Shangwe na vigelele vilisikika kwa mbali, muda ulikuwa umetimia. Wageni walijazika furi furi nyumbani na wanawake walikua wamenitayarisha kweli! Nilikua nimepodolewa, nywele zikanyooshwa na veli nikavishwa. Hakika, nilikuwa nafunga ndoa na kijana niliyempenda kwa dhati, Mlachote.
Baada ya miezi miwili ya ndoa, tulikuwa tunaishi katika boma letu na maisha yalikua mazuri ila ya furaha ya uzazi. Kila ijapo mwezi mpya, mavya na shemeji walikuwa mlangoni kunijulia hali ya ujauzito.Ilikua kama kusugua chumvi katika jeraha, isitoshe walimsihi Mlachote afunge ndoa la pili ili aweze kupata mrithi. Haya yalisababisha vita na matusi tele.
Kama hayo hayakutosha, alizidi kunipiga mangumi na mateke kila alipokuja nyumbani.Pombe ilianza kuwa desturi na kijana niliyempenda alibadilika. Baadhi za siku hakuonekana, na alipokuja nyumbani, alirudi na wanawake tofauti. Nilianza kumchukia! Moyo ulinichafuka! “Hali ya uzazi haimo mikononi mwangu!” Nilimwambia kwa ukali na kwa machozi. Alizunguka na kunizaba kofi nikaanguka.Lilikua jukumu langu kumlisha na kumfurahisha Mlachote kwani bado alikua bwanangu na bado nilikua katika ndoa. Nilijaribu kila mbinu!
Siku chache zilipita na nilihisi unyonge na maumivu katika mwili. Yawezekana nina mimba??? Kisunzi hakikuisha na kichwa kilinigonga. Nilipoamka kutoka kitandani, nilianguka na kupoteza fahamu.Sijui kilichofanyika. Nilipoamka nilijikuta kitandani na mwanamume nisiyemjua! “Ala! Nani wewe??” niligutuka na kutaka kukimbia lakini nilivutwa kwa nyuma na kuzabwa makofi. “Mwanamke mwovu na mpumbavu! Unazo shida tele na unalala na wanaume usiowajua! Isitoshe, kitandani mwangu na ndani ya boma langu?!” mvua ya makofi, mateke na mangumi hayakuisha.
“Mwanahamisi! Mwanahamisi! Mbona watoka damu? Mbona umejitanda leso? Nguo ziwapi? Mlachote yuwapi? Babake!!! Njoo uone mwanao! Mwanahamisi!?” mamangu alinigutusha kutoka fikra zangu na nilimkumbatia na kulia kilio nilichokificha ndani ya roho kwa miaka hiyo yote…