Kuche kusiche, hatimaye kulikucha, giza likatoweka na mwangaza ukashika usukani. Asad, kijana wa miaka kumi na tatu, mwenye kimo cha wastani, rangi ya maji ya kunde, mwembamba na nywele zilizolaini, alidamka kutoka kitandani kwake na kuelekea hamamuni. Tayari kashaanza shughuli za kuenda shuleni. Naam, siku njema huonekana asubuhi, walakin kwa Asad hakukuwa na tofauti za siku za maisha yake kwa miaka mingi sasa. Kama ilivyo ada, yeye huwatayarishia ndugu zake wadogo maji na kuwaekea nguo zao za shule tayari.
“Wewe punda! Mbona umekuwa mvivu siku hizi? Hadi sasa ndugu zako bado hawajaoga! Umekuwa ukifanya nini tangu ulipoamka?” Alipayukwa Bi. Halima.
Bi Halima ni mama wa kambo wa Asad. Alikuwa mrefu, mpana kimwili, mwenye macho ya chawa kama mchina na mweusi tititi. Kwa hakika, Asad alikuwa mtoto yatima. Nina wake wa kumzaa aliaga dunia miaka hamsa iliopita. Babake alikuwa angali hai ingawa ni mfanyabiashara wa nchi ya nje. Kwa hivyo, mara nyingi hakuwa nyumbani.
“Hapana mama, tayari nishawaekea maji ya kuoga ndio ilikuwa naelekea kuwaamsha.” Alijibu Asad huku akitetemeka temtem kama ukuti wa mnazi upeperushwao na upepo wa kusi. Kwa haraka, aliwatayarisha nduguze na hatimaye wakatoka na kuelekea shuleni. Shule yao ilikuwa mtaa wa Kizingo jijini Mombasa iitwayo Serani.
Shuleni,katika darasa la saba, usingeweza kupita darasa hilo bila kusikia sauti ya Asad kwasababu alikuwa mchangamfu na mwerevu. Yeye hutokea kijana wa kwanza au wapili. Alijitahidi kwa ujino na ukucha kufua dafu masomoni. Alifahamu fika kuwa elimu huleta matumaini ya ufanifu maishani. Siku hii shuleni haikuwa kama ya kawaida kwani shule ya Serani ilipata mwalimu mgeni naye alikuwa mwalimu wa kipindi cha mazoezi.
Bwana Hamadi, alikuwa barobaro mwenye miraba minne, mrefu, na mweupe kama theluji. Pindi ilipofika wakati wa somo hilo kwa darasa la saba, wote walitawanyika uwanjani huku furaha zimewajaa na vilevile hamu ya kutaka kujumuika na mwalimu wao mpya. Bwana Hamadi, alikuwa tofauti na walimu wengine kwani michezo yake ilikuwa mingi, ya ucheshi na uchangamfu mno. Baada ya kucheza michezo anuwai wanafunzi walionekaniwa kuwa wako hoi. Hivyo basi, aliwaamrisha wanaume wavue mashati wafunge kwenye macho yao. Wakalalamika kuwa wamechoka ila aliwaahidi kuwa itakuwa mchezo wa mwisho siku hiyo. Bila kusita, walifanya hivyo.
Jambo la kustaajabisha , aliuona mgongo wa Asad ukiwa umejaa alama zisizoeleweka. Zilikuwa nyingi, zipo zilizokuwa kubwa na pia ndogo. Kulikuwa na alama ndefu na fupifupi. Nyingi zilikuwa nyekundu. Alikonda kiasi cha kwamba ungehesabu idadi ya mifupa kifuani. Umbo lake lilikuwa kama mwenye mtapiamlo. Ungalimwona, ungalimhurumia upeo wa kumhurumia. Bwana Hamadi alishtuka sana. Alibaki kinywa achama kiasi cha mheshimiwa nzi kujenga makao dundumioni. Hakuamini macho yake. Baada ya kipindi hiko alimwita Asad na kumuuliza ni jinsi gani alipata alama hizo. Asad alikana kumweleza. Hakutaka kusema lolote kuhusiana na alama hizo. Mwalimu alijaribu kadri awezavyo kumlakini ili Asad afunguke walakin juhudi zake hazikufua dafu. Jambo hili kwa mda mrefu lilimkera sana Bwana Hamadi, akawa anampenda zaidi Asad kuliko wanafunzi wengine. Yeye pekee ndiye aliyeweza kuuona unyonge wa Asad katika tabasamu yake.
