Machozi yalinitiririka na kulowesha kanga niliyokuwa nimejitanda. Damu nayo ilichurizika ndani ya moyo wangu uliovunjwa vipande vipande. Nilikitizama kioo mbele yangu na kovu zilizojaa usoni mwangu zilinizidishia uchungu maradufu. Naam, kovu niliziozipata kwa kupigwa kama punda kila siku iliyoitwa siku. Nilivitizama vitu tofauti tofauti vilivyokuwa juu ya meza yangu ya kuekea vipodozi. Si udi, si fitna, si marashi aina tofauti, si mafuta mazito, si mafuta ya kikuba, si mafuta ya asumini si mekapu. Vitu hivi vyote nilipewa punde tu baada ya kuolewa na kufundwa kuwa ni vitu ninavyopaswa kuvitumia kama mke ili kumfurahisha mume. Hata hivyo, vitu hivyo vyote nilikuwa nimevitumia kwa uchache sana. Furaha, amani na hamu iko wapi ya kujipamba? Na huyo mtu wa kupambiwa anaelewa, kuona au kufurahia kupambiwa huko?
Nilitoka chumbani mwangu na kwenda chumba cha watoto wangu wawili. Pengine sasa wangekuwa hata wanne lau ingekuwa si kupigwa hadi kuharibu ujauzito zaidi ya mara moja. Niliwatizama wanangu wakiwa wamelala lakini bado sura wamezikunja. Hakukuwa na ishara yoyote ya furaha kwenye nyuso zao hata walipokuwa usingizini. Sauti zao za kuhurumisha zilizojaa vilio na simanzi ndani yake zilinjia akilini, “baba muache mama! Usimpige! Baba tafadhali……” Fikra hizo zilipenyeza ndani ya moyo wangu na kuukata kata zaidi. Nilishindwa kabisa kustahmili kubaki chumbani humo na kutoka huku mkono nimeuweka kinywani kwa uchungu. Naam, pengine mimi ningeweza kuhimili uchungu lakini je wanangu? Watoto wadogo waliokuwa bado hata hawajaielewa dunia kinaga naga. Watoto waliotakiwa kuufurahia utoto wao kwa hali zote. Watoto! Watoto wasiokuwa na hatia wala wasiolewa chochote.
Nilienda kuketi sebuleni huku mawazo yakiendelea kucheza densi kwenye kichwa changu. Kichwa kilichogeuka na kuwa kasha la mawazo kwani nilikuwa mtu wa kuwaza laili wa mahari. Niliwaza hili na kuwazua lile. Niliiwaza siku ambayo wazazi wa Mbati, mume wangu walivyokuja kwetu na kutaka niolewe na mwanao. Naam ilikuwa familia iliokuwa na pesa kama njugu na kutokana na hilo, familia yangu haikuona haja kuichunguza zaidi wala kumchunguza Mbati. Waliona hapa mwana wetu ameangukia bahati. Nilijaribu sana kuwashauri wazazi wangu wamchunguze Mbati lakini juhudi zangu ziliambulia patupu.
“Acha ujinga na kisirani Subira! Hebu olewa na sisi angaa tutoke kwenye huu umasikini uliotugandama kama kupe.”
Mama yangu alinifokea kila nilipojaribu kumwambia kuhusu kumchunguza mume. Hatimaye nilikata tamaa na kuamua liwalo na liwe. Posa ililetwa, mahari malaki kwa malaki yalitolewa, dhahabu nilizawadiwa na harusi ya kukata na shoka kufanywa. Siku ya kuongolewa niliimbiwa mashairi kwa mahadhi ya kuvutia huku kukipigwa matwari na mambuji katika fani hiyo. Naam, mashairi yaliyoburudisha lakini zaidi yaliyobeba ujumbe mzito. Ujumbe ambao ulibaki kuwa kitendawili kigumu katika maisha yangu ya ndoa.
‘wanawake hoyahe hoyahe na ulie mshindo mmoya mmoya.
Bibi harusi sikia,
Haya tunayokwambia,
Ndoani ukiingia,
Subira ishike vyema.
Mume kumvumilia
Hiyo ndiyo sawa ndia
Isiwe utakimbia
Ukarudi kwake mama.’
