“Kwako mpendwa,
Salamu zikufikie, Hujambo? Mda mrefu sasa tokea nishtakiwe kwa kosa la uhaini. Nipo gerezani ila sijui ni gereza gani . Nimesokomezwa kwenye chumba kilicho na giza totoro. Hakuna ninachoona isipokuwa matumaini ya kufa angalau nisitirike na mateso yanayonikumba humu. Sijui nilihusikaje haswa na kuuwawa kwa waziri mkuu. Naskia alipatikana amechomwa kisu akiwa ndani ya ikulu kwenye chumba cha maakuli. Kwa kuwa kisu kilichokuwa kimetumiwa kilikuwa ni cha jikoni, nilijipata matatani na kukamatwa mie, mpishi wa waziri mkuu. Hivi nashindwa kuelewa, kwa maana nilikuwa nimepewa barua ya mapumziko ya wiki moja wakati wa tukio. Isitoshe nilikuwa nyumbani nikimsaidia binti yangu kufanya kazi za ziada alizokuwa amepewa shule.
Ilikuja mijitu yenye miraba minne na kuvunja mlango wa nyumba yangu. Nilifungwa kwa kamba kisha nikashindiliwa matambara mdomoni nisipate kutoa hata sauti.wakati uo huo, nyumba yangu ilipekuliwa na kuvurugwa kila kipembe. Kilichokuwa kikitafutwa sina ufahamu ila walibeba baadhi ya karatasi na visu kutoka jikoni mwangu kama vidhibitisho.
Tabu baada ya tabu ziliniandama.Haya yote ya uongo nimezuliwa na kuwekewa. Maskini we!…Nimlilie nani anisikie? Nitoe kafara gani nisiumie? Au ni kwa kuwa nilijenga nyumba bila kuwataarifu wazazi na mizimu inaniandama?
Kisha nimesikia… nimesikia ya kwamba watanipiga risasi mbele ya hadhira, pale Wayo stadium. Lakini kabla ya hapo nitamwagiwa siafu mwili mzima waniume na kunitafuna polepole. nawaskia walio nje ya chumba nilimosukumizwa na kukomelewa kana kwamba nimekua masih dajal au joka hatari lenye vichwa saba na kutema cheche za moto. Wanabishana kuhusiana na mbinu gani muafaka ambayo ingeweza kutumiwa kunitesa mshenzi kama mimi.
“kapten, …si uniruhusu nimcharaze kwa nyahunyo, huyu ni nyang’au mkubwa…tena hatari kwa usalama wa taifa”
“wachana na yeye kwanza, baadae nitamwosha kwa maji ya pili pili. Sisi ndisi vidume tunaoendesha serikali na amebonyeza pabaya mno. Majuto ni halali yake ama kweli.” Waliendelea kujinaki huku najitia hamnazo kana kwamba yasemwayo hayanihusu ndewe wala sikio.
walinzi hawa hufarahia kunipiga na kunitesa. Pengine inwapa pumbazo kidogo na uhalisia wa maisha yanayowapata. Kwani si ni wawa hawa wanaolipwa mishahara ya kinyonge? Si ni hawa tu juzi walikua wanalalamika kuhusu masuala ya nyumba duni wanazoishi? Eti watu wanne wagawanye chumba kimoja cha nyumba ya bati. Nawadharau na kuwaona kama kinyaa. Tena kinyaa kibichi mtaroni. Silii tena wanaponicharaza kwa majifimbo ya muarubaini. Nawacheka kwa upimbi wanaoudhihirisha. Wananilazimisha niwataje wale walio husika katika mauaji ya waziri mkuu. Nitataja vipi watu nisiowafahamu? Jamani! taasubi yangu ya kiume imeshushwa hadhi. Juzi wamepitiliza kiwango cha kunipiga, wamenicharaza mpaka haja ikanitoka pande zote mbili.
