Paukwa pakawa. Kaondokea chenjagaa kajenga nyumba kakaa, mwanangu mwanasiti na jino kama chikichi cha kujenga ukuta na vilango vya kupita.
Fuzi na dahari zilizopita aliondokea banati mmoja mwenye urembo wa sahani. Alikuwa na uso wa kifuu cha nazi na pua ya mtepeto kama Mhabeshi. Nywele zake za julfa daima alizifunga kwa mafundo ya kupendeza na kutaanisi. Meno yake ya bisi yaligawanywa na mwanya wa haiba na mvuto. Viduta vyake vilvyosimama na kiuno chake cha nyigu ilidhihirisha wazi kuwa alikuwa mwanamke wa elfu. Kwa hakika alikuwa mfua uji mwenye umbo la shani. Wana kijiji wa Kidogobasi walimwiita kwa jina la Mwanaurembo. Naye aliitika. Kweli, mate ya nani yasiodondoka ndondondo kwa urembo tamthili hiyo?
Walakin hakuna bamvua lisilo usubi. Chini ya uzuri ule uso kifani, palikuwa na sera zilizozorota. Sio kwa kosa lake Mwanaurembo bali ilikuwa hali ya umbile lake. Alikuwa kucha kutwa yeye huharibu mazingira. Yaani, mazingira hayo ghafla huwa na harufu isioridhisha kabisa. Kwa hili, watu wengi walimuepuka. Kwa muda mrefu sana, Mwanaurembo alichelea kupata mchumba kwa ajili ya hali yake.
Mara kwa mara, zilikuja heri za kuolewa ila hazikufua dafu. Aliendelea na maisha yake huku akijaribu kukubali masaibu yake. Aila yake haikuwa na budi ila kuzoea hali hiyo. Walijaribu kadri ya uwezo wao kumtafutia tiba lakini hawakufaulu. Kwa hakika, ilikuwa vigumu kuishi saa ishirini na nne kwenye harufu isioridhisha pamoja na upweke usiokwisha.
Siku moja, ami yake alikwenda nyumbani kwao na habari njema. Alitaka mtoto wake wa kiume amuoe Mwanaurembo kwa hali yoyote ile. Wingu la furaha lilitanda na kutamalaki kote pale nyumbani. Watu walichangamka kwa bashasha fokofoko. Nyota ya jaha ilikuwa imemmulika Mwanaurembo. Alifurahi kama mvuvi aliyenasa kishazi cha samaki. Waliamua siku ya tatu yake iwe ndiyo siku ya harusi ya mrembo wao. Hawakutaka katu kusubiri muda mrefu kwasababu Mwanaurembo alishangoja wakati wa kutosha. Mwanaurembo alikuwa akishinda na tabasamu tu, ungalimuudhi vipi katika siku tatu hizo katu asingaliudhika. Siku hizo chache aliziona kama miaka. Pilka za kutayarisha sherehe zilianza. Hakuchi, kwacha. Hatimaye yaumu hiyo iliyosuburiwa kwa hamu na ghamu ilifika.
Ukumbi ulijaa shangwe, nderemo, vigelegele, vifijo, chereko na kayaya za ndani kwa ndani. Vicheko vilipamba moto jari moja. Watu walisalimiana kwa furaha na farahani. Vyakula vya kunoga viliandaliwa kwa ustadi na wapishi wajuzi. Ilikuwa tafrija ya kukata na shoka, sikwambii ya ndovu kumfanya mwanawe kitoweo. Ukumbi ulirembwa kwa maua anuwai kifani. Si asmini si waridi. Mashangingi na vitangabari viliegeshwa hapo mbele huku adinasi si kalili wakijumuika kushuhudia harusi kati ya waja hao wawili. Kwanza, aliingia bibiharusi. Kila aliyehudhuria alisimama na kutupa macho kwenye mwango mkuu. Alitembea mtindo bak bandika bak bandua hadi kwenye kiti chake cha kifahari. Kila mmoja ukumbini mle aliweka mkono karibu na uso wakidai kuwa wanajihami maana wakati wowote tu hali ya hewa ingebadilika. Kwa Mwanaurembo ilikuwa jambo la kawaida. Tendo hilo halikumuudhi wala kumliza.
Muda wa kuchakulo kunawia yake mate, bwanaharusi aliwasili kwa mbwembwe akiwa amevalia joho jeusi. Shingoni alikuwa kavishwa koja la haja lilojaa asmini na vilua. Uso wake ulijaa wasiwasi na wahaka. Taratibu alitembea pamoja na dadake huku familia yake ikiwafuata nyuma kwa vigelegele. Akakaa kwenye kiti kizuri kilichoko kando ya kile cha mkewe . Mwanaurembo huku akitabasamu alienuka na kumpokea mumewe. Kisha wakaka chini. Zawadi zilianza kuletwa. Kila kitu kilikuwa shwari. Punde tu, Mwanaurembo alionekena kuwa na wasiwasi. Alianza kuyumbayumba. Alimwita mamake na kumuashiria kitu ambacho waliohudhuria hawakukielewa. Mamake alishika tama huku akiangalia chini.
Baada ya mwia kichele, hali ya mazingira ilianza kubadilika. Wale waliokaribu na mhusika walinyayuka taratibu na kuondoka. Hali ile iliendelea kubadilika. Watu walifunika pua zao kwa mikono. Wengine walitumia vitambara. Walianza kuondoka mmojammoja wengine walikuwa wakishauriana na kuondoka kwa makundi. Loh! Harufu ilizidi kuenea. Mazingira yale yaliokuwa meupe pepepe, yalibadilika kuwa samawati, kisha hudhurungi, ikaenda kuwa nyekundu na hatimaye meusi. Kulikuwa hakukaliki tena. Ukumbi ulibaki nusu ya aila yake tu. Bwanaharusi alikuwa tayari keshakunja uso huku ameizuia pua yake kwelikweli. Masikini Mwanaurembo, alikuwa amejizuia muda mrefu mpaka akashindwa ikabidi ayatoe mabomu yakufautilizana pasi na radhi yake. Aliendelea kupaka rangi mazingira yale. Mumewe alibaki kinywa achama. Aliduwaa waa na kubung’aa ng’aa. Alishindwa kabisa na kutoroka kwenye ukumbi ule.