Sio shairi hili tu lililoniachia kitendawili kigumu bali pia mawaidha niliopewa kama bibiharusi.
“Mwanangu ndoa ina misuko suko chungu nzima. Hivyo basi ni muhimu uwe na subira kwa kila jambo. Mumeo mpende, muheshimu na umtimizie kila analolitaka. Daima uwe chini anapokuwa juu na uwe mwenye kunyenyekea.” Mama yangu aliniambia.
“Ndiyo! Isiwe la kwanza la pili usharudi nyumbani kushtaki. Ndoa ni uvumilivu. Usione watu wameishi miaka thelathini ukadhani ni raha tupu wanazozipata. Ishikilie ndoa yako usije ukaachwa ukatuletea fedheha.” Aliongezea halati Chochea.
Haya yote yalinichanganya si haba. Je huku kuvumilia kuna mipaka? Au ndani ya ndoa mtu huvumilia lolote tu? Mtu huvumilia hata mauti yanapomkodolea macho? Hivi ni hatia kutoka kwenye ndoa yenye misuko suko ya kuvuka mipaka? Aaah! Ni aibu! Ndiyo ni aibu kuachwa. Ndivyo mama na halati wanavyosema. Ndivyo jamii inavyochukulia. Lakini kati ya aibu na mauti lipi hatari?
“Subira! We mwanamke!”
Ghafla nilizinduliwa kutoka katika bahari ya luja na sauti ya Mbati.
” Abee mume wangu. Karibu na pole sana na kazi. Samahani nilikuwa kwenye mawazo mazito, sikusikia ukiingia.” Nilimwambia mume wangu huku nikimpokea mfuko aliokuwa amebeba.
“Mawazo gani hayo? Kwani huli au hunywi humu ndani? Unaishi kwenye kasri na kila utakacho unapata. Sasa mawazo ya nini? Unavyovipata humu ulivipata ukiwa kwenu kwenye nyumba ya makuti?” Alijibu Mbati kwa sauti ya kejeli na ndweo na kumalizia kwa kicheko ambacho kilinikera kila alipokicheka.
Nilimeza mate machungu na kujikaza nisimjibu ili kuepusha majibizano na rabsha. Nilifunua kawa lililoandikwa ‘mkeo ni yai, mtunze umrai rai’ lililokuwa limefunikiwa samaki wa kupaka. Nililisoma kawa hilo nikatabasamu na kutikisa kichwa kisha nikafunua kawa lingine lililofunikiwa mikate ya mofa na kumpakulia mume wangu. Nikachukua buli la chai na kumtilia chai kwenye kikombe chake.
“Pthuuuuu! We mwanamke una akili? Unataka kuniua? Mbona pilipili nyingi kwenye samaki eh?” Alifoka Mbati kwa ghamidha huku amenikodolea macho nusura kunimeza na kutema chakula kilichokuwa mdomoni.
“Lakini mume wangu si unapenda pilipili?”
“Ndiyo napenda lakini hii ya leo imepitiliza.”
“Mbona nimeweka kiwango ninachoweka kila siku tu.”
“Ninapoongea usinijibu.” Alinifokea kwa ghadhabu na ghafla kofi liliniangukia usoni.
“Haya ni maisha gani mbati? Mbona umenigeuza ngoma? Hakuna siku ndani ya nyumba hii tutaishi kwa amani? Hivi ulinioa uje uninyanyase?” Nilimwambia huku nikilia kwa uchungu.
“Unajua kunyanyaswa wewe? Alafu umepata wapi jeuri ya kunijibu? Sasa hii ndio adabu yako.”
Alichukua buli la chai na kunirushia. Nilijaribu kukwepa lakini chai ilinifikia kwenye mkono mmoja na kunichoma vibaya sana. Nilipata maumivu makali lakini wala moyo wake haukumtweta. Ukakatima ulikuwa umemvaa vilivyo mwanamume huyu ambaye alikuwa hana hata sifa moja ya kuitwa rijali. Nililia kwa uchungu na kunyerereka kuelekea chumbani nikamwacha Mbati akiendelea kula kana kwamba hakuna kilichotokea.
Niliketi kitandani na kujaribu kulia kimya kimya lakini hatimaye sauti ilitoka bila kutaka. Nilijikuta napiga mayowe kama mwendawazimu. Maumivu ya kuchomeka na maumivu ya moyoni yalichanganyika na kunipeleka katika ulimwengu tofauti. Nilikumbuka mawaidha niliokaririwa kuhusu uvumilivu na maswali chungu nzima yakanirudia akilini. ‘Hivi huu uvumilivu ni kwa kila jambo? Vipi kuhusu mambo mazito yasiobebeka au yanayoweza kuvunja mabega, nayo pia huvumiliwa? Hapana! Mengine hayavumiliki na hili tukio la leo ni miongoni mwayo.’ Nilishauriana na moyo na kuamua kuwa siku iliofuata nitafunga virago nirudi kwetu. “Nina kwetu, hakunitoa mtini ebo!” Nilijiliwaza.
Nilienda chumbani kwa wanangu kuwatizama na kuwakuta wamezama kwenye usingizi. Nilishukuru kuwa hawakusikia mgogoro uliokuwa ukiendelea. Hata hivyo, migogoro mingi ya nyuma waliyashuhudia na kupelekea kuathirika kisaikolojia. Mapenzi yao kwa baba yao yalianza kuyeyuka pole pole hapo awali na hatimaye kutokomea kabisa. Kila walipomuona walikimbia chumbani mwao au kujikunja kipembeni na kunywea kama waliopigwa na baridi. Nilisikitika kuona kuwa licha ya kuwa na baba hawakuuhisi uwepo na mapenzi yake.
Asubuhi iliofuata, nilimsubiri Mbati aende kazini nami nikaangata virago vyangu na kuwachukua wanangu tukaelekea kwa mama. Nilimkuta mama akiwa katika pilka pilka zake za biashara ya mahamri na mbaazi. Nilimsalimia na kisha kwenda moja kwa moja hadi ndani. Aliniangalia kwa jicho la maswali lakini hakuweza kuniambia chochote kutokana na wateja wengi waliokuwa wamemzunguka. Punde tu baada ya mama kumaliza biashara yake alikuja ndani hata kabla ya kuondosha ondosha vyombo.
“Enhe kumezuka?” Alinuliza huku akichukua kigoda na kuketi.
“Mama nimevumilia mengi ila nimechoka mwanao.” Nilijibu huku machozi yakintiririka.
“Mkono umefanyaje tena?”
“A….me….ni…..chomaaa.”
“Aka! Amefikia huko? Na makovu yote usoni ni ya nini?”
“Mama napitia mengi kwenye ndoa ile. Mengi makubwa na mazito lakini niliamua kunyamaza tu ila hapa nilipofikia nimechoka.”
Mama aliketi vizuri, akaitengeza kanga aliokuwa amejitanda na nikajua sasa ni wakati wa kuimbiwa ile nyimbo ya kila siku, nyimbo ya subira na naam wala sikukosea. Mama alianza kunipa mawaidha ya kusubiri.
“Ndoa ni kuvumilia mwanangu! Subiri tu yatakwisha. “
“Mama lakini nitasubiri hadi lini? Huoni kama huyu mwanamume anaweza kuniua?” Nilimjibu mama kwa uchungu.
“Kwani waanza wewe kuolewa? Mbona wengine waliolewa hawajakufa? Umepata mume mwenye pesa unaanza kuleta kisirani. Subiri angalau na mimi mamako nisikose kupata hivo vizawadi zawadi vya kanga na madera kutoka kwa huyo mkwe. Umesahau pia kuwa mkwe ameahidi kunijengea nyumba? Subiri pia wanao wapate maisha ya kifahari na kusoma shule ya ghali. Au unataka uachwe uje kuishi kwenye hiki kijumba cha makuti uuze mahamri? Unataka wanao waje wabeheneke hapa mtaani?.”
Ghafla halati Chochea aliingia.
“Enhe nana! Umekuja kuamkua au kuleta mashtaka?” Alisema halati Chochea kwa stihazai zake alizozoea kunifanyia.
Nilishangazwa sana na tabia ya mama na halati. Nilishangazwa ni jinsi gani walivyokuwa hawaijali furaha yangu wala afya yangu. Kikuu walichojali ni pesa na ufahari. Walitaka wajifahirishe mtaani kuwa mtoto wao ameolewa na mume tajiri na amedumu kwenye ndoa. Aidha walizifurahikia sana pesa na zawadi zawadi walizokuwa wakipelekewa na Mbati. Naam, waliyajali maslahi yao kuliko walivyoijali furaha yangu.