Usiku mmoja, ndani ya nyumba ya Bi Halima, kulikuwa na anga ya hofu kwani maji mtaa wa Kibokoni yalikatika ghafla bin vuu. Nje ya nyumba, ungalisikia sauti ya mitungi iliobebwa na watu waendao kuteka maji. Kwa ukali, mama huyo alimbumburusha Asad kutoka kitandani na kumwamrisha akateke maji ili ajaze kwenye pipa la hapo nyumbani. Kwa hakika, pipa hilo lingehitaji mitungi ishirini ili kujaa. Asad hakuwa na budi. Aliamka na kutoweka kuenda kisimani. Japo alikuwa na machovu ya siku, alijikaza na kuifanya shughuli hiyo kwa makini. Kwa bahati mbaya, alipokuwa akibeba mtungi wa akhiri alijikwaa kwenye ngazi, mtungi ukamwangukia miguuni kusababisha maji yale kumwagika. Punde si punde Bi Halima alitokezea kutizama kilichotokea. Kwa hasira alirudi chumbani kwake na kuchukua mkia wa taa. Hofu ilimteka nyara Asad, akaduwaa na kukosa la kufanya. Kijasho chembamba kilichirizika chiriri kwapani. Alimpiga Asad kipigo cha punda huku akimtukana na kumuuliza ni kwanini hakuwa makini. Asad alipiga yowe ila hakuna yeyote aliyetokea kuja kumnusuru. Sauti ya Asad ilisikika iikirudi chini na mwishoe kimya kilitanda. Kumbe alikuwa amepoteza fahamu. Bi Halima alimbeba akamuingiza ndani na kumshughulikia hadi alipopata fahamu zake. Jambo hili halikumshtua hata chembe mama huyo katili kwani haikuwa mara ya kwanza kutokea.
Liwike lisiwike, kutakucha! Hatimaye alfajiri pevu ilijiri. Asad aliamka akiwa amedhoofika kiafya. Alihisi maumivu mwili mzima hususan miguuni. Hana ngoma hana maulidi. Hakukumbuka vizuri kilichoendelea baada ya yeye kuchapwa. Sura yake iilionekanwa kuwa na huzuni sana na hakuwa mzugumzi siku hii. Jambo ambalo haikuwa kawaida yake. Aliharakisha na kuwatayarisha wadogo zake na kuelekea shuleni. Darasani, alisinzia sana. Ilipowadia mwia wa mapumziko alienda guu mosi guu pili mpaka kwa Bwana Hamadi. Akamweleza yote yanayomkumba hadi kufikia kisa cha usiku huo uliopita, huku machozi yakimtiririka tiriri. Kwa maisha anayopitia, alitamani ardhi ipasuke immeze lakini hizo zilikuwa ndoto za Alinacha .
“Mwalimu, lau ingewezekana ningetaka sana mama yangu arudi duniani japo kwa siku moja tu niuhisi tena upendo wa mama.” Alisema Asad kwa huzuni sana.
“Usijali Asad, hakuna refu lisilokuwa na mwisho. MwenyeziMungu akipenda leo hii ndio itakuwa mwisho wa mateso yako.” Alimjibu Bwana Hamadi huku akimpapasa Asad mgongo.
Bwana Hamadi alienda kwa mwalimu mkuu na kumweleza yaliojiri. Wote wawili walichukua hatua ya kuenda kituo cha polisi cha Central iliyoko mtaa wa makadara na kuripoti. Bi Halima alikuwa akimshtua Asad kuwa iwepo atasema anayomfanyia kwa mtu yeyote atamuua. Hii ndio ilimsababisha Asad kutoyaongea yanayomsibu kwa muda mrefu sana. Aidha pia hakuweza kumwambia baba yake mzazi pindi anapokuja kutoka safari. Mama huyo alikuwa mara kwa mara akimnyima chakula. Kando na kumtandika ovyoovyo kutumia mkia wa taa kwa sababu ndogo ndogo. Tazama, hakukubali kamwe Asad amwite ‘mama’ wala ajumuike na ndugu zake wadogo. Alimfungia chumbani wakati wenzake walikuwa wakitoka kuenda kucheza. Iwapo utamkosa kitandani, basi bila shaka atakuwa yupo jikoni anaosha vyombo, au varandani anafua nguo za familia au pengine umkute kisimani anateka maji.
Polisi, mwalimu mkuu, Bwana Hamadi na Asad waliandamana moja kwa moja hadi nyumbani kwa kina Asad. Bi Halima alikuwa kakaa sebuleni anatazama runinga.Miguu yake minene kaiweka juu ya meza, na kando yake ameweka maji ya tamu ya ukwaju anajiburudisha.
“ Hodihodi!” Alisema mwalimu mkuu, huku akibisha mlango ule kwa nguvu na hasira.
