Hapo kale, kulikuwa na bwana mmoja na mke wake pamoja na binti yao aliyekuwa mrembo sana. Urembo wake uliwafanya wanaume wengi wakose usingizi na matokeo yake wakajitokeza kuleta posa ili wawe wachumba wa binti yule. Bwana yule hakufanya neno, alizipokea posa saba zilizoletwa ilhali bintiye alikuwa mmoja tu. Kwa sababu ya ugumu wa maisha, alikula pesa zile bila kujali atawaambia nini wachumba wale watakapokuja kudai wake zao.
Siku zilisonga na hatimae awamu ya harusi aliopangana nao ikakaribia na amani ikamtoroka katika mtima wake. Akaamua kumuendea mganga mmoja ili amsaidie kutatua mkasa ule. Bwana mganga akamwambia asijali kwani yeye angemsaidia kumvusha katika janga lile. Akamuagiza alete mifupa ya viumbe sita kando na binadamu pamoja na mwanawe mpendwa. Alifanya kama alivyoagizwa na mganga na akakusanya mifupa ya paka, kuku, mbuzi, tumbili, mbwa na panya. Alimchukua binti yake na kuelekea nae kwa mganga. Mganga alipopokea vitu vile akamuomba kuviacha pale pamoja na binti yake mpendwa na kumtaka arudi siku itakayofuata.
Kulipokucha bwana yule akadamkia kwa mganga akiwa na matumaini makuu. Alipowasili kule aliambiwa afungue chumba kimojawapo katika vyumba vya pale kwa mganga na alipofanya hivyo hakuamini macho yake, kwani ndani ya chumba kile aliwaona wasichana saba wenye sura moja, yaani sura ya bintiye. Kwa jinsi walivyofanana kama shilingi kwa ya pili, alishindwa kumfahamu binti yake. Ilibidi amuulize mganga.
“Bwana mganga nina swali. Ni vipi nitaweza kumjua mwanangu kati ya hawa waschana?” “Hilo lisikusumbue,” alimjibu. “Mwanayo ni mwanayo, hutashindwa kumjua.” Alifurahi baada ya kusikia vile na akawa ni mwenye kuridhika. Aliwaongoza hadi kwake na siku ya pili akawajuza wachumba siku za kuja kuoa ili siri yao kuhusu mabanati wale ihifadhike. Wakaja mmoja baada ya mwengine kila mtu kwa siku yake hadi wasichana walipokwisha kuolewa. Katika kizaazaa kile cha maharusi yaliyofuatana, wazazi wale hawakujua bwana aliyemuoa binti yao ni yupi hivyo basi kubakia na mashaka baada ya maharusi kuondoka.
Baada ya miezi michache, wazazi wale walipatwa na hamu ya kumjua binti yao alipo na hapo wakafunga safari kiguu na njia kwenda kwa wakwe zao mmoja mmoja. Wakatokea kwa mkwe wao wa kwanza na kuwakuta pamoja na mkewe. Waliulizana hali za muda kisha wakataka kujua kama yule ndiye binti yao hivyo wakamsaili.
“Vipi baba, waendeleaje na mkeo?”
“Salama, hatuna neno ila huyu mwenzangu ananishangaza. Mimi kipato changu alhamdulillah, vitoweo hasa samaki havikosekani ndani ya nyumba ila huyu mwenzangu kila tukimaliza kula hutoka nje na kwenda kula miba ya samaki tuliyotupa jaani. Kwa kweli nashindwa kuelewa shida iko wapi.” Wazazi wale wakaaangaliana na baba akamwambia mkewe kwa sauti ya chini,
“Huyu aonesha ametokana na mifupa ya paka. Twende zetu mke wangu tukamtafute mwanetu.”
Kisha akaongeza sauti na kumwambia mkwe wao,
“Mvumilie, ndo tabia zake.” Wakashika njia na kuelekea kwengine.
Wakafika kwa mkwe wao wa pili na baada ya maamkizi wakamuuliza anaendelea vipi na mkewe.
“Naam, baba, vipi habari za hapa na mkeo anaendeleaje?” Alianza bamkwe.
“Hatuna neno ila huyu mwenzangu ananishangaza,” yule mkwe akajibu. “Tunaweza kukaa kibarazani kwa ajili ya kupunga upepo mara nikamuona mwenzangu ameanza kuparaga miti. Sijui hasa tatizo nini.” Wazazi wale wakaangaliana kisha babe mtu akamnong’oneza mkewe,
“Huyu nae aonesha ni tumbili, siye mwanetu. Twende zetu wala tusirudi tena hapa”. Kisha akaongeza sauti na kumwambia mkwewe, “ndivyo alivyo, mvumulie tu.” Wakashika njia na kuelekea kwa mkwe wao mwengine.
Walifika kwa mkwe wa tatu na baada ya kubadilishana salamu baba yule akaulizaswali lile lile,
“Munaendeleaje na mkeo hapa?” Mkwe akajibu, “Hatuna neno lakini namshangaa sana huyu mwenzangu. Tutakula hapa shibe yetu, ila cha kunishangaza baada ya kula mwenzangu hutoka nje na kuanza kutafuna nyasi! Nikimuuliza hanipi jibu la kueleweka.” Wazazi wakaangaliana na kisha baba kumwambia mkewe kwa sauti ya chini, “huyu atakuwa ni mbuzi. Twende zetu mke wangu tukamtafute mwanetu.” Kisha akamgeukia mkwewe na kumwambia amvumilie tu kwani ndo tabia yake. Wakaaga na kuondoka.
Wakaelekea kwa mkwe wao wa nne na walipotokea tu uwanjani mke akawaona na kuwakimbilia huku akiita, “Mama! Baba! Karibuni sana kwangu. Nimefurahi kuwaona wazazi wangu!” Hapo wazazi wale wakajua wamefika kwa mwana wao halisi na hawakuwa na haja ya kumaliza safari ile.
Sasa, mabinti wote saba walijaliwa kupata watoto na watu wakaongezeka. Kwa muonekano walikuwa watu ila kwa tabia walitofautiana. Watoto waliotokana na wale mabinti sita waliokuwa ni wanyama awali walikuwa na tabia zisizoeleweka lakini watoto waliotokana na yule binti halisi walikuwa na utu na tabia za kuvutia.
Hivyo basi, katika dunia hii wengi ni binadamu na wachache ni watu.