Ilikuwa zamu ya Tatu, binti mdogo mwenye umri wa miaka ishirini kupanda jukwaani na kuutumbuiza ummati na nyimbo aliyokuwa amejiandaa nayo siku hiyo. Alinyanyuka na kuvipanda vidato vya jukwaa taratibu kama aliyetahadhari kutopiga kelele kutokana na viatu vyake vya kodonkodo alivyokuwa amevaa. Rinda la kijani kiwiti lilitulia barabara katika ngozi nyeupe iliochanganyika na wekundu wa mrembo huyu. Kila mara alizisogeza nyuma nywele zake singa zilizokuwa nusura kufunika jicho lake la kushoto. Alisimama mbele ya kipaza sauti na kukishusha chini ili aweze kukifikia kutokana na ufupi wake uliompendeza na kumkaa sawa sawa. Aliwaangalia waliohudhuria Kwa macho yake makubwa na ya kulegea, akatabasamu na kudhihirisha vidu vyake kisha Kwa ujasiri mkubwa akaanza kuimba.
Rama, shababu mwenye umri wa miaka ishirini na minane, aliyekuwa amekaa nyuma na aliyeonekana kusinzia sinzia aligutushwa ghafla na sauti ya Tatu. Sauti ile ilipenyeza hadi katika moyo wake na kuuyeyusha. Bilauri ya sharubati aliyokuwa ameishika ilimponyoka na mara akajiona yupo katika ulimwengu tofauti. Alimtizama Tatu na kumuona kama malaika aliyemsimamia mbele yake. Moyo ulimwenda mbio na hisia asizozielewa kuchukua nafasi katika moyo wake. Tatu alimaliza kuimba na hadhira ikashangilia Kwa shangwe na hamre hamre. Bila shaka, alistahili shangwe na zaidi kwani sauti yake ilikuwa kitu tofauti. Rama alikuwa bado ameduwaa na macho yake yalikataa kata kata kumbanduka Tatu. Alimuona kama kiumbe cha ajabu ambacho hajawai kukiona maishani mwake.
Mashindano yalifikia hatima lakini sauti ya Tatu bado ilikuwa ikicheza densi katika masikio ya Rama. Rama alivaa ujasiri na kwenda hadi alipokuwa ameketi Tatu. Alijaribu kuongea lakini ulimi wake ulimsaliti. Alichukua kitambara kutoka mfukoni mwake na kujifuta jasho lililokuwa likimtirika jari moja licha ya kuwepo Kwa viyoyozi kila kipembe. Hatimaye ulimi wake ulisalimu amri na aliweza kuongea japo Kwa kigugumizi.
“Ha..ba..ri yako mrembo!” Alitoa salamu Rama huku mapigo ya moyo wake yakizidi maradufu.
“Nzuri sana.” Aliitikia Tatu huku akimtizama Rama kwa jicho la maswali.
“Naweza jiunga nawe?”
“Ndiyo! Bila shaka.”
Rama alisogeza kiti na kukaa. Kwa muda mchache, wote walikuwa kimya huku wakiangaliana kisiri siri. Rama alipomtizama Tatu, Tatu alijifanya anaitazama simu yake na vivyo hivyo ilifanyika Kwa Rama. Hatimaye Rama aliuvaa ujasiri na kuuvunja ukimnya uliokuwa umeshika usukani.
“Naitwa Rama!”
“Nami ni Tatu.”
“Jina zuri sana. Nimependezwa sana na sauti yako pamoja na kipaji chako cha kuimba. Kweli umebarikiwa.”
“Asante.” Alisema Tatu mwingi wa haya.
“Ningependa tufahamiane zaidi Tatu ila naona saa hi muda umesonga sana na sitoweza kukueleza yote niliyodhamiria kukueleza. Sijui kama naweza kupata namba yako ya simu.”
Tatu alisita kidogo lakini baada ya kubembelezwa na kuraiwa kwa muda alimuandikia Rama namba yake ya simu.
Mawasiliano yalikuwa mchana kutwa usiku kucha na penzi la Rama Kwa Tatu lilizidi kunoga. Walipendana na kushauriana mambo mbali mbali ya kimaisha.Wanakijiji katika kitongoji alimoishi Tatu, walimuonea sana gere Tatu baada ya kumuona akiletwa na kuja kuchukuliwa kwa gari la kifahari.
“Aah Tatu amemroga bwenyenye yule ili amuoe tu.” Walinong’onezana wao kwa wao.
“Ndivyo hivyo, sisi tutabaki kuolewa na wachochole wenzetu tu.” Aliongeza mwengine.Hata hivyo, Tatu aliyapuuzilia mbali yote hayo na kuamua ima fa ima lazima alipate alitakalo.Mapenzi yalikuwa mubashara na moto moto na Rama hakuona tena sababu ya kupoteza muda wakati ashampata mwanamke aliyekuwa akimtafuta kwa udi na ambari kwa miaka dahari. Alishauriana na Tatu kuhusu nia yake ya kumuoa naye hakusita kukubali.
