Nina zito la moyoni, laniumiza akili
Nalitema hadharani, basi tulieni tuli
Liwangie akilini, hasa nyie marijali
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani
Kwa kweli nasikitika, kuona yanayojiri
Mke apewa talaka, kisa hapiki vizuri
Sio sheria hakika, tumuogope qahari
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani
Na wengine wanapigwa, Kwa kuchelewa kupika
mume matusi atowa, kwa hasira na hamaka
Wanaume sio sawa, hata kwa mola rabuka
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani
Ni nani aliyesema, jikoni pa mwanamke
Tusipotoshane jama, hizo fikira tuzike
Mie leo nasimama, nasema na nisikike
mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani
Mume jikoni kungia, pia kuzikuna nazi
Tena akampikia, mke wake laazizi
Si ajabu nisikia, huyaongeza mapenzi
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani
Wasema unampenda, mke wako laazizi
Wala huezi jipinda, kumsaidia kazi
Jamani mke si punda, basi hilo tumaizi
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani
Ila mwanamke pia, basi usifure kichwa
uwe utajilalia, usiku mchana kutwa
Kuwa makini sikia, sije mumeo kavutwa
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani
Jibidiishe kupika, na usafi wa nyumbani
Nyumba itanawirika, furaha ‘tajaa ndani
Mume ‘tarudi haraka, kutoka kwake kazini
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani
Na pia kwa mola wako, ajra utaipata
Kumtwii mume wako, bila ya wewe kusita
‘tanawiri ndoa yako, utaviepuka vita
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani