Bila shaka intaneti ni nyenzo muhimu katika kuzalisha maendeleo. Sekta aina nyingi zimeboreshwa kwa ujio wa kipengele hiki. Hivyo basi, kuchangia pakubwa katika kuimarika kwa uchumi wa nchi. Ila ningependa kuchukua fursa hii kuzungumzia hususan mitandao ya kijamii.
Swadakta, mitandao ya kijamii ni huduma ambayo watu huitumia na huletwa pamoja na watu wengine, ikiwemo kujenga urafiki miongoni mwao. Mifano ya makala ya mitandao ya kijamii ni kama ‘facebook’, ‘instagram’,’whatsApp’, ‘twitter’ na kadhalika. Asilimia kubwa ya watumizi wa mitandao hii hutumia kupitia simujanja. Vilevile, ndani mna mukundi inayokusanya waja wenye shuku ya aina moja kama vile dini, waandishi, mpira wa miguu,shule na kadhalika.
Aidha, mitandao ya kijamii hutumiwa na wanabiashara kutangaza bidhaa zao kwa njia ya picha ua hata filamu fupi fupi. Wanahabari nao hutumia chombo hiki kukusanya habari zinazozijiri. Mashekhe na waubiri hawakuachwa nyuma kwani huitumia kusambaza mawaidha yanayotokamana na ilimu za dini. Hatimaye wapo wale wanaoitumia kwa njia ya kupitisha mda tu wakiwa mapumzikoni au hata kazini.
Mitandao hii imeundwa kwa namna ambayo kila mwenye ufahamu wa kusoma na kupiga chapa anaeza kuitumia. Kwa ujumla tunaeza sema kuwa mitandao ya kijamii ina faida nyingi sana. Sasa, ningetaka tutafakari namna ilivyopokelewa na wengi wetu. Ni jambo la kusikitisha mno kuona jamii yetu ikizoroteka kimaadili kupitia mitandao hii.
Labeka! Siku hizi watu huanika kila hatua ya maisha yao kwenye mitandao.
Wakiamka hadi wakilala, Januari hadi Disemba. Kwa mfano utamuona mtu kaachia ujumbe ,
“Naelekea Nairobi”
Sasa, ndio tufanyeje? Tuje tukupokee kwa gwaride? Au azma haswa yakuacha ujumbe huu ni gani?
Pengine uone,
“Mume wangu, kipenzi changu”
Kwahiyo? Inamhusu nani kuhusu mume wako? Mmh!
“Karibu duniani kischana chetu!”
Jamani! Mtoto mchanga hata kuona hajaanza, tayari kashaanikwa mitandaoni utadhani ni bidhaa inanadiwa.
Hivi tunafahamu fika kuwa kijicho kipo? Sio kila mtu unayemjuza habari za maisha yako anafurahia. Wangapi wamekaa miaka majumbani hawajapata kazi? Ni wangapi wanatamani mtoto lakini hawajajaaliwa? Ni wangapi wanatamani japo mwaka kwa mara moja kula hotelini? Ni wangapi walitamani kufika angalau chuo kikuu lakini kwa kukosa uwezo hawakuenda?
Inatulazimu kujitahadhari. Kuna umuhimu mkubwa wa kuweka faragha maisha yetu. Ishi kwa lengo la kumridhisha MwenyeziMungu, sio watu. Mitandao sio ya kurekodi matukio ya maisha yako. Ujumbe mwingine haufai kusambazwa. Katu haipendezi.
Pili, ni kuwaona vijana kukosa dira ya maisha. Hii ni kwa jinsi wanavyokesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa kwenye simujanja zao. Wanapoteza mwida wao wakati wangelikuwa wanatumia wakati huo kwa jambo aula zaidi. Akili zao zimekorogeka. Wamekuwa zumbukuku. Hawaambiliki hawasemezeki, hawaliki hawatafuniki, hawapiki na wala hawapakui. Wamesahau kuwa maisha ni bahari yenye papa na papaupanga na uhai ni umande, lichomozapo jua la kifo, huyeyuka kama barafu. Ndivyo ujana wao unawapita hivyo tu, kama moshi.Ni vyema tukizingatia haya ili tusije kuishia laiti tungalijua na vyanda viwili kinywani. Tazama ewe kijana! Maisha ni wajibu, tekeleza.
Jamani! Dunia inaelekea wapi? Ipo hoja moja kubwa kuhusu mahusiano yanayotokana na mitandao hii. Vijana wadogo wanajiingiza kwenye mahusiano shaghalabaghla. Hawaelewi hata maana ya penzi ni kitu gani. Utamkuta mschana katembea na wanaume sita pengine kwa mda wa miaka miwili. Bado hajaolewa bado ni mdogo ila keshachukia wanaume. Amefanya mambo chungu nzima na wanaume tofauti. Sasa kwa mume wake ataenda kufanya nini? Na kadhalika kwa wanaume. Wanajikoroga akili zao. Wanatokea kupata maono tofauti kuhusu penzi,mume au mke yasiyo sahihi kwani maana halisi utaijuwa ukiwa kwenye ndoa. Hii imechangia pakubwa kukithiri kwa talaka awamu hizi. Jambo hilo sio sahihi kidini. Kwahiyo mitandao ya kijamii imeizidisha sana kiwango cha zina. Simu zimekuwa tundu za kuta za nyumba zetu. Wanawali wamekosa haya na mabarobaro wamezidi ukosefu wa adabu.
Tonge lililokolea mchuzi lahitaji ujuzi kulimeza. Kwanza ni lazma tukubali kuwa mtandao ni kama msumeno hukereza mbele na nyuma. Yaani japo una faida zake nyingi umebeba maafa pia. Pili, tunapaswa kuwa na fikra moja ya kutaka kupiga vita matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Kisha, ni vyema ikiwa tutashikamana na mafunzo ya dini ili kuepukana na mitego ya mitandao. Mtume Muhammad rehma na amani zimshukiye yeye alisema,
“Ikiwa hauna haya, basi fanya utakacho”.
Kubwa tuwezalo kufanya, ni kuambiana na kukumbushana. Namuomba MwenyeziMungu atuongoze, atujaalie hekima ya kuelewa na kutofautisha baina ya maovu na mema. Amin