Asilimia kubwa ya adinasi kisiwani Mombasa hutumia matatu au bajaji maarufu kama tuktuk kwenye usafiri wao wa hapa na pale. Matatu huweza kubeba jumuia ya abiria kumi na nne ilhali bajaji hubeba abiria watatu peke yake. Leo nimependelea niwaangazie aina tofauti ya abiria wenye kutumia magari hayo.
Abiria bubu. Abiria huyu ni kama kakatwa kilimi. Katu haongei kuanzia mwanzoni wa safari hadi hatimaye. Sana sana utampata kafurisha mashavu utadhani kaudhiwa na abiria wenzake. Hata kukatokea hali ya mtafaruku wowote, hasubutu kutenganisha mdomo wake. Ikimbidi sana utamsikia amesonya tu. Maongezi yake yanakuwa kwenye matendo au aashirie na uso wake.
Aina ya pili ya abiria ni naibu dereva, wala sio utingo. Abiria huyu utadhani ndio macho ya dereva. Anamuongoza na kumpa tahadhari dereva huyo kila sehemu na kila wakati.Mhepe huyo!.. Cheki bumps hizo mbele… Angalia hilo shimo hapo.Anaona kila kitu, mbele, nyuma na hata ubavu. Anajua hadi abiria wanaokwenda naye safari moja. Mara tu utaskia, mbebe huyo mother anaenda pia. Na sio macho tu ambayo huwa sambamba bali hata masikio. Anaskia kila kitu, kukiitishwa change tayari kashaingiza mikono kwenye mifuko yake na kutazama kama ana pesa hizo.
Tazama, yupo abiria mchanganuzi au tumwite mchambuzi. Wananishangaza sana abiria hawa kwasababu hukaa tayari na ripoti zao. Kukatajwa mada yoyote ile huwa ni kama kateuliwa kutoa taarifa. Ataifafanua kimasomaso kwani atatoa historia, takwimu, vigezo, matatizo, suluhisho ilimradi yeye huwa na maelezo kamilifu kuhusu mada hiyo. Si siasa, si mpira, si biashara si tabia za vijana, si matatizo yanayoathiri jamii, aghalabu yeye hufahamu kila kitu.
Mwenzangu, kunao abiria wakiingia tu kwenye gari huwa ni kama wamedungwa sindano za usingizi. Gari likianza kuondoka na kuingiza kipepo kitamu, macho yanaanza kujifunga na mwia tu utampata anadonadona kwenye kiti. Anasinzia kama gude. Dharubu za kudona zikishamchosha, anajiegesha vyema kwenye kiti hicho ili kuepuka izara hiyo. Mda tu utamsikia anakoroma. Hata gari lisukesuke vipi, utampata ameganda kwenye kiti habari hana. Kachoka bwana huyu! Wengine huishia hapo ila wengine usingizi unapozidi kukolea nyute huanza kuwatoka. Jambo la kustaajabisha ni kuwa ni nadhra sana kuwaona wakipitwa na sehemu wanazostahili kushuka.
Yupo abiria ambaye kutoka wakati apande gari hilo hadi atakaposhuka huwa amewacha taswira kamili na kuweka dhahiri kama jua la mtikati maisha yake. Aila yake, mali zake, vyeo vyake, ndugu zake walioko ughaibuni watajulikanwa, bei ya nguo na viatu alivyovaa, sehemu anakonunua vitu vyake, vitu anavyopenda na asivyovipenda. Hana siri ya maisha yake. Ukweli wa anayoyadhihirisha ni MwenyeziMungu pekee ndiye aujuaye. Mara nyingi abiria hawa huwa ni wanawake au wasichana.
Teknolojia ni moja wapo wa mambo yanayotuathiri sana sisi wanaadamu. Kunao abiria ambao muda wote wa safari wapo kwenye simu zao. Wameinamisha vichwa vyao na wala hawavienui isipokuwa wakati wa kutoa nauli na kupokea kisalio iwapo kipo chochote. Vidole navyo vimehamanika vinapapasa simu janja zao. Utadhani wanashindana. Hawaangalii gari linavyokwenda au hata abiria aliokaa kando yao. Wapo wengine ambao ghafla dereva akiweka mziki unaowagusa sana, wanaanza kuchukua video huku wanaimba kisha wakiviweka kwenye mitandao ya kijamii. Wapo ndani ya gari ila ni kama hawapo. Wapo viwiliwili tu.
Hakika kuna tabia moja mbaya sana ambayo baadhi ya wanaume huwa nazo. Kuna mijanadume haiwezi kukaa tu na amani hadi watakaposhuka. Akiona kidosho kakaa kando yake basi lazima kama ibada atafte namna yakumzungumzisha. Arushe mistari miwili mitatu ili ajipendekeze ilhali huwa hawana lulu wala lulumizi. Wengine huitisha hadi nambari za simu. Wanaume hawa huwa wasumbufu sana. Pindi tu atakapotoa salamu na amejibiwa vizuri basi ndio anaanza mission yake. Tena hawachagui. Sio watoto wa shule, sio akina mama, bora tu awe kavalia sketi au gauni..
Aina nyengine ya abiria ni baadhi ya kina mama. Ghafla utaona ameingia mama kwenye gari na watoto kama watano hivi, ila anataka kulipia kiti kimoja. Loh! Sielewi huwa wanapanga kukaa vipi. Huruma za abiria wengine zikiwa nyingi basi kila mmoja amchukue mtoto mmoja ampakate. Au pengine apate viti visivyokuwa na watu, basi utamsikia akimuambia utingo, nawaeka hawa hapa mtu akiingia nitawaondoa. Hivi itakuwa ni hali za maisha ndizo zinazowafanya kutenda hayo au ni kujisheua tu?
Aina ya mwisho ya abiria ni ‘mhubiri’. Ukimya wa safari huja kuvunjwa ghafla na abiria huyu, anapopokea rununu yake, anaongea kwa fujo na sauti ya juu sana. Hapa ndio kila aliyetulia na kutuama atatweta na kuhema. aliyelala ataamka na aliyezama zii katika dimbwi la mawazo atazinduka. Atahubiri maongezi yake yote. Tena huku anaashiria kwa vitendo kana kwamba mwenziwake anayeongea naye anamuona.
Abiria wako aina nyingi sana, nakukaribisha na wewe uniambie unaowajua.