Niliinuka na kuelekea chumbani huku damu moyoni ikizidi kuturuzika. Nyumbani nilikokutumainia kuwa ningepata faraja na amani kumezidi kunipa maumivu. Ni wapi nitakimbilia? Ni wapi nitakwenda nipate mtu wa kunisikiliza? Ni wapi nitakapopata ushauri wa kunifariji? Nilisimama dirishani na kuwatizama wanangu wakicheza bila kufahamu kilichokuwa kikendelea wakati huo. Moyo ulipata furaha kidogo kuwaona angalau walipata kucheza kwa furaha. Walifurahikia zaidi walipokuwa nyumbani kwa mama hata kuliko walipokuwa nyumbani kwa baba yao. Wanangu pekee ndio waliokuwa faraja yangu. Walikuwa na mimi katika kila hali. Walinihurumia na kunifuta machozi na viganja vyao vidogo. Walinipga pambaja lililonipa furaha na faraja kila nilipokuwa na majonzi. Naam, licha ya umri wao mdogo waliweza kuniambia maneno ya kunitia nguvu na ujasiri. Ghafla mawazo ya mbati yalinijia. Nilimkumbuka yule Mbati nilyeingia kwenye penzi nzito naye mwanzo mwanzo wa ndoa yetu. Nilimpenda kutoka katika kila kipembe cha moyo yangu. Nilimjali na kujaribu kadri niwezavyo kumuweka furahani. Naye alinionyesha mapenzi na kunipeleka katika ulimwengu tofauti. Ulimwengu wetu peke yetu. Ulimwengu wa mapenzi. Hata hivyo, hayo yote yalidumu kwa muda mchache mno. Mbati alibadilika ghafla na kuanza vitimbi. Au niseme alianza kuyatoa makucha yake na kuidhihirisha rangi yake halisi. Vitimbi na masimango yake ya kila siku yalianza kuyayeyusha mapenzi yangu pole pole na hatimaye moyo wangu uligubikwa na uoga juu yake badala ya mapenzi. Hata hivyo, kulikuwa na sehemu katika moyo wangu iliokuwa bado na mapenzi juu yake. Nilijaribu kukataa kuwa nampenda lakini kila nilipokaa mbali naye nilipata hisia juu yake. Nilihisi kuwa siwezi ishi mbali naye. Alinikamilikisha! Naam aliyakamikisha maisha yangu. Ndiyo! Licha ya manyanyaso yote bado kuna wakati aliniambia maneno mazuri nami nikajihisi kupendwa. Katika maisha yangu sikuwahi kupata mapenzi ya baba wala mwanamume yeyote yule na hivyo basi mapenzi yake japo ya dakika mbili yalinipa furaha flani ingawa haikudumu. Aliponiambia, “Nakupenda!” hata kama hakumaanisha bado iliuyeyusha moyo wangu na kunipa hisia. Nilikata shauri kuwa usiku huo nitalala kwa mama lakini siku ya pili yake nitarudi kwa Mbati wangu.
Siku ya pili nilijitayarisha na kuamua kurudi nyumbani kwangu. Nyumbani nilikoitwa mke! Mama alifurahika sana alipoyasikia maamuzi yangu. Alinipa hongera kutokana na ujasiri wangu na kuniimbia tena ngonjera yake ya subira. Aliniambia kuwa ndoa yangu ndiyo heshima yangu na lolote litakalofanyika nilivumilie. Abaadan nisiruhusu jambo lolote linitoe kwenye ndoa yangu. Nilimsikiliza vyema na kuamua kuwa safari hii nitajaribu juu chini, kwa udi na uvumba kumuonyesha mapenzi ya dhati Mbati na pengine huenda akabadilika na kunionyesha mapenzi pia. Nitajaribu kila mbinu kumdhihirishia kuwa mimi ni mke bora. Nitayavumilia yote atakayonifanyia na kusimama imara kuhakikisha kuwa ndoa inakuwa dhabiti na kunapatikana itifaki ndani yake.
