Kila nilivyomuangalia Subira machozi yalinibubujika tele njia mbili mbili. Sikuamini katu kuwa huyu ndiye aliyekuwa mwandani wangu tangu utotoni. Alikuwa amelala usingizi wa pono bila ya kuhisi chochote kwani nina yake Bi. Mrembo alinifungulia mlango wa chumba chake na kunieleza hali yake na yote yaliyomtokea bila ya yeye kuinuka. Nilivuta taswira nyuma na kukumbuka zile zama tulipocheza na kukua sote. Tulienda shuleni na kurudi pamoja, tulicheza ‘kibe’, ‘kode’, mchezo wa kukimbia na hata kula na kuzurura mtaa sote hadi tukajulikana kama ndugu wa toka nitoke.
Mara ya mwisho kuonana na Subira ilikuwa miezi mitatu iliopita. Alikuja kuniaga katika kituo cha magari nilipokuwa naelekea Nairobi kusomea shahada ya udaktari katika chuo kikuu cha Nairobi. Uso wake uligeuka mwekundu huku machozi yakimlengalenga kwa huzuni ya kutengana nami. Mimi nilijaribu niwezavyo kupigana na hisia hiyo na hatimaye nilishindwa kwani machozi yalinichuruzika chururu. Hakuna aliyeweza kuhimili huzuni ya kutengana na sahibu wake kwani tuliandamana mahali popote pamoja kama mtu na kivuli chake. Tulisoma shule pamoja kuanzia chekechea hadi shule ya upili. Tulikumbatiana na kuahidiana kuwa kila mmoja angemtembelea mwingine wakati wa likizo.
Kila Jumamosi nilitenga muda maalum wa kuzungumza naye kupitia rununu. Tulipiga gumzo na alinihadithia kila tukio lililotokea mtaani kwetu Majengo. Nilicheka hadi mbavu zikaniuma kila alivyonisimulia hadithi za mzee Juma aliyekuwa akipenda kugombana na mkewe akitaka ampikie vyakula ainati ilhali hakuwa na magego ya kutafunia. Subira alijiunga na chuo kikuu cha Kenyatta Mombasa na alisomea shahada katika ualimu. Wimbo wake tangu utotoni ulikuwa ni wa kutimiza ndoto ya kuwa mwalimu na alipopata fursa aliikimbilia kwa furaha isiyo na kifani.
Jumatatu moja, Subira aliabiri basi kuja Nairobi kukutana nami. Tuliongea kwa simu tukiwa na bashasha na aliniuliza kama nilihitaji kitu kutoka kwetu na kama ada yangu nilimuagiza achari ya maembe na ya mbirimbi aliyokuwa akiifanya jirani yetu Bi.Mtamu. Alifanya achari nzuri hadi tuligoma kutoa sahani zikaoshwe tuliramba mpaka zikang’aa ungedhani ni mpya. Aliniambia alikuwa na jambo muhimu sana alilotaka kuniambia na juhudi zangu za kumrai anipe fununu kuhusu jambo hilo zilitumbukia nyongo. Alishikilia kuwa lilikuwa muhimu na asingeweza kuniambia kwenye simu. Gari liling’oa nanga na lilipofika Mtito Andei lilikumbana na ajali mbaya. Dereva alikosa kudhibiti gari nalo likapenduka mara mbili na kulipuka. Subira alibahatika kama mtende kwani kila mmoja aliaga dunia isipokuwa yeye. Alipata jeraha kubwa kichwani na kupoteza kumbukumbu yake.
