Samahani kijana, naomba uieweke simujanja yako kando. Sio lazima uweke mtandaoni namna daktari anavyokudunga sindano.
Samahani kijana, naomba uweke rununu kIpembeni. Haina haja kuweka mtandaoni kuonyesha waja msaada unaopeana kwa watu.
Samahani kijana, kwa dakika chache tu nakuomba utembee bila kutazama simu yako. Chukua mda huo kuangalia watu, vitu, njia na kadhalika.
Samahani kijana, ukiwa kwenye shughuli ya mkusanyiko wa watu, jaribu japo mara moja kuweka simu kando na kutangamana na ndugu jamaa na marafiki. Kuna umuhimu na faida pia katika kufanya jambo hilo.
Samahani tena kidogo, sio lazima ukiwa unafanya ibada utuwekee video mtandaoni. Unatuomba sisi au MwenyeziMungu? Wakati mwingine tunajikosesha malipo ya kitu kwasababu za kutaka kuonekanwa tu.
Samahani vijarunga, leo ningependa kuingilia maisha yenu. Najua hayanihusu ila kuna mda inakera. Je, ni mimi pekeyangu au wewe pia umegundua kuwa imekuwa ‘too much’? Nishaandika kuhusu hili na saa hii naandika tena na nitaandika tena na tena hadi nitakapohisi kuwa sauti yangu imewafikia wahusika. Nataka niwausie nyinyi. Ndio, nyinyi munaoweka kila jambo la maisha yenu katika mitandao. Nyinyi munaotuanikia Baraka za ukweli na za urongo kwenye mitandao. Ningependa munifahamishe munashindana na nani?
Faragha katika maisha kwa kiasi Fulani ni muhimu sana. Ni kipi tunachokitafuta haswaa katika mitandao ya kijamii? Umaarufu? Au ni kitu gani chengine?. Nashindwa kuelewa. Tazama jinsi jamii inavyopelekwa mbio na mitandao hii. Vipaumbele katika maisha yetu hivi sasa vimebadilika. Nia za kutenda mambo pia zimebadilika.
Shinikizo rika, kutojithamini na unyogovu ni sababu kidogo tu miongoni mwa sababu nyingi zinasosababisha mtu kutuchapishia maisha yake mtandaoni. Sababu hizi humfanya mtu kuona anahitaji upendekezo Fulani kutoka kwa watu hivyobasi anatupa mambo tumbunzima kwenye mtandao. Naweza sema ni asilimia kubwa ya watumizi hawa, huweka mambo mazuri tu. Kwa mfano, wataeka picha ya siku walioenda sehemu za starehe, kama vile mikahawani na kadhalika. Wataweka picha za vitu vizuri tofauti wanazo miliki au zisizokuwa zao. Wataongea kuhusu tabia zao nzuri, matokeo ya maisha mazuri na kila jambo zuri au jambo litakalompa mtu ‘attention’ atakapotuma kwenye mtandao. Bila shaka mambo mazuri haya hutufanya tukajidhania au kujiona na thamani ya juu, kwa namna tutakavyopokelewa mtandaoni. Walakin, jambo aula Zaidi ni kuwa matokeo yake ni kushindwa kujidhibiti. Kushindwa kuijua mipaka ya yanayopendekezwa kuwekwa mitandaoni na yasiyopendekeza. Tunakataa kufikiria tunachokiweka kitaleta faida au hasara katika maisha yetu na ya wenzetu. Mwisho wa siku, jambo la muhimu kabisa ni uamuzi wako. Jinsi utakavyoamua kutumia mitandao ya kijamii ndivyo itakavyokuathiri.
Yakini, wacha niseme munajidanganya tu kwa kudhani mitandao ya kijamii inawapa hadhi na kujiona muko na thamani kutokamana na upande mmoja tu wa uzuri munaoonyesha mtandaoni. Thamani ni jambo linalotokana na mtu binafsi yeye mwenyewe. Ni pale mtu anapotambua hadhi na heshima yake mwenyewe. Cha muhimu ni kwamba hatutambui kuwa kujithamini bora ni kule kukua bila ya kuogopa kutofaulu kwani kutofaulu hakubadilishi wala hakuharibu hadhi ya mtu.
Jambo la kusikitisha Zaidi utapata vijana wasiokuwa na uwezo wa kufanya mambo ya kifahari wawe na lazima wayafanye. Wanataka kufanya mambo pasi na uwezo wao kung’ana’ana vilivyo, ima kwa njia za sawa au zisizo za sawa ilimradi tu naye aweke mtandaoni kama wenzake. Hii ni hatari kubwa sana. Ni heri ikiwa tutaachana na vitu vinavyopita uwezo wetu. Hamu ya kutaka kuishi mitindo ya maisha tusioyaweza ni kubwa sana.. Narudia tena, iwapo tumekosa uwezo wa kupata au kumiliki kitu Fulani, tafadhali tukiwache, ikitokea kuwa ni lazima kukipata basi aula tuifanyie kazi ili tuipate.
Je, itakuwa nimekosea nikisema utumiaji wa mitandao ya kijamii ni kama utumiaji kwa sigara? Hakika, sioni tofauti kwani tushakuwa waraibu na imefikia mda sasa hatuezi kuenda bila simu. Tukitokea kuibiwa au kupokonywa simu tunanyauka, tunajawa na huzuni utasema tumefiliwa, tunakosa raha, tunakosa utulivu wa roho na tunahisi ni kama tunaachwa nyuma wenzetu wanasongea. Kama vile tunavyoweza kufanya mambo mengi tukitumia simu zetu basi halkadhalika tusipokuwa nazo.
Samahani kijana, naomba ukimaliza kusoma ujumbe wangu weka simu kando utafakari.
FAFI