“Why me?” Mimi! Nilikosea wapi? Je, ni wazazi wangu? Walikosea mtu kwa njia yoyote ile? Je, ni deni hawakulipa? Walimcheka kilema? Ama ni laana ya babu wa mababu wangu imemrudia kilembwe chao? Mimi! Kiumbe niliyekoseka!! Wanaoujuwa ulimwengu vizuri, niliwasikia wakisema nilitumika kama ‘kitoweo’ kwa wazazi wangu ili wapate mali. Mali! Mali gani? Zaidi ya maduka mawili waliokuwa nayo. Moja katika kijiji chetu na jengine katika kijiji jirani cha Watia ndani. Ama kwasababu maduka mawili hayo ndiyo yaliyokuwa maduka makubwa zaidi kuliko machache yaliyokuwepo kwenye vitongoji viwili hivi. Mali gani? Mifugo? Mifugo waliokuwa nayo, ng’ombe, mbuzi na kondoo waliokondeana kwa ukosefu wa chakula chakutosha kutokana na ukame uliokithiri. Bado utajiri huu haujaridhisha kupelekea mtu kumtoa mwanawe kafara. Ni nini haswaa? Nilitoka wakati haujafika? Mhhh mama angeniambia. Maswali hayakuwahi niishia kichwani. Nilipokuwa na umri mdogo, wazazi wangu walijaribu kila namna ya matibabu angalau mtoto wao awe sawa kama watoto wengine. Juhudi zao hazikufua dafu. Maumbile hayabadiliki, Labda kubadilisha mwendo tu!
Shule karibu iliyokuwa kijijini mwetu ni shule ya msingi ya Wanastigima. Haikuwa mahali pangu. Wanafunzi walinicheka, walinikejeli na kunikebehi, hawakuniona kitu. Walinichukulia kama kiumbe wa ajabu aliyetoka katika ulimwengu usiojulikana. Miaka ilivyozidi kwenda, nao walimu walijiunga na chama cha Wanafunzi ili kuzidi kuziumiza hisia zangu. Hisia ambazo wengi walidhani sikuwa nazo. Siwalaumu! Mumbile yangu hayakubadilika kama ilivyotarajiwa. Nilipofika darasa la sita, nilikataa kwenda shule. Tangu darasa la nne nilijipata narudia darasa mara mbili mbili. Nilikua dutu, sishiki. Hivyo ndivyo walimu walivyowaeleza wazazi wangu, sababu waliyoiambatanisha na maumbile yangu. Nilijaribu kujieleza lakini wazazi wangu hawakunielewa, Angalau mama kidogo, naye pia alijipata akiambiwa yuanidekeza sana kupelekea kufeli kwangu. Baba alikuwa akinibeba kwa baisikeli yake iliyozeeka zaidi ya jumba la historia la Fort Jesus.
Vivyo hivyo, Mzee tajiri, walivyomuita babangu, aliienzi baiskeli yake. Kubebwa kwa baisikeli ilikuwa lazima! kila asubuhi. Sasa alikuwa akinibeba na kunipeleka shule iliyokuwa nyuma ya nyumba yetu, umbali wa dakika tatu. Bidii hii yote alikuwa lazima ahakikishe amenifanikisha na kuniingiza ndani ya lango la shule. Hii ilitokana na sababu ya mtoto wake, mimi kutofika shule. Nilikuwa nikijificha katikati ya shamba letu la mihogo lililo ubavuni mwa nyumba yetu. Walimu waligundua utoro wangu na kwa haraka wakaripoti kwa mzee Tajiri. Nilishangaa mbona walijisumbua, nilidhani inglikuwa afadhali kwao kutokuwa na kiumbe cha ajabu kama mwanafunzi. Ama walitaka waonekanwe wanajali mbele ya Mzee Tajiri? Kwa mpango gani? Ili waweze kukopesha zaidi ya walivyozowea na wasiulizwe kuhusu kulipa deni lao.
Mzee Tajiri alifuatilia suala hilo kwa haraka. Kama wanavyosema,sikio la kufa haliskii dawa. Nilianza mtindo mpya! Kujificha chooni. Nilivumilia harufu iliyokuWa huko. Baada ya siku kadhaa, mikojo ya dadake mkubwa Yalinukia asmini kwenye pua Yangu. Niliipenda, ilikuwa rafiki, rafiki kipenzi wa dhati. Afadhali choo na vilivyondani yake havikuniangalia kwa jicho lakuogopa ama kunicheka, wala ile mbaya ya kunihurumia haikuthubutu. Tulielewana zaidi kutokana na majaaliwa yetu ya kutengwa na viumbe. Lahasha! Choo kina afadhali. ‘Wasiojielewa’ hufurahia starehe ya kufanya tendo la siri litokealo misalani. Maskini mimi! Baada ya majuma mawili, mamangu alinitetea kwa Mzee Tajiri. Walikuja kupata ufahamu wa usuhuba wangu na mpenzi choo. Mamangu, mwanamke mmoja kati ya wanawake wawili wanaonipenda na kunijali licha ya ulema wangu, alinihurumia na kunitetea angalau nitolewe nipelekwe shule ambayo ingekuWa na mazingira yakunifaa.
“Leo ndio umekubali? Ni kitu gani ambacho kilikufanya umkatae mwanao kilema tangu kitambo…” kabla aendelee mama alimkatiza
“Babake Matokeo tafadhali mume wangu punguza sauti, Matokeo atakuskia….” “Kuna shida akiskia? Miaka kumi na nane aliyonayo bado haelewi yeye ni kilema? Umesahau…” Mama alimkatiza tena
“Mume…”
“Uuus…”
Machozi yalikuwa yameanza kunitiririka tiriri njia mbilimbili, nilikuwa nimejificha nyuma ya mlango wa chumba chao.