Rama aliamua kwenda Kwa halati yake Tatu ambaye alikuwa mtu wa pekee katika maisha ya Tatu baada ya wazazi wake kuuliwa kinyama. Rama aliduwaa nusura atoke mbio baada ya kumuona halati yake Tatu.
“Shikamoo halati!” Alimsalimu Tatu halat yake.
“Marhaba mwanangu! Naona leo umeniletea mgeni.”
“Ndiyo halati! Huyu ndiye yule ghulamu niliyekuelezea, Rama.”
“Ooh nimefahamu. Hujambo Rama!” Halati alimgeukia Rama huku akitabasamu baada ya kuiona hofu iliomvaa tangu aingie nyumbani humo.
“Si.. ja ..mbo! Halati ni kama nimekufananisha lakini.”
Alisema Rama Kwa hofu kuu.
“Sidhani kama tunafahamiana. Duniani wawili wawili mwanangu.” Halati alimhakikishia hilo Rama naye akashusha pumzi. Mazungumzo ya posa yalianza rasmi na mikakati ya ndoa ikapangwa.
Ilikuwa tarehe ishirini na mbili mwezi wa tatu. Siku muhimu katika maisha ya Rama, mmh! Na Tabu pia labda. Siku ya harusi yao. Rama alikuwa yupo katika chumba chake akijitazama kwenye kioo huku akiitengeza vyema suti yake. Ghafla alijiwa na fikra.
“Mmh mbona hii tarehe ya leo ni sawa na Ile tarehe ya…. mbona halati akataka harusi iwe tarehe ya leo. Aaaah ni sadfa tu.”
Aliitupilia mbali fikra hiyo na kuendelea kujitengeza vyema. Lazima apendeze,ni siku muhimu kwake ebo! Tatu naye alikuwa katika pilka pilka za mwisho mwisho za kupodolewa na wapambaji mbuji waliolipwa senti chungu nzima na Rama ili wahakikishe mwari anapendeza. Ghafla Tatu alianza kulia. Aliyakumbuka maisha yalivyokuwa bulbul kabla ya kifo cha wazazi wake. Alitamani mama yake angekuwepo katika siku hii muhimu ya maisha yake. Ghafla hisia za majonzi zilitoweka na kuzibwa na ghamidha iliokita mizizi katika moyo wake. Alitamani siku ifike. Siku aliyoisubiri. Siku ambayo ataipata haki.
“Usilie Tatu, utaharibu ‘make up’ mpenzi.” Tatu alizinduliwa ghafla katika bahari ya luja na sauti ya mpambaji. Aliyafuta machozi yaliokuwa hayajakoma kumbubujika na kuvaa tabasamu bandia. Tabasamu ya kweli ilipotea baada ya kifo cha wazazi wake. Neno furaha kwake lilionekana neno lililozikwa punde tu walipozikwa wazazi wake.
Uwanja ulipambwa ukapambika. Si taa za kila rangi, si maua yaliopangwa Kwa ustadi, si meza na viti vilivyovishwa vitambara vya kijani kiwiti, si vyakula mzo mzo vilivyotengewa sehemu maalum. Aidha ,Watu walifurika ungedhani ni sherehe za jamhuri. Nyimbo za kuburudisha na kuongoa ngoa ziliwashwa na watu wenye vipaji vya kucheza walipata fursa ya kuvionyesha vipaji vyao. Watu walikula shibe yao. Wengine walibeba vyakula kwenye mifuko na wengine kwenye mashati. Walirusha roho si haba. Hatimaye, muda uliosubiriwa Kwa hamu uliwadia, muda wa kuingia maarusi. Si vigelegele na nderemo. Picha zilipigwa na sherehe zikatia nanga. Rama alimchukua mkewe na kuelekea nyumbani kuanza maisha mapya kama mume na mke.
Jumba la Rama lilikuwa jumba la kifahari lililojengwa Kwa nusu vioo nusu mawe. Lilikuwa na vyumba takriban kumi na wafanyikazi karibia watano. Tatu alisimama tutwe mlangoni akashindwa kuingia ndani. Alilitizama lile jumba Kwa makini kisha akamtizama Rama.
“Usijali mke wangu, hii yote ni mali yako sasa.”
“Nafahamu.” Alisema Tatu huku kamkazia macho Rama. Rama alishangazwa na jawabu lile lakini akalipuuzia.
Tatu na Rama waliishi kwa mapenzi na itifaki. Ndoa yao ilitawaliwa na furaha iso kifani. Licha ya hayo yote, kila wakati Tatu alionekana mwenye mawazo mengi sana.
“Mbona mke wangu aghlabu unaonekana mwenye mawazo?” Rama Aliamua kumaliza shauku yake siku moja walipokuwa wakila chajio.
“Nipo sawa mimi. Ni kuwatamani tu wazazi wangu.” Alijibu Tatu huku akionekana kuificha hisia flani iliokuwa inataka kujidhihirisha.
“Usijali mpenzi, mimi nipo hapa, ondoa wasiwasi na fikra nyingi.” Alisema Rama huku akimkumbatia mkewe Kwa mapenzi tele.