Nilipopata habari ya ajali hiyo kwenye runinga moyo ulipiga kwa kasi sana. Kijasho chembamba kilinitiririka usoni na mwili mzima ulitetema kwa hofu. Akilini nilimfikiria Subira pekee na nikakimbilia kituoni kuabiri gari. Mawazo yalinizonga nikifikiria hali rafiki yangu aliyokuwa yuko. Ama kweli ajali haina kinga. Nilimuomba Rabana amuhifadhi Subira. Alizuiwa hospitalini kwa muda wa majuma mawili kwani hali yake ilizidi kuzorota. Nina yake alijawa na wasiwasi na nilipata tabu sana kumtuliza kwani hakuongea kwa muda mrefu. Wanahabari nao hawakuachwa nyuma kwani walikuja kumhoji nina na kuandaa taarifa iliyogonga vichwa vya habari kuhusu msichana aliyeponea kifo wengine walisema aliyebarikiwa ilimradi kila mtu alipata la kunena na habari zilienea kwa kasi mithli ya moto unavyochoma nyasi. Subira alipoanza kupata afueni aliruhusiwa kuenda nyumbani na madaktari walisema kuwa hali yake haitabiriki na huenda asipate fahamu kabisa au akapata fahamu wakati wowote na tusimlazimishe kukumbuka wala kumpa dhiki yoyote.
Tulimshukuru Maulana kwa kumponya Subira na tulizidi kumuombea apate fahamu vizuri. Ghafla bin vuu, Subira aligutuka kutoka usingizini na kupiga ukelele mkubwa. Bi. Mrembo alimkimbilia kwa haraka na kumuuliza, “Una nini mwanangu?”Subira alimtazama kisha akaniangalia mimi kwa muda na kumuuliza, “Huyu ni nani mama?” Nilijaribu kuzuia machozi yangu yaliyojaa machoni kwa kuyafuta na kitambaa. Nilitamani kumpigia kelele na kumlaumu kwa kunisahau lakini sikuweza. Niliondoka kuelekea nje nilikolia kwa kite na simanzi. Nilifuta machozi nilipohisi mkono juu ya bega langu na kugeuka. Subira alikuwa nyuma yangu na alisema, “Jamila rafiki yangu…” Kabla hajaendelea nilimkumbatia kwa furaha na kumuambia, “Subira vipi hali yako? Je maumivu yamepungua? Usijali utapona na utakuwa na siha njema. Umenikumbuka sasa? Nilidhani hutanikumbuka tena.” Subira aliniangalia kwa mshangao na kusema,
“Sijambo namshukuru Mola kwa kila kitu. Asante sana kwa kunishughulikia na kuwa nami wakati wote. Pole sikukumbuki mama yangu ndiye aliyenieleza kuhusu urafiki wetu.”
Nilikunja uso ukakunjika huku machozi yalinibubujika na bila ya kufikiria nilimshika Subira mabega kwa nguvu huku maneno yalinitoka kinywani mwangu, “Mbona utakuwa hivi Subira? Hukumbuki nilipokuwa nikigota mlango wenu kila asubuhi ili twende shuleni pamoja? Je umesahau jinsi tulivyokuwa tukiyabukua mabuku sote wakati mtihani wa kitaifa ulipokaribia tukiwa nyumbani? Hukumbuki tulivyocheza pamoja na kuhakikisha kila siku tulionana wakati wa likizo? Nilizungumza na wewe kila Jumamosi nilipokuwa Nairobi na tuliongea kwa simu kabla hujaabiri gari na kupata ajali. Nilijawa na wasiwasi uliponiambia una jambo muhimu sana usiloweza kuniambia kwa simu na mpaka sasa najaribu kubahatisha kuhusu jambo hilo. Ni jambo gani? Jaribu kukumbuka! Subira aliyaondoa mikono yangu mabegani mwake na kushika kichwa kwa muda kana kwamba anakumbuka matukio ya maishani mwake kisha akaniangalia kwa huruma na kusema, “Nisamehe Jamila sikumbuki na nikijaribu kujilazimisha nahisi maumivu kichwani.”
Subira aliingia ndani akiniacha katika hali ya kuhuzunisha. Nilihisi kama viungo havifanyi kazi nikaketi chini haraka nikiogopa kudondoka. Nililia kama mtoto mdogo aliyenyang’anywa chakula nikatamani ingekuwa ni ndoto mbaya inayonihitaji kufumbua macho tu kuiangamiza. Moyo uliniuma ungedhani nimedungwa mkuki. Nilitamani ajali ile haingetokea kwani nilimpoteza kipenzi wangu.