Bi Halima, bila kusita alijibu,
“Karibu, subiri kidogo tafadhali.”
Alinyanyuka kutoka kochi lile na kukimbilia chumbani ambapo alichukua kanga na kujitanda. Kisha akaelekea kufungua mlango. Alishtuka kuwaona wageni hao. Kwanza alifikiri kuwa macho yake yalikuwa yakimchezea shere. Punde si punde kofi la fahamu lilimpiga. Akajuwa fika kuwa yupo hatarini. Kwa haraka, alimchukua Asad na kumbeba huku akitabasamu na kusema,
“ Mwanangu kipenzi changu, karibu nyumbani. “
Polisi alimtazama Bi Halima kwa macho makavu na kumwambia kuwa hawana wakati wa kupoteza. Alitoa pingu mfukoni na kuchukua mikono ya Bi Halima na kumfunga. Akamweleza kuwa amekamatwa kwa mashtaka ya kumtesa mtoto wa mume wake kando na kumnyima haki zake nyingi. Bi Halima alianza kulia na kulalamika kuwa yote anayoshtakiwa ni ya maneno ya urongo.
Waliandamana hadi kituo cha polisi na Bi Halima kutiwa mbaroni huku akisubiri siku ya kusikizwa kwa kesi yake. Abu yake Asad alipigiwa simu na kuelezwa kinagaubaga yote yaliyokuwa yakitokea ndani ya nyumba yake pasi na yeye kuyafahamu. Hivyo basi ,alifunga safari ya kurudi Mombasa . Hayawi hayawi huwa, siku ya kusikizwa kesi iliwadia. Bi Halima alishindwa kujitetea na kuamuriwa kifungo cha miaka ishirini kwenye gereza la Shimo La Tewa kijijini Shanzu. Machozi ya majuto yalimchuruzika chururu njia nne nne. Alitamani mauti yaje yamuokoe lakini ndo! Aliishia laitani. Ama kweli, majuto ni mjukuu. Asad alifurahi kama mvuvi aliyekinasa kishazi cha samaki kwani alijuwa kwa hakika kuwa ndio ulikuwa mwisho wa mateso yake. Yeye pamoja na ndugu zake wadogo wakachukuliwa na shagazi yao. Shangazi huyo aliwalea wote kwa upendo na bila kubagua.
Tangu siku hiyo ndugu hawa walieza kujumuika bila ya vizuizi vyovyote. Shuleni nako, Asad alisoma kwa Amani na furaha. Alizidi kujitahidi ima fa ima kwani bidii huzaa matunda. Hatimaye, alifuzu mtihani wa darasa la nane na hata pia shule ya upili. Aliibuka kijana wa kwanza mkoani pwani. Walisema, chanda chema huvikwa pete na mcheza kwao hutuzwa. Asad alipata mfadhili wa kumsomesha chuo kikuu. Aliamuru kusomea shahada ya Uhandisi. Hakulegeza kamba abadani, kwani baada ya hapo alifanya shahada ya uzamili. Akabarikiwa kupata kazi ya cheo kikubwa nchini Kenya. Waama, maisha ni fursa, itumie.
Labek! Vitanga vya mkono hunawishana. Asad hakutaka kamwe mafanikio yake yasalie kuwa yake tu. Alijenga jumba la mayatima ,ambapo ilikuwa ikikusanya watoto walio mabarabarani wasiokuwa na makwao, na kuwapa mahitaji ya msingi ikiwemo kuwafaidisha na elimu. Aidha, alifungua shirika lisilo la kiserikali lenye kuhusiana na kukuza vipaji vya vijana na sanasana mayatima.
Ahaa! Hauchi hauchi, kunakucha. Baaada ya muda mrefu sana, safari ya Bi Halima korokoroni ilifikia ukingoni. Alikuwa keshakula chumvi nyingi ila wajihi wake uling’ara kwa furaha ya kuachiliwa huru. Mambo yalikuwa yamebadilika sana. Mumewe alishajipatia jiko jengine. Wanawe walikuwa wameshakuwa mabarobaro na hata wao walifanikiwa kupata shahada kwenye nyanja mbalimbali. Kwanza alimtafuta Asad na alipompata, alimuomba msamaha kwa yote aliyokuwa akimfanyia. Asad hakusita kumsamehe kwakuwa alijuwa wazi kuwa chuki ni sumu ya uhusiano. Alimlaki mamake Bi Halima kwa furaha na kumwambia kuwa wasahau yaliyopita kwani si ndwele. Wote walijumuika kwa mara nyengine tena baada ya muda mrefu na wakaishi kwa furaha hadi hatima yao.