“kimyaaa! Leo umejuwa kuninyamazisha? Umesahau vile ulivyonikaripia siku nilipotaka kumpeleka Matokeo katika shule ya ‘Dull Mental School’ Umesahau nakuuliza? Ukosefu wako wa elimu ndio ulikufanya uzae mtoto wa aina hii, wajuwa huyu mtoto matatizo aliyoniletea!? Nachekwa na wenzangu, nimekosa kiti cha Mzee wa mtaa sababu watu wananiogopa, yote yameletwa na huyu mtoto, kwanza nikuulize? Huyu mtoto ni wangu kweli…”
Nguvu zilipotea, sikutaka kukatika maini zaidi sababu ya maneno ya Mzee Tajiri, babangu! Nilikimbia sikujuwa wapi naelekea. Babangu? Kweli? Baba yuaweza kusema maneno makali zaidi ya kisu kipya kilichonolewa namna ile kuhusu mwanawe aliyemzaa? Ama sikuwa mtoto wake kweli? Kwani mamangu ndiye alieniumba? Mbona amlaumu yeye. Kwani mtoto hutokana na mama pekee? Mbona asitumie hiyo elimu anayoijali zaidi kuniumba tena niwe sawa? Nirudi sawa kuwa na rangi ya kawaida kama binadamu wengine? Mbona asiitumie hiyo elimu akanieka na urefu sawIA na mtoto wa umri wangu? Vicheko vya wanafunzi wenzangu. Kutengwa na walimu. Kiumbe wa ajabu wanavyoniita. Kutumika kama kitisho kwa watoto walio wasumbufu. “Hutaki kula? Ngoja nimuite yule Zeruzeru kifupi”. Yote hayo hayakuwa na uchungu tena. Maneno ya babangu yalinikata maini, moyo na viungo vyote viliniuma zaidi. Kati ya watu wote. Yeye pia. Loh! Mungu nichukuwe, sina tena umuhimu.
Mama zeruzeru kifupi, walivyomuita mamangu, alisimama na mimi, kufa kupona. Hakuvunjika moyo wala kuchoka na mmi wala kujutia kuzaa mwana mfano wangu. Mbali na talaka tatu alizozipata siku ile. Je, nikueleze vile mama huyu alipata shida kuanza maisha upya, mitihani na majanga aliyopitia, kutokuWa na ndugu wakumsaidia, kuachwa na kufukuzwa na mume, tegemeo na nguzo pekee aliyokuWa nayo maishani. Vibarau vya kufua, kuchota maji na kulima? Hatutomaliza leo.
Miaka kumi sasa imepita, siamini nimefika hapa. Shukran za dhati kwa mama yangu mlezi. Bidii za mama na mwanawe Zeruzeru, walimpeleka Zeruzeru kifupi shule ya vilema. Mahali pekee pangenisaidia. Huko maisha yalikuwa rahisi kidogo. Kutokana na juhudi zangu za masomo na bahati ya akili ya kushika masomo haraka, jambo ambalo walimu wa shule ya msingi ya Stigima hawakuliona. Nilimaliza shule ya msingi baada ya miaka miwili. Kumbukuku za tabasam alilo onyesha mamangu kipenzi baada ya matokeo bado hazijakufa.
Shule ya Upili ilikuwa na afadhali, kutokana na watu kutoka sehemu mbalimbali, sikuonekana wa ajabu sana. Misukosuko kidogo kawaida haikosekani. Kutofikia ubao pindi nlipotaka kuonyesha mfano ama kujibu swali mwalimu aliuliza. Kutofikia dawatini kwa kuekewa chakula. Kutokana na umri wangu, miaka 21, kidato cha kwanza! Loh! Wengi walishangaa baada ya kujua hilo. Mwili wangu mdogo ulisaidia. Wengine hawakuamini, labda uzee wa mamangu ulimfanya asikumbuke mwaka niliozaliwa. ‘Last born’ waliniita, nilikuwa mfupi kulikoni wote. Hili halikubadilika mpaka kumaliza kwangu kidato cha nne. Maisha niliyazoea, vicheko na kejeli havikuniumiza sana tena. Huko waliniita Albino.
Nilipojiunga na chuo kikuu, hapo ndipo mengi niliyafahamu. Mbali na mitihani midogo. Labda, babangu na ukoo wake, wanakijiji wa Stigima wangeletwa Hapa kwa jumLa wangetaalamika nakujuwa, Albino, mrefu ama mlingoti, kipofu, bubu, mfupi kama nyundo wote binadamu. Binadamu wanaostahili mapenzi, utunzi, elimu na mengineyo mengi kama binadamu wengine. ‘Special Education’ ndiyo niliyojitomoa kusomea. Matatizo yote niliyoyapitia nilitaka kuhakikisha nilitengeza mazingira mazuri kwa wote wale wanaonekanwa kama kasoro katika jamii.
Maridhia, mke wangu mtarajiwa; nguzo yangu ya pili baada ya mama. Mfano bora wa wote. Hakuna atakaye tokea kama yeye. Mwanamke aliyewakata kauli wote waliouliza nani atakubali kuolewa na mume mfupi, Albino anaelazimika kutembea na miwani meusi na chepeo ya kuziba jua kama mimi. Nilisahau sababu ya kumbukumbu zote hizi, swahiba aliyekuwa pembeni mwangu aliendelea na maswali, “Na je utamridhisha vipi Maridhia kama mume? Una uhakika hatatafuta starehe nje ya ndoa?”