Ratiba ya jinsi nitakavyokumbana na mauti ishatoka. Daktari mkuu wa serikali amekwisha ithibitisha. Nililetewa nitie sahihi kuwa nimeridhia, lakini ukweli ni kwamba iwe nimeridhia au sikuridhia ratiba hio bado tu ningeuwawa, kama si kwa mtutu basi ni kwa hali duni ya maisha humu ndani. Shehe Magwira amepangiwa aje kuniombea siku moja kabla ya kuuwawa kwangu. Naapa kutomsikiza wala kuitikia amina dua zake. Nitamtemea kohoo zito usoni mwake ajute kwa nini amekuja nilimo. Shehe gani huyu? Anajihusisha na siasa, anapokea hongo, na riba ndio uchumi wake. Ilikuwaje mashahidi katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya ubakaji wakafa mmoja baada ya mwengine kwa njia za kutatanisha? Na si mwishowe kesi ilitupiliwa mbali? Ashazini na wanawake wangapi? Simhukumu hata kidogo ila sikubaliani na falsafa zake za kimsingi. Nitampaka kinyesi kibichi anuke sawia na roho yake.
Dini iko moyoni mwangu, nitasali kwa mola wangu na ataniskia. Sitaki aje mtu mchafu wa roho ila msafi wa lebasi kuniombea. Kama nitachomwa siku ya kiyama basi huyu shehe atanitangulia. Baada ya shehe, amepangwa mwanasheria mkuu wa serikali aje anisomee haki zangu. Nilicheka kwa kejeli niliposoma hii sehemu ya ratiba. Nashindwa kuelewa falsafa ya walioko kwenye usukani wa hili taifa. Hivi wana utimamu uliokamilika? Sidhani, lazima itakua kuna skrubu kama mbili au tatu ambazo ziko regerege kwenye mabongo yao. Kama itatokea waniachie nakala ya katiba basi nitaikojolea irowame kweli kweli, kisha niichane vipande visivyopungua mia elf. Kipengele cha bill of rights ndicho nitakachoanza kukichanilia mbali. Hivi haya yote ninayopitia humu gerezani ni haki?
Kama kweli haki ipo basi ningepewa muda nijitetee. Mbona hukumu itolewe kwa haraka na taratibu kutofatwa kwa usawa? Na si ni juzi tu waziri Fulani ameshikwa akiwa na pesa bandia nyumbani mwake? Mlanguzi wa dhahabu bandia na takataka nyenginezo za kimagendo. Kima cha karibia shillingi bilioni moja nukta saba zimepatikana kwake. Mbali na kumfuta kazi wamemfanya nini? Eti ameundiwa kamati ya kumfanyia uchunguzi kisha jopo maalum likaundwa tena kuchunguza kamati inayomchunguza waziri huyo mbadhirifu wa mali. Kushangaza zaidi, huyu waziri ni miongoni mwa wanachama katika kamati inayomchunguza. Anapewa sitting allowance kila wakati akihudhuria kusikizwa. Hata pingu hajawai fungwa wala kutiwa korokoroni akawa rizki ya kunguni. Hajakula maharage yaliyosheheni ving’onyo. Sisi wasakatonge ndio tuko taabani, bill of rights yetu labda ni bill of plights. Huenda ikawa walikosea katika kuchapisha. Upuzi mtupu.
Nimechoka kudhulumika, nimekinai wala sina hamu ya kuendelea na maisha. Humu ndani ni kero na dhiki kwenda mbele. Jana usiku nimesikia mayowe ya mfungwa mmoja akilia asibakwe. Alimsalia mtume na kumtaja mola angalau afueni ipatikane. Sijui yaliendaje au yaliishaje maana nilijipa shughuli ya kuwauwa kunguni waliokuwa wakinishambulia kutoka kila upande. Manywele yangu yamesheheni chawa. Isitoshe yamejimelea si haba. Ukinitizama utadhani nimekua sokwe mtu. Midevu imekwenda kuoteana, mdomo wote umezibika. Mwili wangu wanata kwa jinsi jasho la kila siku linavyonichuruzika na nongo kurundikana. Ninanuka kama beberu lililo komaa. Kucha zangu nazo zimekua kama kuni au magamba ya mamba vile. Kila mara najikunakuna, ninadhohofika kiafya.