Nilipofika katika mlango wa nyumba yangu nilipata kumbimbi. Niliufungua mlango huku machozi yakinitirika. ‘Subira unatakiwa kuwa jasiri. Ingia ndani ukailinde ndoa yako! Ingia ndani ukailinde nyumba yako. Ingia ndani ukazitimize haki zako kama mke!’ Nilijiambia kisha nikavaa ujasiri na kuingia ndani. Nilioyaona ndani yalinimaliza nguvu zote. Ujasiri wote niliouvaa ulinivuka. Moyo ulinienda mbio kuliko kawaida. Nilikuwa tayari kuukabili unyanyasaji wa Mbati lakini sio jambo hilo nililoliona. Hakika sikuwa tayari kabisa kulihimili hili na licha ya ukakatima wa Mbati, sikutarajia kama angefikia hatua hii. Mbati alivuka mipaka yote! Nilimkuta akiwa ameketi na mwanamke wakiwa katika hali tatanishi. Mkao waliokuwa wamekaa sio wa mtu na dada yake wala rafiki au mfanyikazi mwenza. Ulikuwa mkao dhahiri wa mtu na mpenzi wake. Nilikorogeka na kushindwa kabisa kusema au kufanya lolote katika hali ile. Nilienda moja kwa moja chumbani na kukaa kitandani. Mbati alikuja mbio na kunikuta nimeketi kitandani huku uso nimeuzika kwenye viganja nikilia.
“Alaa! U…me…rudi! Mbona hukunitaarifu ka.. ma…wa..ja?” Alisema Mbati akiwa amepata kigugumizi cha ghafla.
“Yule ni mkeo?” Niliuinua uso wangu uliobadilika mwekundu nikamuuliza Mbati.
“Ha..pa…na ila tu…na …we…za limaliza hili.”
“Hata afadhali angekuwa mkeo mimi nisingekuwa na shida na hilo. Kama unataka kuongeza mke si uongeze tu Mbati! Kwanini unionyeshe madharau kiasi hichi?”
“Samahani subira!” Aliniambia Mbati kwa upole na kwa sauti iliyodhihirisha ni kiasi gani alivyojutia kosa lake.
Aliposema hivyo tu moyo wangu uliyeyuka na hasira zote kuisha. Niliisikia sauti yake ya mapenzi baada ya muda mrefu na hilo lilinipa furaha ya ajabu. Alinishika begani na kuendelea kuomba msamaha.
“Naomba unisamehe mke wangu.”
Nilifarijika na kuhisi kwamba ndoa yangu haiko mbali na kusimama imara.
Maisha yaliendelea na Mbati aliendelea kuninyanyasa kama kawaida. Kama nilivyoyavulia nguo kuwa safari hii nitaipigania ndoa yangu basi ilinibidi kuyaoga. Kila aliponifokea nilinyamaza na alipopoa nilijaribu kuzungumza naye kwa upole. Hata hivyo, yote niliyomwambia yalionekana kuingia sikio moja na kutoka kwenye sikio lingine. Sikukata tamaa! Aliponipiga niliuvumilia uchungu na kuuguza majeraha kimya kimya. Nilijipa moyo kuwa hakuna marefu yasiokuwa na ncha. Nilizidi kuipigania ndoa yangu na kujaribu kadri niwezavyo kuwaeka wanangu mbali na matatizo yangu. Kila Mbati aliporudi nyumbani, niliwapeleka wanangu chumbani kwao ili ikiwa kutatokea rabsha wasishuhudie chochote. Nilijaribu kujiweka mwenye furaha kila nilipokuwa mbele ya wanangu. Waliponiuliza kuhusu majeraha yangu nilitafuta urongo wowote wa kuwaambia.
