Ni mingi tumepitia. Ni mbali tumetoka, ila bado safari ni ndefu. Miradi hapa na pale, sheria kali dhidi ya wakiukaji na mikakati mizuri. Katu hatumkufuru muumba kwani hali ilivyo kwa sasa hivi sivyo ilivyokua jana. Nahisi jambo hili la vita vya kijinsia limeongelewa sana ila bado wengi wetu hatulifahamu. Ima ni kusudi au kutotaka.
Wamelipiga vita wengi wetu, ‘Oo, hatuwezi kusawazishwa na mwanamke’, ‘mwanamke mahala pake jikoni’, mara ‘ mwanamke mapishi’. Hivi nani kasema yote haya? Nani kaleta mtindo wa kuwaoza mabinti zetu mapema tena kwa jitu kubwa sawa amuite babu? Na hili suala la kuwauza mabinti zetu je linawapendeza? Kule maeneo ya Kilifi na Siaya kuna hili linalojulikana kama ‘fish for sex’ kwa kiingereza. Yani mtu anaupeana mwili wake kwa mvuvi ili apate kitoweo angalau akalishe familia yake. Mbona tuwadhulumu mabinti zetu? Kwani kusaidiana mpaka malipo? Tena malipo ya kikatili kama tunayoshuhudia? Je tumesahau kuwa hawa ndio viongozi wetu wa kesho? Tumeupeleka wapi utu na ubinadamu? Ni mambo ya kusikitosha mno.
Kuzinduka tumezunduka ila ni kama tunaambulia patupu. Kwani kila kukicha habari magazetini, ‘Fulani kauliwa na mumewe’, ‘Ukeketaji wa wanawake unaendelea sehemu mbalimbali nchini’, ‘Binti anajisiwa na kuuawa’. Mbona mambo kama haya yasipewe kipaumbele serikalini? Ni tofauti gani iliopo kati ya wake na waume? Si wote wana umuhimu wao? Hivyo basi wote wanastahili kuheshimiwa, kwenda shule na kusikizwa maoni yao bila upendeleo kwa jinsia yoyote. Kwani shida zote hizi zimeletwa kwa kuthamini jinsia moja kuliko nyengine.
Mikakati yenyewe iliopo haifuatiliwi, wanasiasa wetu ndio mwanzo wanaongoza katika kukiuka sheria walizoweka wenyewe. Si kinaya hiki? Sisi wazuri wa kunena ila kutenda balaa. Jambo hili limeendeleza kudhulumiwa kwa mabinti zetu. Sio kuwa watoto wa kiume hawadhulumiwi ila idadi ya kuukeni imezidi. Ni kana kwamba dhambi zetu zimetuzidia hivyo basi kuleta kuadhibiwa kwa duniani, tusiishi kwa amani huku akhera ikitusubiri kesho kwa adhabu za jalali. Ewe mola tunusuru.
~Swaga Khalfan