoni
Naomba tuozesheni, tuwache huko kuzini
Kutizama wanandoa, je kuna ubaya gani?
Kama tumeridhiana, ni vyema kutuozesha
Kuliko mukitukana, na huba latukimbisha
Kunena mimi ‘tanena, ‘kikosa nirekebisha
Hivi hisia hatuna? Kwani sisi madirisha?
Kutizama wanandoa, je kuna ubaya gani?
Tamati nimefikia, hoja nimewaachia
Mambo yote kiwambia, nahofu mutazimia
Lau mutazingatia, muje kutusaidia
Sana tutafurahia, dhambi kutupunguzia
Kutizama wanandoa, je kuna ubaya gani?
Pili, ni shinikizo rika. Hili ni tatizo sugu linalowaathiri vijana wengi. Kupotezwa ni rahisi haswa pale kijana anapotaka kuwa sawa na wenziwe. Kwa hivyo, ni muhimu kuwafunza dini watoto wetu na kuhakikisha kuwa imani zao ziko sawa. Aidha, kuwaeleza jinsi ya kuchagua marafiki wema. Nasi pia kama watoto ni jukumu letu kuwa waangalifu katika kuchagua maswahiba ili keshole tusije kujuta.
Mwenyezi Mungu asema,
“Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume!
Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!” (Sura ya 25, aya 27- 28)
Tuchukue mfano huu mzuri. “Mfano wa rafiki mzuri na yule mbaya ni kama sawa na mbeba mafuta mazuri na muashi (mfua vyuma na kutengeza vitu vya chuma). Mbeba mafuta mazuri ukiwa naye karibu,utapata kuhisi harufu nzuri. Muashi ukiwa naye karibu, huenda akazichoma nguo zako au utanuka harufu mbaya.’
Waswahili nao walipata waliposema, ‘Nioneshe rafiki zako, na mimi nitakutajia tabia zako.’ Kwa kuzingatia ukweli huu, wosia wa Mtume rehema na amani ziwe juu yake amesema
“Mtu hufuwata dini (mwenendo, imani na mila) ya rafiki yake. Na atazame kwa makini mmoja wenu nani anayemfanya rafiki yake.”
Vilevile, iwapo tumeshaingia kwenye mtego huu na maadamu tungali hai basi fursa bado iko. Bado hatujachelewa. Tunayo fursa ya kurudi nyuma, kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hatimaye kujirekebisha pamoja na kurekebisha wenzetu. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe. Wala hakuna dhambi kubwa kuliko huruma yake. Anasema Mwenyezi Mungu,
” Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao- na nani anaye futa dhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu? – na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua.” (Sura ya tatu, aya ya 135)
Tazama, huu ni mtihani kwetu sisi vijana kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ila tukumbuke kuwa Mwenyezi Mungu asema,
“Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadri ya iwezavyo” ( Sura ya pili, aya ya 286)
Kwa hivyo ni changamoto ambayo inayo suluhu. Suluhisho ya kufunga iwapo mmoja wetu hana uwezo wa kuoa,(swaum) ni mojawapo tuliyopewa na Mtume wetu. Kufunga kutachangia kwa kuweza kuzizuia hisia zetu. Pili, ni kusubiri. Subira huvuta heri. Inatulazimu kusubiri hadi pale wakati tulioandikiwa na Mola kuoa au kuolewa ufike. Muhimu, ni kuijuwa dini yetu vizuri na kuitenda.
Kwa hakika, ikiwa ni mapenzi basi tunafaa kumpenda Mola wetu. Hakuna majuto yoyote tutakayopata kwa ajili ya kumpenda yeye. Ndiyo, nafahamu vizuri kuwa kuepuka matamanio haya ni dharubu lakini haimaanishi kuwa haiwezekani. Hatuwezi kushindwa kuepuka janga hili ikiwa tumempa kipaumbele MwenyeziMungu. Isitoshe, tayari alishatuandikia watakao kuwa wake na waume zetu kabla hata hatujazaliwa. Kwahivyo mbona tujitese kwa pupa zetu. Tunafaa tusubiri na tuwe na imani kuwa apangalo yeye ndio bora kwetu.
Mwenyezi Mungu atulinde kutokamana na mahusiano haya haramu. Azipe subra nyoyo zetu. Atujaalie wake na waume wenye dini, wazuri na wapenda amani walio na kheri na sisi. Amin.