Kuna mfalme aliuawa.
Mwanawe, aliyerithi taji, alikula yamini kubaini chanzo cha vita viliv’oyaleta mauti yaliyomfarakanisha babake na kiti chake cha enzi.
Akamuita Waziri aliyekuwa tayari kuukoboa moyo wake kifuani ili upandikizwe kwenye kifua cha mfalme mahututi kisha yeye, haidhuru, awekewe pera pahala pa moyo wake. Waziri huyo aliyedhihirisha uaminifu timilifu akapewa jukumu la kwenda kudadisi kuanzia utandu hadi ukoko wa vita hiv’o viliv’oitetemesha milki yao ya Lamu. Waziri akaanza kuwatambalia na kuwanong’oneza wazee wa Amu ili apate ufumbuzi wa kiini cha vita hiv’o. Hakupata. Akaambiwa nenda Mokowe, kuna mtu mzima fulani twafikiri hiv’o vita avijua vizuri. Waziri akafunga safari, akaenda mpaka Mokowe. Akamkuta mtu mzima, hana kazi tena mbali na kwenda msikitini na kurudi nyumbani. Akamuuliza. Huyo mtu mzima akanyamaa kwa muda, kisha akamjibu kuwa yeye pia havifahamu vizuri lakini akamwambia aende eneo-jirani la Hindi kuna ndugu mkubwa wake aweza kuvifahamu vita hiv’o vizuri.
Waziri akafunga safari tena akaenda mpaka Hindi. Akamkuta mzee. Guu lake halijui nje, mwendo wake ni wa kwenda chooni na kurudi chumbani, basi! Akamuuliza habari ya vile vita. Mzee naye akamjibu kuwa pia yeye havifahamu kwa kina lakini akamtaka aende Mpeketoni kuna ndugu mkubwa wake pengine atampa taarifa zaidi. Waziri nusura afe moyo. Ule ule moyo wake mkubwa aliotaka kumtunukia mfalme kisha badili yake abandike pera kifuani. “Ah! Basi tu ni kufuata hiyo amri ya mfalme mpya lakini kama hawa hali zao ni hizi, huyo mkubwa wao ela hajafunga kauli kama hajapiswa kamwe?” Waziri alinung’unika.
Akafunga safari kuelekea Mpeketoni japo shingo upande. Alipowasili, akauliza ‘fulani’ nimemkuta? Akaashiriwa nyumba ya ‘fulani’ ni ilee. Akaenda, akabisha. Akatoka bibi kizee. Akamshikamoo na kumuulizia ‘fulani’, “Kwake si huku?” Akajibiwa, “Enh, kwake ni huku.” Waziri akamwambia, “Namtaka, nimetumwa na mfalme.” “Yuko shamba,” akajibiwa.
Waziri akaona haya ndiyo yale aliyoyahofia. Yaani afunge tena safari aende hukooo shamba, akakizuru kikongwe ambacho kimepelekwa huko pengine kisubiri mauko yake huku kikitazama kaburi lake.
“Mbona bumbuwazi?” Bikizee alihoji.
“Lo! Nafikiria bibi…nimetoka mbali…kisha niende huko shamba…” Waziri aligugumiza.
“Haa-ah ya nini uende shamba? Hii ni saa hedashara, mwenyewe hayuko mbali tena,” Bikizee alitaarifu.
Waziri alikaa tahiyatu juu ya jamvi, akiitazama njia kwa hamu.
Muda, fremu ya mtu aliyebeba tita la kuni huku ameshika fimbo ndefu ilichomoza kwa mbali.
Bikizee akatimua mbio kumfuata. Akamtua tita la kuni na kujitwika yeye kisha akamwekea mkono begani na kumuacha amuongoze njia na fimbo yake ndefu.
Wakaandamana mpaka wakafika pale nyumbani. “Mke wangu namna gani? Amekuja mgeni hata tanga(butternut) hukumkatia…” Mume alitanguliza kabla ya kumkongowea mgeni wake. Mke akaingia ndani upesi kisha akatoka na tanga. Yule mume akalifinya akamwambia, “Tanga hili bado ni gumu.” Mke akarudi ndani kwa muda kisha akatoka tena na tanga. Yule mume akalifinya kisha akamwambia, “Pia hili bado ni gumu kidogo.”
Mke akarudi tena ndani kwa muda kisha akatoka tena na tanga. Mume akalifinya kisha akamwambia, “Naam, hili tayari.”
Zamani ilikuwa huwezi kumuuliza mgeni haja yake mpaka atimize angalau siku tatu. Au kwa mgeni kama huyu aliyetumwa na mfalme, basi lazima atabaruku chakula japo kidogo kabla hajasikizwa dharura yake.
Wakakatiwa tanga wakala na mgeni.
Waziri akauliza habari za vile vita. Akaelezwa vilikuwa kadha…kadha…kadha, akapewa taarifa zote kwa vikomo na nukta.
“Haya ya mfalme tumeyamaliza, sasa ni yangu mimi na wewe…” Waziri akadokeza.
“Nimekwenda kwa ndu’ yako Mokowe, nikamdirika hali yake hwenda msikitini na kurudi nyumbani tu. Kisha nimekwenda kwa mwingine mkubwa wake uko Hindi, nikamdirika hali yake hwenda chooni na kurudi chumbani tu. Lakini wewe mkubwa wao wote nimekudirika hwenda mpaka shamba na kurudi umeangata tita la kuni, isitoshe akili yako Mashallahu ina kumbukumbu imara. Ni vipi mambo haya?” Waziri aliuliza.
Mzee alicheka kiuungwana kisha akakipisha kimya kifupi.
“Niskize mwanangu…aghalabu ukipata mke mkorofi, ukazaa nae watoto wakorofi basi utazeeka upesi,” Mzee alianza kumwaga busara zake.
“Wamuona huyu mke wangu na utu uzima wake umemshuhudia akiingia ndani akirudi, lile tanga hakuna lingine ni lile lile moja tu nililomletea mimi. Nilipomwambia ni gumu mara ya kwanza, alirudi akalisuguasugua akaniletea. Nikamwambia bado, akarudi akalisuguasugua tena mpaka likawa laini. Hakunambia ‘Ah! Sasa uliyelileta si ni wewee, na ni hili hili moja tu hakuna linginee’. Hakuweza kuniudhi. Na daima haniudhi, si kwa maudhiko madogo wala maudhiko makubwa. Sasa nizeeshwe na lipi mwanangu, nami sipati tewengo la moyo, kila siku mapenzi t’ungu-nzima!”