Siku ziligeuka na kuwa wiki nazo wiki kugeuka na kuwa miezi lakini hakukuwa na dalili ya Mbati kubadilisha mwenendo. Bidii zangu zote ziliambulia patupu na subira yangu katu haikuvuta heri. Nilianza kuchoka! Nilianza kuchoka kuuguza majeraha yaliojaa mwilini. Nilianza kuchoka kujidanganya kuwa mapenzi yangu huenda yakambadilisha mume. Nilianza kuchoka kuulazimisha moyo kuvumilia maumivu! Nilianza kuchoka kuwaza na kuwazua! Majeraha niliokuwa nayo mwilini yalianza kunidhoofisha. Aidha nilidhoofika kutokana na mawazo na pia nilikosa nguvu kutokana na kutoweza kula kwasababu ya kukosa furaha. Nilikonda na kukondeana nikawa sitamu sinyamu. Haiba na nuru kwenye wajihi ilizidi kufutika. Nilianza kujichukia! Nilichukia hata kujiangalia kwenye kioo. Nilikosa hata hamu ya kuoga, kupiga mswaki, kubadilisha nguo wala kuchana nywele. Sikuwa hata na hamu ya kupika. Kazi zote niliwaachia wafanyikazi ndani ya kasri hilo.Wanangu pia sikuwa na wakati nao tena. Sikukaa nao na kuwatolea hadithi kama hapo awali. Sikukaa na kula nao wala kuwasaidia kazi zao za shule. Walipokuja kunipiga pambaja na kunibusu kama kawaida yao niliwaangalia tu. Maisha kwangu yalikosa maana kabisa. Mume wangu aliiona hali yangu lakini alijifanya hamnazo. Hata hivyo, ilifikia wakati naye akakimwa hadi ya kukimwa na hali hiyo. Alinifokea sana na kuniita kila aina ya majina. Hisia zangu zilikuwa zimezima na sikuathirika kivyovyote na maneno yake. Nilikuwa katika ulimwengu tofauti!
Hiyo siku! Mbati aliingia nyumbani akiwa amelewa chakari. Tangu kuolewa naye hakuna hata siku moja niliomuona Mbati akiwa katika hali hiyo.
“Mwanamke gani mchafu! Mwanamke unanuka! Hivi umeteta na maji we mwanamke? Mimi nimekuchoka! Mwanamke unatisha! Sura mbaya!.” Alifoka kwa sauti ya kilevi
Mara alianza kunipiga mangumi na mateke kila sehemu. Kama haitoshi akaenda kuchukua mchi wa kinu na kunipiga nao. Nilianza kupoteza fahamu lakini nilizisikia sauti za wanangu kwa mbali.
“Mama! Mama! Baba usimuue mama! Baba muache mama!”
Alinipiga mchi wa mwisho wa kichwa na hapo nilipoteza fahamu kabisa na sikujifahamu tena.
Nilijaribu kuinua mkono lakini ulikuwa mzito. Nilijaribu kuinua mguu nao pia ulikuwa mzito.Niliyafungua macho taratibu na kumuona mama amekaa pembeni. Niliangaza macho huku na huku na hapo ndipo nikagundua nipo kwenye kitanda cha hospitali. Mguu wote ulikuwa umefungwa bendeji na mkono nao hali kadhalika. Mama aliponiona nimefungua macho alikuja mbio kuniangalia.
“Alhamdulilah mwanangu umeamka!” Alisema mama huku akinipapasa kichwa.
“Samahani mwanangu!” Aliendelea huku machozi yakimdondoka, “Samahani sana mwanangu. Mimi ndiye chanzo cha yote haya. Najuta mwanangu. Ikiwezekana nisamehe.” Machozi yalizidi kumbubujika mpaka akashindwa kuongea. Aliinuka na kwenda pembeni kisha akarudi. “Nimekuwa mama muovu sana kwako. Nimekugandisha pasipostahiki kugandwa! Naumia! Najuta! Hakika sio yote ya kuvumiliwa ndani ya ndoa. Subira ina mipaka. Ndoa ni utulivu, mapenzi na furaha. Ndoa sio manyanyaso!”
“Wanangu mama!” Nilijaribu kujitahidi kuongea.
“Usijali mwanangu, wanao wapo nyumbani kwangu na Chochea. Mbati naye amekamatwa na polisi. Ni lazima ahukumiwe kutokana na makosa yake. Ni lazima ajifunze kuwa mwanamke ni kiumbe adhwimu anayetakiwa kutukuzwa, kuheshimiwa na kujaliwa. Mke ni zawadi na tunu kwa mwanamume. Ni lazima ajifunze kuwa ndoa ni jambo muhimu katika maisha wala sio kitu cha mzaha. Ni lazima ajifunze!”