Picha: https://stephenmunene.files.wordpress.com
Jina langu ni Najma Saleh Abdusheikh maarufu kama Mamake Usaamah; maarufu zaidi kama mraibu wa chai nambari moja. Nakukaribisha katika ulimwengu wangu wa vitabu, uandishi na kusikiliza ile sauti kichwani mwangu. Usishtuke, sina wazimu, Alhamdulillah. Naamini kuwa sisi waandishi na wapenzi wa vitabu na kalamu- au pengine niseme wapenzi wa tarakilishi na simu za mkono- tuna sauti zinazotupeleka tutake kujitenga kando na wenzetu huku vidole vikikimbia mbio kwenye kurasa au ‘screen.’ Ngoja nikugusie masuala mawili ambayo- wanaonijua watashuhudia- hamna kikao nilochokuwemo mimi isipokuwa mawili haya nimeyazungumzia. La kwanza ni uchafu na Mombasa. Tangu utoto wangu nakumbuka kusinywa kabisa na takataka na uchafu ndani ya hili jiji letu. Kiasi cha kuwa, na Mamangu Mama Maryamu atawaeleza zaidi, nilikuwa nikiota naisafisha Bahari Hindi. Wengi wametuambia kuwa sisi wenyeji wa Mlango wa Papa tumebahatika kuishi karibu nayo. Mmmhh, bahati gani hiyo! SubhanaAllah! Utasinywa na vile takataka zinavyorushwa kwenye bahari bila wenye kurusha kuhisi dhambi yoyote. Si magodoro ya zamani, si mipira ya kufinika chini walivyopanda bei watu wakaitupa na wakaweka ’tiles’, si mabaki ya chakula! Jamani Mombasa ni yetu! Basi ujue mimi ndiye yule anaye kihifadhi kikaratasi cha funiko wa chupa ya maji swiha. Mara hukitumbukiza kwenye kibeti changu, mara huzuia hadi nifike nyumbani. Pia, ni mimi yule atakaye kukodolea macho ya ukali na lawama pale ninapo kukuona watupa taka – hata kama karatasi ya mjazo wa simu- barabarani. Ndugu yangu- uchafu ni aibu na usafi unaficha umaskini. Kesho likipita gari la watalii sitaki kuinamisha kichwa changu kwa tahayari kama ninavyofanya sasa. Kumbuka usafi unaanza na Wewe na Mimi. La pili ni tamu hebu tuliite sukari. Wa Mombasa sisi tunajulikana kwa mahamri asubuhi, ndizi za kiume zilizokolea nazi na sukari adhuhuri, mitai au donasi alasiri na mkate wa sinia jioni. Sukari, sukari, sukari. Sukari hatari! Usihadaike! Ni mbwa mwitu aliyevaa nguo za kondoo! Sote tuna watu tunaowajua wenye maradhi kila aina sitaki kuyataja hapa, Allah atuhifadhi sote. Baada ya majaaliwa ya Allah Subhanahu wa taala, ni vyakula vya zama hizi ndivyo ambavyo hutuangamiza. Na nahodha ni huyo sukari. Jipangie kula mapochopocho haya siku za sherehe peke yake.Hivi si vyakula vya kuliwa kila siku. Swiha yako ni muhimu. Sukari si rafiki yako. Utamu wa maisha ni upendo na maskizano. Sukari si rafiki yako. La mwisho kabisa. Najifakhiri kuwa makala haya nimeyandika moja kwa moja kwa Kiswahili, si kama zamani- kuandika kwa Kiingereza halafu nikijitahidi kutafsiri. Wabillahi attawfeeq |