Mwanadamu ni kiumbe wa mazoea. Hebu njoo nami tuangalie jinsi wewe mwenyewe unavyoishi nayo.
Pengine unalala upande huo huo(wa kushoto karibu na dirisha) wa kitanda chako. Pengine unaamka wakati huo huo(saa kumi na moja na robo alfajiri); pengine kiamsha kinywa chako ni hicho hicho(mkate, siagi na chai ya tangawizi)
Si ajabu kuwa unapita njia hio hio ya mkato unapoelekea shuleni au kazini(kupita nyuma ya kijiduka cha Mjomba karibu na muuzaji wa miraa) 😀 Shuleni unakaa nyuma kabisa mbali na macho makali ya mwalimu na kiranja wa darasa (kundi la “backbenchers” munajijua wenyewe )
Pengine vitabu vya hadithi unavyovisoma ni aina ile ile tangu ulipokuwa kidato cha kwanza; sinema au tamthilia “unazojipumzisha” nazo ni zile zile(za risasi na ngumi)
Jumapili jioni inapofika Baba akiwaalika mikahawani wewe hutaki kingine isipokuwa mishkaki na shawarma yako ya kila mara.
Hata watoto nao wanashamiri katika vitu au mambo waliyoyazoea. Ndio maana utamkuta analia iwapo umemwekea juisi yake kwenye kikombe cheupe ambapo yeye mwenyewe haridhiki ila kwa kikombe cha rangi ya samawati. Atakulilia hapo mpaka utakapombadilishia, Allah atustiri.
Wajua kuna maliwazo na utulivu katika mambo na ada tulizozizoea. Kana kwamba tunasema dunia iharibike, yatokee yatakayotokea lakini haya yetu bado yamebakia kama tunavyoyajua. Tunahisi amani na usalama.
Binadamu sisi hatupendi mabadiliko- yanatutia khofu na wasiwasi. Ndio sanasana tunaridhika na yetu tunayoyajua na kuyafahamu.
Lakini je, lau tungejiuliza: ” Pengine kuna mazuri zaidi nje ya mazoea yangu? Pengine kuna heri zaidi? Nitajua vipi ikiwa sitaruka hichi kizingiti nilichojiwekea mwenyewe?” Lau tungejiuliza tungeanzisha mangapi yenye manufaa nasi?
Sanasana, kinachoturudisha nyuma ni khofu. Khofu kuwa tujaribu tusoyajua, tujaribu yaliyo nje na mazoea halafu tusifaulu, tuharibikiwe, tuchekwe au mbaya zaidi tuumie mahali mwilini?
Jawabu, ndugu yangu msomaji, ni Allah peke yake ndiye ajuaye. Lakini kweli ni kuwa kiasi cha kwamba tuko tayari kujaribu mambo mageni kwetu ndiyo kiasi tutakavyo panuka kiakili, bali mara nyingi ndio huwa ni sababu sisi kufanikiwa kwenye njia zengine. Tukafaidika kiafiya na hali yetu ya kiuchumi kuboreka. La muhimu ni kuweka imani yetu kwa Allah na baada yake imani kwa nafsi zetu.
Utajuaje usipojaribu?
Sio lazima kuanza na makubwa. Sema bismillahi kwa jambo jepesi. Jambo ambalo halikutoi jasho au kukusabibishia moyo kuenda mbio kila unapolifikiria.
Pengine anza kwa kula mkate wa mofa badili ya mahamri, pengine uombe kuketi mbele karibu na ubao(asaa somo la Kemia litaeleweka baada ya hapo)
Kokote utakapoanza nakuahidi kuwa, kwa uwezo wa Allah, maisha yako yatabadilika hadi ya wewe kujiuliza: ” Kwa nini sikuanza mapema?