Siku iliofuata ilikuwa siku ya Tatu ya kuzaliwa. Rama aliamua kumpatia mke wake laazizi, nyonga mkalia ini zawadi ambayo hangeitarajia maishani mwake. Alirudi nyumbani kutoka kazini siku hiyo akiwa na bashasha tele. Alifika na kumkabidhi Tatu bahasha iliojaa stakabadhi ndani. Tatu hakuamini alipogundua kuwa ni stakabadhi za nyumba na magari ambazo zimebadilishwa na kuandikwa jina lake. Aliogelea katika bahari ya furaha mzo mzo na kumkumbatia mumewe huku machozi ya furaha yakimbubujika.
“Nafanya haya yote ili kudhihirisha mapenzi yangu kwako. Sikudhania katika maisha yangu nitakuja kumpata mwanamke nitakayempenda kiasi hichi. Nakupenda sana Tatu na nimeona hii ndiyo njia pekee ya kukudhihirishia hilo.” Alisema Rama mwingi wa mapenzi ya dhati.
Asubuhi Rama alidamka alfajiri kama kawaida yake na alipotizama pembeni aliona kiamsha kinywa kipo tayari. Alifurahika sana kuona kuwa mkewe anazidi kuonyesha upendo kwake. Alichukua kikombe cha chai lakini chini aliona barua.
“Mmh barua za asubuhi asubuhi! Huyu Tatu mtundu.” Aliifungua barua huku akitabasamu.
Ramadhani Mkavulo,
Najua umeshtuka kuiona barua hii. Nisiwe mneni sana acha nikuelezee yote yaliokuwa yamenisonga moyoni. Kwanza kabisa mimi ni mtoto wa Bi Zakia na Bwana Hamisi, viumbe visivyokuwa na hatia ulivyovitowesha ulimwenguni kikatili miaka miwili iliopita. Hiyo siku ulipotuvamia nyumbani kwetu yaani katika hilo jumba unalojinaki ni lako, nilikuwa narudi kutoka shuleni niliposikia ukwenzi wa mama kutoka mbali.Nilinyatia nyatia na kujificha kando kidogo ya nyumba na kuchungulia kupitia tundu ndogo iliopo katika ukuta ulioizunguka nyumba yetu. Niliyaona yote! Niliona ulivyomzamisha mama yangu katika kidimbwi na kumkata kichwa baba yangu bila huruma. Taswira ya unyama uliowafanyia wazazi wangu bado ipo katika akili yangu. Nilikutambua siku ya kwanza tu nilipokuona katika mashindano yale ya kuimba. Sikutaka kuchukua hatua ya haraka sana na nikaamua kwenda nawe pole pole. Kweli Mungu si Athumani! Ulijileta mwenyewe kichinjioni na pia kunirahisishia kazi Kwa kuandika mali zote kwa jina langu japokuwa mimi ndio mmiliki halali wa mali hizo. Niliamua kuchukua hatua hii nzito ya kuolewa na wewe ili tu nilipize kisasi na nipate haki. Isitoshe hii yote ilikuwa mipango yangu na halati. Unakumbuka ulipomuona halati ukashtuka. Najua ulishtuka kwasababu anafanana sana na mama yangu na pengine ulidhani ni mama yangu uliyemuua. Hayo ndio yote niliotaka kukwambia. Mwisho kabisa, nimefunga milango yote ya nyumba hiyo na polisi watafika muda wowote.
Tatu Hamisi
Rama alimaliza kusoma barua lakini bado alikuwa haamini alioyasoma. Alidhani pengine yupo katika ulimwengu wa ruiya. Aliyakuna macho yake kuhakikisha kuwa hayamhadai na kuisoma barua kwa mara nyingine tena. Mikono ilimtetema na jasho kummiminika katika kila kiungo cha mwili wake.
“Ta…ta..ta….tu! A..na..we..za..je?…aah Rama nimekwisha. Sina jinsi.” Alijisemesha Rama huku akikizinguka chumba chake kama anayetufu. Alienda kutafuta upenyu wa kutoroka lakini ilikuwa kweli milango yote ilifungwa kwa nje. Muda si mlonje, mapolisi walifika na kuizunguka nyumba hiyo. Rama alikamatwa na kutiwa pingu. Alimtizama Tatu aliyekuwa amesimama nyuma ya polisi Kwa jicho la kutoamini. Alijuta kwanini hakuweza kufahamu kuwa Kwa muda huo wote aliishi na adui yake. Usilolijua ni usiku wa kiza kweli. Rama alihukumiwa kifungo cha maisha Kwa kosa la uuaji na uporaji wa mali.
Tatu na halati walifurahika mno baada ya kuipata haki na kuzipata tena mali zao zote. Hata hivyo, kadri siku zilivyozidi kusonga, kuna hisia flani ilioendelea kukua katika moyo wa Tatu. Aligundua kuwa anamtamani Sana Rama. Alijikuta anashindwa kuishi bila Rama. Alikosa furaha ya maisha kwa kuishi bila Rama. Loh! Kumbe moyo wa Tatu ulikuwa umeanza kuota mapenzi juu ya Rama bila ya yeye kujifahamu. Alishindwa la kufanya!