Hatimaye, alibaki yeye na mama yake tu. Ulikuwa wakati mgumu sana kwake. Aibu aliyoipata, katu asingeweza kuisahau. Walirudi nyumbani wakiwa na huzuni tele. Hawakudhaniya kuwa siku ile ingegeuka na kuwa vile. Juhudi zao walizozifanya zote zilipotelea nyongo. Mwanaurembo hakuwa amekula siku nzima kabla ya siku hiyo. Pia, ilimbidi avae mabinda matatu ili kuzuia harufu isitoke nje. Tatu, alijibidiisha kujikaza kwa mda mrefu ila mwishowe alishindwa. Liandikwalo na Mola halifutiki. Ndio majaaliwa yake. Mumewe alituma ujumbe kuwa asingeweza kukaa naye hivyobasi ashamuacha. Wingu la simanzi lilitanda nyumbani kwao.
“ Sitaki tena kuolewa!” Mwanaurembo alisema kwa huzuni ya sakafu ya moyo wake.
“La! Usiseme hivyo mwanangu. Usikate tamaa. Haya yote ni mitihani kutoka kwa MwenyeziMungu. Kila jambo lina mwisho. Tuombe Mungu.” Alimjibu mamake huku akimliwaza.
Tukio hilo lilikuwa gumzo kijijini Kidogobasi na hata vijiji vilivyo karibu. Mwanaurembo aliona haya sana hakuweza hata kutoka nje. Baada ya muda wa takriban miezi kadhaa maneno yale yalianza kupotea. Maisha ya Mwanaurembo yakaanza kurudi kama kawaida.
Miaka ilisonga, umri nao ukazidi kuwa mkubwa. Wenzake walikuwa tayari washaolewa na wamezaa watoto. Akatokea kijana mmoja aliyeguria kijijini huko kwa minajili ya kazi. Kijana alionekenwa kuwa mwenye heshima. Mwanamume mwenye misuli tinginya na mtanashati kwelikweli. Kama ilivyo ada, alipomuona Mwanaurembo tu, moyo ulianza kuenda mbio. Akashangazwa sana kuwa kufikia umri ule banati huyo hajaolewa wala hajapata mchumba. Alianza kumuulizia kupitia jamaa wa mitaani na bila shaka taarifa aliipata kamili. La kustaajabisha, hakuliona kama pingamizi. Au pengine hakuelewa fika kina cha masaibu yale. Aliamua kuchukua hatua nyengine.
Moja kwa moja alienda hadi kwa wazazi wa Mwanaurembo. Alieleza nia na madhumuni ya ujio wake. Wazazi nao wakamueleza kinagaubaga mitihani aliyonayo binti yao. Bila kusita, kijana huyo alisema yupo tayari kumpeleka jijini Nairobi kumsaidia kwa matibabu ima akubali au hata akikataa amuoe. Eh! Hawakuamini walichokisikia. Kwa haraka mwanaurembo aliitwa na kuelezwa yote yaliyozunugumzwa. Hakuonekanwa kuwa na furaha sana kwani aliamini fika kuwa hali yake isingeweza kubadilika. Alikubali kuolewa na kijana yule. Kulifanywa harusi ndogo sana na baada ya harusi hiyo walisafiri kuelekea jijini Nairobi kwa matibabu.
Safari ilikuwa ya kipekee. Hawakueza kusafiri kwa basi la kawaida kama watu wengine kwani walijuwa wazi wangewatorosha abiria wote kwenye basi hilo. Iliwabidi wakodishe gari la kipekee. Kulingana na hali ya mkewe pamoja na uchumi wa nchi yao dereva wa gari hilo alilipwa pesa chungu nzima. Wakati wote huo Mwanaurembo alikuwa bado hajaamini kinachoendelea. Aliona ni kama ndoto. Alishindwa namna ya kueleza furaha yake. Mumewe naye, alikuwa akimpa moyo Mwanaurembo kuwa kwa uwezo wa Jalali,mambo yatakuwa mazuri. Ilifika wakati na mumewe alianza kusema,
“ Wala harufu sio mbaya hiiivyo! Mimi hata sisikii harufu mbovu kamwe.”
Mwanaurembo alishangaa sana baada ya kusikia maneno hayo. Alikatambua wazi kuwa mumewe kampenda bila pingamizi. Waama, ukipenda chongo utaita kengeza.
Walifika jijini Nairobi na kumuona daktari aliyehusika na mambo yale. Daktari aliwaeleza kuwa angesaidika iwapo atatumia dawa alizoandikiwa pamoja na upasuaji mdogo sana aliotakiwa kufanywa. Waliyatimiza yote hayo huku wakiwa na hamu ya matokeo. Mambo yalikuwa mazuri. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Mwanaurembo alikaa mda wa masaa nane bila kuharibu mazingira. Furaha iliyoje! Aliyatupa mabinda yake yote. Mumewe naye hakuweza kuficha furaha aliyonayo. Walirudi kijijini Kidogobasi kwa raha na starehe. Kila mmoja alifurahia hali mpya ya Mwanaurembo. Huo ndio ulikuwa mwisho wa masaibu ya mwanamke huyu wa shani. Ama kweli, zito hufuatwa na jepesi na hakuna dhiki wa dhiki.