Sikuandikii barua hii ili usononeke au umlaumu mungu kwa yaliyonifika, la hasha. Nakujuza tu ili upate kufahamu uhalisia wa mambo huku niliko. Siku nitakapopigwa risasi,usiogope kunitizama ukipata nafasi. Niangalie machoni uone jinsi ushujaa unavyong’ara kupitia mboni zangu. Nikazie macho na wala usipese,tizama jinsi bongo langu litakavyomwagika baada ya kulengwa shabaha. Itizame haki itakavyokandamizwa hadharani huku umma ukishangilia kwa nderemo. Ione haki itakavyobatilishwa, ovu likafanywa jema na jema kutupiliwa mbali. Ona jinsi mwizi amefanywa hakimu kwenye mahakama na aliyeibiwa kufikishwa kizimbani kujibu mashtaka. siku hiyo, utaelewa kwa undani zaidi ile hadithi ya chui aliyepewa mamlaka ya kuwalinda mbuzi zizini. Niwie radhi, falsafa yangu mara nyingi huwa ni yenye kuwakanganya wengi. Wengi walio na uchache wa utimamu. Demokrasia inavuja damu, imenajisiwa peupe.
Nahisi kana kwamba nitakuacha na jukumu zito kimaisha nitakapoondoka hapa duniani. Swala la urithi huenda likaleta shida haswa tukizingatia hatukua tumefunga ndoa kwa kadhi. Nawaona mawifi zako wakikutenga kwa ulafi wa mali. Watajifanya kutetea haki za kaka yao na kujitia kufuata dini na sharia kali ili wakutoe kwenye urathi. Sikuwahi kuandika will lakini ilikua miongoni mwa ratiba zangu. Iwepo utatokea mgogoro, usibishane, hama na virago vyako vyote. Rudi kwenu, hukufukuzwa. Kisha mtafute Abubakar Mwavyombo, msiri na swahiba wangu, atakupa miraba sita ya dhahabu yenye takriban kama kilo nne hivi. Kauze kwa sonara utapata pesa za kujikimu wewe na mwanangu. Usigombanie mali, sitokua radhi kwa hilo…”
Nashindwa kuendelea kusoma barua hii. Ni mara ya tatu sasa imebidi nisimame kujifuta machozi na michirizi ya kamasi nyembamba. Najikaza lakini wapi! Wacha nisimame hapo kidogo. Namkumbuka vyema huyu bwana kwani alizungumziwa sana kwenye vyombo vya habari. Kwanza lile gazeti la national daily standard.
Ndio mwanzo nilikuwa nimepata uhamisho wa kazi kutoka jela ya Kodiaga na nilikua nasimamia kusafishwa kwa seli aliyokuwemo ndipo ile barua ikadondoka kutoka kwenye yale mararu. Niliwaamuru wale mahabusu waniletee nikaificha ili niisome baadae.
Niliwahi kukutana na huyu haini wakati mmoja tu wa uhai wake na kumuongelesha kuhusu yaliyomkumba.wakati huo. Barua yake hii niliiokota kwenye maguo aliyokua ameyavaa ile siku kabla kwenda kupigwa risasi. Nakumbuka alipewa mavazi mapya ya wafungwa kwani yale mararu alokuwa amepewa tokea aingizwe jela yalikua yamechanika sana.
Nailaumu nafsi yangu kwa kuuusaliti utu na kuipa kipau mbele pesa. Kwa nini niseme hivi? Natizama jinsi tunavyowagonga wana wa wenzetu kwa mijeledi na bakora za mipera kama wanyama wakati wanapozembea kufanya kazi. Nafsi inanisuta nikikumbuka yale makofi ninayowanyuka mahabusu wanapochelewa kujibu maswali yangu yasiyo na msingi mara nyengine.
Najirudi, kisha najikuna kichwa nikifikiria kwa undani. Je barua hii itamfikiaje mke wa haini? Nikionekana na makachero nikiongea na jamii yake basi huenda nikafutwa kazi na kushtakiwa kama msaidizi katika mauaji ya waziri mkuu. Vilevile nisipoipeleka mke na mtoto wake haini watadhulumika kwenye urathi.